Mtumishi wa Mungu Padre Nicolo' Rusca kutangazwa kuwa Mwenyeheri
Kardinali Angelo Amato, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la kuwatangaza waamini kuwa
wenyeheri na watakatifu, tarehe 21 Aprili, 2013, Jumapili ya nne ya Kipindi cha Pasaka,
maarufu kama Jumapili ya Kristo mchungaji mwema, kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko,
anatarajia kumtangaza Mtumishi wa Mungu Padre Nicolo’ Rusca kuwa Mwenyeheri katika
Ibada ya Misa Takatifu itakayofanyika kwenye Kanisa la Sondrio mahali ambako kwa miaka
thelathini aliwahudumia waamini kama Kasisi mkuu.
Wakati wa
machafuko ya kidini kati ya Wakatoliki na Madhehebu ya Kipentekoste katika miaka ya
1600, alikamatwa, akafungwa na kuteswa sana gerezani na hatimaye, akauwawa kikatiliki
kutokana na chuki za kidini dhidi ya Imani ya Kanisa Katoliki. Akimwelezea Mwenyeheri
Padre Nicolo’ Rusca, Baba Mtakatifu Francisko anasema kwamba, ni kiongozi na mchungaji
mwema, aliyejitoa bila ya kujibakiza, akatekeleza wajibu na utume wake wa kuwahudumia
Kondoo wake mintarafu mapenzi ya Kristo, kiasi hata cha kuyamimina maisha yake kwa
ajili ya imani kwa Kristo na Kanisa lake.
Mwenyeheri Padre Nicolo’ Rusca alizaliwa
kunako mwaka 1563 huko Canton Ticino, Kaskazini mwa Italia. Baada ya karne nne, Mama
Kanisa ametambua ushujaa, ari na imani thabiti na sasa anamtangaza kuwa ni Mwenyeheri
kama sehemu ya mchakato wa kumtangaza kuwa Mtakatifu wakati utakapowadia kama kielelezo
cha imani thabiti. Miaka mingi imepita, lakini bado watu wengi wanamkumbuka kutoka
na utakatifu wa maisha ambao kamwe haukuweza kupitwa na wakati.
Kardinali
Amato anasema kwamba, Mwenyeheri Padre Nicolo’ ni kielelezo cha mwamini ambaye alijitoa
bila ya kujibakiza, akasimama kidete kutolea ushuhuda wa imani yake kwa Kristo na
Kanisa lake kwa njia ya madhulumu. Jambo hili linaonesha maana na umuhimu wa mwanga
wa imani na ile kiu ya kutaka kufahamu ukweli kuhusu Mwenyezi Mungu. Hata katika matukio
ya kibinadamu, Mwenyezi Mungu anaendelea kujifunua kwa watu wake, ili waweze kuutambua
na kuushuhudia ukweli.
Mwenyeheri Padre Nicolo’ ameuwawa kutokana na chuki
za kidini, changamoto kwa waamini wa dini mbali mbali kujenga na kudumisha misingi
ya haki, amani, upendo na mshikamano. Kwa pamoja waendeleze majadiliano ya kidini
na kiekumene, kwa kujikita katika upatanisho wa kweli unaojionesha kwa namna ya pekee
katika maisha ya waamini wenyewe.
Watu wajenge utamaduni wa kuheshimiana,
kuthaminiana na kusaidiana wakitambua kwamba, wote wameumbwa kwa sura na mfano wa
Mungu, tofauti zao za kidini ziwe ni cheche ya upendo na mshikamano wa dhati. Wakristo
washikamane kutangaza Habari Njema ya Wokovu kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao pamoja
na kujitahidi kuvunjilia mbali kuta za utengano ambazo bado zinaendelea kuleta ukakasi
katika maisha.
Kardinali Angelo Amato anakumbushia kwamba, watakatifu ni mashujaa
wa imani waliyotolea maisha yao kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. Ni mashujaa wanaoendelea
kuwachangamotisha waamini kutambua na kuthamini uwepo wa Mungu katika hija ya maisha
yao ya kila siku: Waoneshe jambo hili kwa njia ya ushuhuda wa maisha adili, manyofu
na matakatifu. Kila mwamini anaalikwa kuwa ni Mtakatifu.