2013-04-19 15:39:28

Rais wa Ecuador akutana na kuzungumza na Papa Francisko mjini Vatican


Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 19 Aprili 2013 amekutana na Rais Rafael Vicente Correa Delgado kutoka Ecuador pamoja na ujumbe wake na baadaye Rais Delgado amekutana pamoja na ujumbe wa Kardinali Tarcisio Bertone Katibu mkuu wa Vatican mjini Vatican.

Mazungumzo baina ya viongozi hawa wawili yamefanyika katika hali ya urafiki na maelewano na kwamba, wamepongeza mchango wa Kanisa katika medani mbali mbali za maisha nchini Ecuador. Wamekazia umuhimu wa Kanisa katika kuendeleza mchakato wa majadiliano ili kuiwezesha Serikali iweze kukabiliana na changamoto mbali mbali katika maisha ya kijamii.

Baba Mtakatifu pamoja na mgeni wake wamekazia kwa namna ya pekee kabisa kuhusu haki jamii, umuhimu wa mshikamano wa kidugu unaoongozwa na kanuni auni katika harakati za kutafuta mafao ya wengi. Viongozi hawa wawili wamepembua kwa kina na mapana kuhusu umuhimu wa kuwathamini na kuwajali wazawa katika utamaduni na mapokeo yao sanjari na utunzaji bora wa mazingira.







All the contents on this site are copyrighted ©.