Ujumbe wa siku ya 50 ya kuombea Miito Mitakatifu ndani ya Kanisa kwa Mwaka 2013
Miito ni alama ya matumaini yanayosimikwa katika imani ndiyo kauli mbiu inayoongoza
maadhimisho ya Jubilee ya miaka hamsini tangu Papa Paulo wa sita alipoanzisha rasmi
Siku ya Kuombea Miito Duniani, inayoadhimishwa tarehe 21 Aprili 2013, sanjari na Maadhimisho
ya Jubilee ya miaka hamsini ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican na Mwaka wa Imani.
Mavuno ni mengi lakini watenda kazi katika shamba la Bwana ni wachache.
Mama Kanisa
anatambua uhaba wa miito ya Kipadre kielelezo wazi cha imani na upendo unajionesha
katika maisha ya mtu binafsi, Parokia na Jumuiya za Kijimbo; hiki ni kipimo cha uhai
wa Familia za Kikristo. Pale ambapo kuna idadi kubwa ya miito ya kipadre na kitawa
hapo kwa hakika anasema Papa Paulo wa sita kuwa watu wanaoishi Injili kwa moyo wa
ukarimu.
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, katika ujumbe wake kwa Siku
ya Kuombea Miito Duniani kwa Mwaka 2013 anasema kuwa kila mwaka ifikapo Jumapili ya
nne ya kipindi cha Pasaka, waamini hukusanyika kwa ajili ya kuombea miito mitakatifu
ndani ya Kanisa, changamoto kwa waamini kuonesha moyo wa ukarimu. Hili ni tukio ambalo
limetoa kipaumbele cha pekee katika kuombea miito ya Kipadre na kitawa, kama chemchemi
ya tasaufi, sala na mikakati ya kichungaji inayotekelezwa na waamini.
Baba
Mtakatifu anaonesha matumaini makubwa kwa siku za usoni; matumaini ambayo yanapaswa
pia kuongoza hali halisi ya maisha kwa nyakati hizi ambazo haziridhishi na zinaonesha
mapungufu. Matumaini ya Kanisa kama ilivyokuwa kwa Waisraeli katika Agano la Kale,
walipokuwa wanakabiliana na hali ngumu ya maisha hasa nyakati zile walipokuwa uhamishoni,
walikumbuka ahadi za Mwenyezi Mungu kwa Mababa wa Imani, walionesha matumaini makubwa
kiasi hata cha kuwashangaza.
Ndivyo ilivyotokea kwa Abraham alipoambiwa na
Mwenyezi Mungu kwamba, atakuwa ni Baba wa Mataifa na kwa hakika Mungu Mwenyezi aliweza
kutekeleza Agano lake kwa uaminifu mkubwa licha ya dhambi, gharika, kukombolewa kutoka
utumwani na safari ya Waisraeli Jangwani kwa miaka arobaini.
Mwenyezi Mungu
ameendelea kuwa ni mwaminifu kwa Agano Jipya na la Milele lililofanywa na Mwanaye
Mpendwa Yesu Kristo kwa njia ya damu yake azizi; kwa kuteswa, kufa na kufufuka kutoka
katika wafu. Mwenyezi Mungu katika nyakati za shida na magumu anaonesha nguvu yake
katika historia ya ukombozi kwa kuibua watu ambao waliamsha matumaini kwamba, siku
moja wataweza kuifikia Nchi ya Ahadi. Kwa hakika Mwenyezi Mungu hawezi kuwaacha waja
wake anaendelea kuwa mwaminifu kwa neno lake. Hiki ndicho kiini cha matumaini ya Kanisa,
katika hali njema au ugumu wa maisha.
Mwenyezi Mungu anaimarisha matumaini
ndiyo maana mwamini anaweza kuimba na Mzaburi kwa kusema kwamba, moyo wangu unaweza
kupata kitulizo kwa Mwenyezi Mungu kwani tumaini lake linatoka kwake. Kuwa na matumaini
ni sawa na kujiaminisha kwa Mwenyezi Mungu ambaye ni mwaminifu ana anatekeleza Agano
lake. Imani na matumaini ni fadhila ambazo zina uhusiano wa karibu. Imani ni neno
la msingi katika Biblia kiasi kwamba wakati mwingine Imani na Matumaini yanaonekana
kuwa ni maneno yanayoweza kutumika kwa pamoja
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi
na sita, katika Ujumbe wake kwa Siku ya hamsini ya kuombea Miito Duniani kwa Mwaka
2013 anabainisha kwamba, uaminifu wa Mungu unajikita kwa namna ya pekee katika upendo
ambao ameumimina kwa njia ya Roho Mtakatifu, ukajionesha kwa njia ya Kristo na kwamba
unahitaji kupata jibu la uhakika kutoka kwa waamini ili kuweza kuishi kwa ukamilifu
zaidi. Matumaini yanarutubishwa na upendo wa Mungu kwa waja wake unaowakirimia ujasiri
na matumaini katika hija ya maisha yao, kiasi hata cha kuweza kujiamini kwa siku za
usoni, katika historia na miongoni mwa watu wengine.
Baba Mtakatifu anapenda
kuwakumbusha vijana umuhimu wa upendo wa Mungu unaojionesha tangu kuumbwa kwa ulimwengu
na utakaofikia ukomo wake nyakati za mwisho, atakapokamilisha kazi ya ukombozi. Kanisa
lina imani thabiti kwa njia ya Kristo Mfufuka anayeendelea kufanya hija ya wafuasi
wake ambao wamezama katika shughuli mbali mbali, wakiwa na matarajio na mahitaji
yao. Lakini Kristo anaendelea kuwaita na kuwakaribisha ili kuishi pamoja naye kwani
ana uwezo wa kuzima kiu ya matumaini yao ya ndani.
Yesu anaendelea kuishi
katika Jumuiya ya Waamini ambao ni Kanisa na anawaita watu kwa nyakati mbali mbali
kumfuasa. Kwa kukubali wito wake kuna maanisha kwamba, hakuna tena uwzekano wa kufuata
njia nyingine. Hiki ni kitendo cha kutoa utashi wao kwa ajili ya kutekeleza utashi
wa Kristo; kwa kutoa kipaumbele cha kwanza katika medani mbali mbali za maisha: ndani
ya familia, sehemu za kazi, na katika mambo binafsi. Ni mwaliko wa kujitoa bila ya
kujibakiza ili kuunganika na Fumbo la Utatu Mtakatifu pamoja na jirani zao. Umoja
wa maisha katika yesu ni mahali ambapo mwamini anaweza kuonja tumaini na utimilifu
wa maisha na uhuru kamili.
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita anaendelea
kusema kwamba, miito ya upadre na maisha ya kuwekwa wakfu yanapata chimbuko lake kwa
mang’amuzi ya mtu anayekutana na Yesu katika hija ya maisha yake; ni chimbuko la majadiliano
ya kweli na thabiti na Kristo, ili kuingia katika utashi wake. Ni muhimu kuendelea
kukua katika mang’amuzi ya imani, yanayofahamika kuwa ni uhusiano wa dhati kabisa
na Yesu na kuwa makini kusikiliza sauti yake inayozungumza kutoka katika undani wa
mtu.
Mchakato unaomwezesha mtu kutoa jibu chanya kwa wito kutoka kwa Mungu
unawezekana tu katika Jumuiya za Kikristo ambamo imani inamwilishwa kwa ukamilifu
kabisa; mahali ambapo ushuhuda wa ukarimu unajidhihirisha kwa kujishikamanisha na
Injili; kwa kuonesha umuhimu wa utume unaowaongoza watu kujitoa bila ya kujibakiza
kwa ajili ya Ufalme wa Mungu, kwa kulishwa na Sakramenti za Kanisa, hususan Ekaristi
Takatifu na maisha ya sala. Sehemu hii ya mwisho inapaswa kuonesha uhusiano wa mtu
binafsi na Mungu aliye hai. Kwa upande mwingine, sehemu hii haina budi kuongozwa na
Sala kuu ya Kanisa, Watakatifu na katika Sala ya Liturujia ambamo Kristo anawafundisha
waamini kusali vyema.
Baba Mtakatifu anawaalika waamini kujenga utamaduni wa
kusali daima kama njia ya kukuza imani ya Jumuiya za Kikristo kwa kuamini kwamba,
Mwenyezi Mungu kamwe hawezi kuwatupa waja wake na ataendelea kuwaongoza na kuchipusha
miito ya upadre na maisha ya kitawa kama alama ya tumaini duniani. Mapadre na Watawa
wanachangamotishwa na Mama Kanisa kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya Watu wa
Mungu, katika huduma ya upendo kwa Injili na Kanisa kwa kuhudumia tumaini linalowezekana
kwa kujiachilia wazi kwa ukuu wa Mungu.
Kwa njia ya ushuhuda wa imani na ari
katika utume, wanaweza kurithisha hasa miongoni mwa vijana wa kizazi kipya hamu ya
kujibu kwa ukarimu na kwa utayari wito wa Kristo unaowaalika kumfuasa kwa ukaribu
zaidi. Mfuasi yeyote wa Kristo anapoamua kujitoa kikamilifu katika maisha na utume
wa Kipadre au Maisha ya kuwekwa wakfu, Kanisa linashuhudia matunda ya ukomavu wa Jumuiya
ya Kikristo, inayowawezesha kuamini na kuwa na matumaini kwa Kanisa katika siku za
usoni; ili kuadhimisha Sakramenti ya Ekaristi Takatifu na Upatanisho.
Baba
Mtakatifu anawaalika Mapadre kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya kuwaongoza katika
hija ya maisha yao, kwa kuwasaidia kupambana na magumu, ili hatimaye, waweze kumtambua
Yesu ambaye ni Njia, Ukweli na Uzima. Wawaambie kwa ujasiri wa Injili inavyopendeza
kumtumikia Mwenyezi Mungu, Kanisa pamoja na kuwahudumia ndugu na jamaa zao. Wawepo
Mapadre wanaoonesha matunda ya kujitoa bila ya kujibakiza kwa kuonesha utimilifu wa
maisha yanayopata msingi wake katika Imani kwa Kristo ambaye aliwapenda upeo!
Baba
Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita anahitimisha ujumbe wake kwa Siku ya hamsini ya
Kuombea Miito Duniani kwa kuonesha matumaini yake kwamba, vijana ambao wanaoneshwa
mambo mengi kwa juu juu tu pamoja na kuwa na chaguzi nyingi katika maisha yao, wataweza
kukuza hamu ya kuwa na kitu chema zaidi, malengo thabiti na uchaguzi makini na huduma
kwa wengine kwa kumuiga Yesu.
Anawataka vijana wa kizazi kipya kutoogopa kumfuasa
na kutembea katika nyayo zake zinazohitaji kwa namna ya pekee upendo na majitoleo
ya ukarimu. Kwa njia hii wataweza kutumikia kwa furaha na kutolea ushuhuda wa ile
furaha ambayo kamwe haiwezi kutolewa na Ulimwengu; watakuwa ni mwanga wa upendo wa
Mungu na watajifunza kutoa ushuhuda wa tumaini lililoko ndani mwao!