Baraza la Maaskofu Katoliki Ureno linaangalisha kwamba, familia ni tunu ambayo haina
mbadala ni chemchemi na mhimili mkuu wa nguvu kazi: kiroho, kijamii na kiuchumi kwa
taifa lolote lile. Ni taasisi nyeti na ambayo inapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza.
Katika kukabiliana
na athari za myumbo wa uchumi kimataifa, kuna haja kwa Jamii kuonesha mshikamano wa
dhati na familia ili ziweze kutekeleza wajibu na dhamana yake katika Kanisa na Jamii
kwa ujumla wake. Mshikamano huu ujengeke kati ya vijana wa kizazi kipya na wazee ambao
ni hazina kubwa katika Jamii na kamwe wasiwatenge na kuwabeza.
Mshikamano
huu ni muhimu sana hasa kwa wale watu ambao amepoteza fursa za kazi kutokana na athari
za myumbo wa uchumi kimataifa na kwa sasa wanakabiliana na hali ngumu ya uchumi. Changamoto
hii imetolewa hivi karibuni na Baraza la Maaskofu Katoliki Ureno katika mkutano wake
wa Mwaka uliofanyika mjini Lisbon.
Mshikamano wa upendo uanzie ndani ya Familia
yenyewe kwa ndugu na jamaa kusaidiana na hatimaye kuvuka mipaka na kuwagusa majirani
na Jamii katika ujumla wake. Familia za Kikristo zinaalikwa kwa namna ya pekee kuwa
kielelezo cha upendo na mshikamano na wale wote walioathirika kutokana na myumbo wa
uchumi kimataifa. Sera na mikakati ya kuinua uchumi nchini Ureno imegonga mwamba kwani
taasisi za fedha na uzalishaji zilijikita katika kutafuta faida kubwa wakasahau kuwekeza
katika Familia na matokeo yake ni kuzorota kwa ulaji na utoaji wa huduma za kijamii.
Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, katika ujumbe wake kwa Maadhimisho
ya Siku ya Amani Duniani kwa Mwaka 2013, alionya kwamba, katika kipindi cha miaka
ya hivi karibuni, kumeibuka ubinafsi, ulaji wa kutisha na sera nyingi za kiuchumi
zinatafuta faida kubwa hata kwa gharama ya maisha ya watu. Kumekuwepo na ushindani
usiokuwa na tija na matokeo yake ni kuzorota kwa uchumi.
Maaskofu Katoliki
Ureno wanakumbusha kwamba, mafanikio yanapatikana kwa kufanya kazi kwa juhudi, akili
na maarifa. Mshikamano wa kidugu na mafao ya wengi ni mambo yanayopaswa kupewa msukumo
wa pekee katika sera na mikakati ya maendeleo endelevu inayozingatia mahitaji ya mtu
mzima: kiroho na kimwili. Familia ziwe ni kitovu cha upendo, kwa watu kukaribishana
na kusaidiana.
Viongozi watambue kwamba, madaraka waliyo nayo ni dhamana ambayo
wamekabidhiwa na umma kwa ajili ya kutoa huduma ya upendo na mshikamano hasa kwa maskini
na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii. Hawa ndio wagonjwa, wazee na wote wenye
kuhitaji msaada kutoka katika Jamii. Viongozi wahakikishe kwamba, wanatumia vyema
rasilimali ya nchi ili kuleta maboresho katika sekta ya elimu, afya na maendeleo endelevu.
Maaskofu
Katoliki Ureno wanasema kwamba, ili Familia iweze kutekeleza wajibu wake barabara
katika Kanisa na Jamii, haina budi kuheshimiwa, kuthaminiwa na kuwezeshwa kwa hali
na mali. Takwimu za hivi karibuni zinaonesha kwamba, Ureno ni kati ya nchi zenye idadi
ndogo sana ya watoto wanaozaliwa duniani. Kuna mwingiliano mkubwa kati ya idadi ya
watu na uhusiano wa kijamii.
Kuna haja ya kuwekeza zaidi katika Familia si
katika hali ya kujisikia, bali kwa kujitoa kimasomaso kwa ajili ya ustawi na maendeleo
ya Familia. Kwa hakika wanasema Maaskofu Katoliki wa Ureno kuna haja ya kuwekeza pia
katika Injili ya Uhai.