2013-04-19 16:15:01

Ukame wa kutisha na vita nchini Mali ni chanzo kikuu cha kuenea kwa baa la njaa nchini Mali


Kwa muda wa miaka minane, wananchi wanaoishi katika Ukanda wa Sahel wameendelea kukabiliana na baa la njaa wakati wote huu na kwamba, hakuna matumaini ya kuweza kujikwamua na hali hii kwa siku za hivi karibuni. Kuna zaidi ya watu millioni 10.3 wanakabiliwa na ukosefu wa uhakika na usalama wa chakula.

Hali hii ni mbaya zaidi nchini Mali ambayo kwa miezi ya hivi karibuni imeshuhudia kinzani na machafuko ya kisiasa yaliyopelekea watu wengi kuyakimbia makazi yao kwa kuhofia usalama maisha na mali zao. Hayo yamo kwenye taarifa iliyotolewa na Shirika lisilo la Kiserikali lijulikanalo kama "Action Contre la Faim". Kuna watoto wadogo wanaokabiliwa na utapia mlo wa kutisha.

Uhaba wa mvua ya kutosha na vita inayoendelea nchini Mali ni kati ya vikwazo vikubwa vinavyowakwamisha wananchi wengi kujihusisha na shughuli za uzalishaji wa mazao mashambani. Kuna zaidi ya wananchi wa Mali 450, 000 ambao hawajawa tayari kurudi majumbani mwao kutokana na hofu ya vita kuendelea bado kutanda nchini humo.

Hali ya wakimbizi inaendelea kuwa mbaya kutokana na mahitaji makubwa ya fedha kwa ajili ya kununulia chakula, dawa, malazi pamoja na utoaji wa huduma msingi za kwa wakimbizi hawa.







All the contents on this site are copyrighted ©.