Papa asema ameguswa na mahangaiko ya wanawake wa Argentina
Baba Mtakatifu Francisko anasema yuko karibu na akina mama wote waliopoteza watoto
na wapendwa wao wakati wa utawala wa kidikteta wa nchini Argentina. Anawataka wanawake
wa Argentina kupiga moyo konde, kuwa na ujasiri na matumaini mapya katika maisha yao
na anawaomba kwa namna ya pekee kusali pia kwa ajili ya maisha na utume wake kama
Khalifa wa Mtakatifu Petro.
Ni ujumbe ulioandikwa kwa niaba ya Baba Mtakatifu
Francisko na Monsinyo Antoine Camilleri,Katibu mwambata anayeshughulikia uhusiano
wa kimataifa mjini vatican kama jibu la barua kutoka kwa wanawake wa Argentina wanaojulikana
kama "Madri di Plaza de Mayo".
Baba Mtakatifu anawaalika wanawake wa Argentina
kumsindikiza katika utume wake na kwa namna ya pekee, aweze kuchangia kwa katika mchakato
wa kupambana na baa la umaskini duniani pamoja na kuleta faraja kwa wote wanaoteseka
kiroho na kimwili.
Baba Mtakatifu katika ujumbe huu anawapongeza wale wote
wanaojitosa katika mchakato wa kuwajengea maskini uwezo ili kukabiliana na changamoto
mbali mbali za maisha; ni vyema kufahamu matatizo yao, kuwaelewa na kuwasaidia kupata
ufumbuzi wa changamoto hizi pale inapowezekana.
Baba Mtakatifu anawataka viongozi
wa Jumuiya ya Kimataifa kujifunga kibwebwe kutafuta kwanza kabisa mafao ya wengi pamoja
na kupambana kufa na kupona dhidi ya umaskini, kwa kutumia njia muafaka zinazojali
usawa na mshikamano wa kidugu.