Kardinali Antonio Maria Veglio', Rais wa Baraza la Kipapa la wahamiaji na watu wasiokuwa
na makazi maalum, anaungana na Jumuiya ya Wanasarakasi Kimataifa katika Maadhimisho
ya Siku ya Nne ya Sarakasi Kimataifa, hapo tarehe 20 Aprili 2013 chini ya udhamini
wa Mtoto wa Mfalme Stephanie wa Montecarlo. Hayo yamo kwenye ujumbe ambao Kardinali
Veglio' amemtumia Dr. Urs Ilz, Rais wa Shirikisho la Wanasarakasi Ulaya na Duniani
katika ujumla wake.
Anawashukuru wote waliowezesha kufanikisha tukio hili ambalo
linawakusanya Wanasarakasi kutoka pembe mbali mbali za dunia na hivyo kuvuka vikwazo
vya kitamaduni na kijamii, ili kujenga Jumuiya moja ya Kimataifa. Maadhimisho haya
ni changamoto kwa watu wenye mapenzi mema kukuza na kudumisha mshikamano wa kidugu,
ushuhuda unaotolewa na kuhifadhiwa kwa namna ya pekee na Jumuiya ya Wanasarakasi.
Ni
Maadhimisho yanayoonesha umoja na majadiliano; uwazi na ukarimu mambo yanayowagusa
watu wenye umri tofauti wanaounda Jumuiya hii na kuwa ni sehemu ya utambulisho na
wito wake. Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, Mwezi Desemba 2012 alipata
nafasi ya kukutana na kuzungumza na Wanasarakasi wa Kimataifa mjini Vatican, aliwapongeza
kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa familia, watoto wadogo, watu wenye ulemavu; huduma
kwa wagonjwa pamoja na kuwathamini wazee kama sehemu ya amana na urithi mkubwa katika
mafanikio ya michezo yao.
Ni Jumuiya inayojikita katika majadiliano ya kina,
urafiki na mshikamano wa kazi kama timu moja Huu ndio utajiri na amana inayooneshwa
na Wanasarakasi kutoka sehemu mbali mbali za dunia katika Maadhimisho ya Siku ya Nne
ya Sarakasi Kimataifa. Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, kwa wakati
ule aliwapongeza kwa weledi na ufanisi mkubwa wa shughuli zao kimichezo, jambo ambalo
linahitajika hata katika ulimwengu mamboleo.
Kardinali Veglio' anasema kwamba,
Mama Kanisa anatambua mchango wa Wanasarakasi, lakini kwa namna ya pekee, vikundi
vinavyoendelea kuchangia kwa hali na mali katika kuwasaidia watu waliofikwa na: vita,
maafa pamoja na majanga kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Vikundi hivi vimekuwa
ni faraja kwa watoto, wazee, kiasi cha kuwakirimia na kuwaonjesha amani na utulivu
wa ndani, furaha na upendo.
Baba Mtakatifu Francisko, katika mahubiri mwanzo
wa utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro alikazia umuhimu wa waamini kuwa ni
vyombo vya matumaini mapya, kwa kulinda, kuheshimu na kutunza kazi ya uumbaji, ili
kuendeleza; heshima, urafiki na mafao ya wengi. Kanisa linawaangalia Wanasarakasi
kwa moyo wa matumaini kutokana na ukweli kwamba wanajitahidi kutumia karama na vipaji
vyao kwa ajili ya ujenzi wa Jumuiya ya Kimataifa na mshikamano wa dhati kati ya watu
na Jamii zao.