2013-04-20 10:20:30

Majadiliano ya kidini na kiekumene Barani Asia yanapania kujenga na kudumisha amani pamoja na kutafuta mafao ya wengi!


Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu, hivi karibuni amehitimisha rasmi Kongamano la Kimataifa lilikuwa linaongozwa na kauli mbiu "kulisikiliza Bara la Asia: njia za imani, jamii na dini kati ya mapokeo na usasa".

Kwa ufupi, Kongamano hili limetoa fursa kwa washiriki kuweza kutafsiri changamoto ambazo zinaendelea kujitokeza Barani Asia; umuhimu wa majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni; mang'amuzi ya imani na ushuhuda unaoweza kutolewa na waamini katika maisha ya kijamii.

Kardinali Filoni anasema kwamba, changamoto zinazojitokeza Barani Asia zinaweza kuwa chanya kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wananchi wa Asia au zinaweza pia kuwa hasi kwa kudumaza mafanikio yaliyokwisha kupatikana katika medani mbali mbali za maisha: kisiasa, kiuchumi, kijamii, kitamaduni, kisayansi na kidini.

Mambo yote haya yanapaswa kuangaliwa kwa umakini mkubwa, huku wakijitahidi kuwa wakweli na waaminifu sanjari na usomaji wa alama za nyakati, changamoto kubwa kutoka kwa Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican.

Kardinali Filoni amekazia kwa namna ya pekee majadiliano ya kidini na kiekumene, ili kukabiliana na dhana ya baadhi ya waamini kuwa na misimamo mikali ya kidini hali inayopelekea: uvunjifu wa misingi ya haki na amani; madhulumu na nyanyaso za kidini katika nchini mbali mbali Barani Asia. Watu wajitaabishe kufahamiana na kuheshimiana na kamwe tofauti zao za kidini na kiimani zisiwe ni chanzo cha vurugu na uvunjifu wa misingi ya haki na amani.

Majadiliano ya kidini na kiekuemene ni dhana inayopania kwa namna ya pekee kujenga na kudumisha misingi ya amani na utulivu; upendo na mshikamano wa kidugu, kwa kutambua kwamba, kama Jamii wanategemeana na kukamilishana. Kwa pamoja na waamini wa dini mbali mbali wanaweza kusimama kidete kupambana na baa la umaskini ambalo limekuwa ni chanzo cha kinzani na vurugu nyingi sehemu mbali mbali za dunia.

Watu wa Asia watambue na kuthamini mapokeo na utamaduni wao kama mambo msingi yanayowaunganisha badala ya kuwatenganisha. Ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia yamegusa na kutikisa hata mizizi ya imani ya wananchi wanaoishi Barani Asia. Watu wengi wamekata tamaa kutokana na umaskini wa kipato na hali, matokeo yake ni baadhi ya watu kuanza kukata tamaa na hatimaye, kutema zawadi ya maisha.

Waamini wanachangamotishwa kutolea ushuhuda wa imani yao kwa kuwajengea wananchi matumaini thabiti yanayobubujika kutoka katika imani ya dini zao na kwa namna ya pekee wakristo watambue uwepo endelevu wa Yesu kati yao!

Ushuhuda wa imani uweni mwaliko wa kujenga umoja na mshikamano; kwa kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili; kwa kusimama kidete kulinda na kudumisha: haki, amani, upendo na mshikamano wa dhati.

Kardinali Filoni anasema Imani haina budi kumwilishwa katika maisha ya kijamii ili kupambana fika na nyanyaso, ubaguzi na madhulumu; utu na heshima ya binadamu vipewe kipaumbele cha kwanza. Waamini wa dini na madhehebu mbali mbali washirikiane kwa dhati kwa ajili ya ujenzi wa nchi yao; daima wakitafuta mafao ya wengi ili kujenga na kuimarisha Jamii inayowajibika barabara kwa watu wake. Wananchi wajifunze kuvuka vikwazo na kujenga madaraja ya ushirikiano na mshikamano katika nyanja mbali mbali za maisha.








All the contents on this site are copyrighted ©.