2013-04-20 09:43:06

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lajadili kuhusu: wanawake, amani na usalama


Askofu mkuu Francis Chullikatt, mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Umoja wa Mataifa, hivi karibuni ameshiriki katika mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lililojadili kuhusu wanawake, amani na usalama.

Anasema, tangu mwaka 2000 Umoja wa Mataifa umekuwa ukifuatilia kwa umakini mkubwa kuhusu mchango wa wanawake katika kujenga na kudumisha misingi ya haki na amani, jambo linalohitaji kuwajengea wanawake uwezo mkubwa zaidi ili kuweza kukabiliana na changamoto mbali mbali katika Jamii zao.

Wanawake wakiwezeshwa wanaweza kusaidia kuzuia vita, kujenga msingi wa upatanisho na maridhiano ya Kijamii na kwamba, wao ni wadau wakuu na vyombo vya amani duniani.

Askofu mkuu Chullikatt anasema inasikitisha kuona kwamba, bado wanawake wengi wanatumbukizwa kwenye utumwa mamboleo, nyanyaso za kijinsia, biashara haramu ya binadamu pamoja na matumizi haramu ya dawa za kulevya. Wanawake ni waathirika wakuu katika kinzani za kikabila, kiuchumi na kisiasa na kidini. Baadhi ya watu wanaofanya vitendo hivi wakati mwingine wanatoka kwenye Serikali, Vyombo vya Ulinzi na Usalama au kwenye Majeshi ya kulinda amani ya Umoja wa Mataifa.

Hivi ni vitendo vinavyodhalilisha utu na heshima ya binadamu na kwamba, kuna baadhi ya Jamii na Makundi ya watu wametumia vitendo hivi kama silaha ya vita. Ujumbe wa Vatican kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa unamesisitizia umuhimu wa kuzuia vitendo vya uvunjaji wa sheria; kwanza kabisa kwa kuhakikisha kwamba, sababu ya vita na kinzani za kijamii zinabainishwa na kutafutiwa ufumbuzi wa kudumu, kwani vita vingi ni kutokana na hali ngumu ya kiuchumi na kijamii. Kuna haja ya kuwekeza katika elimu, maadili na utu wema pamoja na kuwa na mwono sahihi kuhusu dhana ya wanawake katika Jamii.

Wahusika wa vitendo hivi vya jinai wanapaswa kuchukuliwa hatua madhubuti kwa kufikishwa kwenye mkondo wa sheria, ili haki iweze kutendeka. Pale ambapo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linahusika moja kwa moja, basio hatua za haraka ziweze kuchukuliwa kwa kuzingatia haki na usawa na wala si kusukumwa na sababu za kisiasa mambo ambayo yanaweza kukwamisha juhudi za Umoja wa Mataifa katika kupambana na vitendo vinavyodhalilisha utu na heshima ya binadamu.

Waathirika wa vitendo hivi wanapaswa kupewa fidia jambo ambalo halikubainishwa kinaga ubaga kwenye taarifa ya Umoja wa Mataifa katika mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Waathirika wahudumiwe kwa dhati ili kuponya undani wa madonda haya yanayoacha kurasa chungu katika maisha ya waathirika wa vitendo vya dhuluma za kijinsia. Jumuiya ya Kimataifa ijali na kuheshimu zawadi ya uhai na kamwe isikimbilie kutoa ushauri unaokumbatia utamaduni wa kifo kwa kisingizio cha mimba zisizotarajiwa.

Mama na mtoto wake ambaye bado yuko tumboni wahudumiwe, wasaidiwe na kupatiwa elimu, ushauri pamoja na kupatiwa huduma mbali mbali zitakazomsaidia Mama na mtoto wake: kiroho na kimwili. Pale inapowezekana juhudi zifanyike kutafuta familia itakayoasi mtoto anayezaliwa katika mazingira magumu na dhuluma za kijinsia, kwani maisha ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Askofu mkuu Francis Chullikatt, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Umoja wa Mataifa anahitimisha mchango wa ujumbe wake kwenye mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa kutaka Jumuiya ya Kimataifa kuwekeza zaidi katika kulinda na kudumisha misingi ya haki na amani miongoni mwa Jamii na kwamba, amani ya kweli inabubujika kutoka katika moyo wa mwanadamu. Jamii ijifunze kuenzi zawadi ya maisha kwa kusimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima ya kila binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.







All the contents on this site are copyrighted ©.