2013-04-20 08:21:01

Siri ya furaha ya maisha na wito wa Kipadre! Yaaani, we acha tu!


Askofu mkuu Josephat L. Lebulu wa Jimbo kuu la Arusha katika mahojiano na Radio Vatican wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha Jubilee ya Miaka 50 tangu Baba Mtakatifu Paulo wa Sita alipoanzisha Siku ya Kuombea Miito Mtakatifu ndani ya Kanisa anasema; Upadre unakua na kukomaa siku kwa siku. RealAudioMP3

Upadre unarutubishwa kwa maisha ya Sala, Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa na maisha ya Kijumuiya. Padre hana budi kufurahia upadre wake na mapadre wenzake! Hii ndiyo siri ya urembo katika maisha na utume wa kipadre!

Askofu mkuu Lebulu anabainisha kwamba, katika maisha yake tangu akiwa Seminari kuu, alitamani kupata elimu ya juu, lakini anaonya kwamba, hamu na shauku hii haina budi kuratibiwa ili iweze kuzaa matunda yanayokusudiwa katika hali ya ukomoavu. Viongozi wa Kanisa walimpatia fursa ya kwenda kusoma zaidi Jijini Kinshasa na aliporudi aliendelea na maisha ya Kipadre Jimboni Same.

Anawashukuru Mapadre waliokuwa wamemtangulia katika Daraja takatifu la Upadre kwani walikuwa ni msaada mkubwa kwake kwa mwongozo na dira na mifano ya maisha. Anasema, Mapadre vijana wanapaswa pia kujifunza na kuiga mifano bora kutoka kwa Mapadre waliowatangulia. Anawashukuru pia waamini walei ambao wamemsindikiza kwa njia ya sala na kushirikiana naye katika maisha na utume wa Kanisa.

Askofu mkuu Josephat Lebulu kwa namna ya pekee anawaalika Mapadre kufurahia upadre wao na kamwe wasijutie kwa nini wamefanya uamuzi kama huu. Waendelee kuujenga na kuuimarisha kwa njia ya mahusiano mema na Mapadre na Waamini walei. Maisha ya Kijumuiya ni msaada mkubwa katika maisha na utume wa Kipadre.







All the contents on this site are copyrighted ©.