2013-04-19 10:07:52

Kristo ndiye mchungaji mwema!


Ni siku nyingine tena tunakutana katika kushirikishana Neno la Mungu Neno ambalo ni kiunganishi cha maisha kati yetu na Baba wa mbinguni. Tunaendelea katika safari ya furaha ya Pasaka, tayari tuko Dominika ya IV ya Pasaka. RealAudioMP3

Kama kawaida Dominika ya IV ya Pasaka ni Dominika ya mchungaji mwema, Dominika ya kuombea miito katika Kanisa. Jambo la kwanza Mama Kanisa anatualika kusali kwa ajili ya miito na pili kuijenga kuanzia ngazi ya familia hadi kanisa la ulimwengu. Ujumbe wa Baba Mtakatifu juu ya miito unatumbusha kwamba, miito ni alama ya matumaini yanayosimikwa katika imani.

Baada ya kupokea ujumbe wa Papa tunasonga mbele tukiuunganisha na Neno la Mungu likitufundisha nia ya Mungu ya kututaka sisi tukue katika kujitoa kwa mapendo zaidi, mapendo ambayo yanadai mabadiliko ya ndani, kinyume na Wayahudi ambao kadiri ya Neno la Mungu wanakwamisha mafundisho juu ya Neno la Mungu. Hata hivyo kwa kuwa Bwana na Baba yake ni wamoja na nguvu yao yapita kila aina ya nguvu basi wapinzani hawataweza kulishinda Neno la Mungu na mafundisho yake.

Katika somo la kwanza Mtakatifu Paulo na Mtakatifu Barnaba wako katika safari ya kimisionari na wanatenda kazi ya Bwana wakiongozwa na nguvu ya ufufuko. Katika ufanisi wa kazi hiyo wanakumbana na vikwazo mbalimbali na mojawapo ni upinzani toka kwa Wayahudi. Wanafanyiwa fitina na kukatishwa tamaa, lakini kwa kuwa wamejitoa kiaminifu na wakijitafiti wajibu wao mbele ya Mungu wanakaza kamba na kusonga mbele.

Bwana yu pamoja nao, kama kawaida kwani mtenda kazi ya Bwana hakosi msaada na nguvu ya Mungu. Nasi basi mpendwa kazi ya uinjilishaji katika ulimwengu wa leo inao upinzani na hata wakati fulani upinzani usi ona miguu wala mikono! Kumbe, wajibu wetu katika hali hii kwanza ni kukaa chini na kutafakari kwa kina nini maana ya alama hiyo, na kisha kutoa jibu lililojaa upendo wa kimungu ndani mwake. Jambo moja la kutuongoza ni kwamba sisi tu watu wake na kondoo wa malisho yake na hivi lazima tumtegemee mchungaji wa kondoo.

Sehemu ya Injili ya Mt Yohane inatufundisha juu ya upendo wa Mungu kwa wanadamu. Kawaida sura ya 10 ya Injili ya Yohane ni tafakari juu ya mchungaji mwema. Kwanza mchungaji mwema ni Bwana wetu Yesu Kristo ambaye anazo sifa zote za mchungaji mwema, sifa ya kwanza ikiwa ni kuwajua kondoo wake wote, yaani kujua shida zao, mahitaji yao na wema wao.

Jambo jingine muhimu ni lile pia la kuwafundisha waziwazi anachotaka, alivyo yeye mwenyewe, kumbe ni mwalimu ambaye anataka wanafunzi waweze kuwa na maarifa ya kumtambua mwalimu wao. Hii ni alama ya upendo, ni alama ya kuondoa ubaguzi na mipaka katika muunganiko wetu na Bwana. Bwana anasema nao wanijua mimi!.

Lengo la Bwana katika fundisho hili ni kutaka kusema lazima watu wote wafikie uzima wa milele, kamwe hata mmoja asipotee. Katika hili Bwana anasema watu ninaowajua mimi ni wale ambao amenipa Baba yangu, kumbe yeye na Baba yake wako wamoja na lazima atimize mapenzi ya Baba yake.

Mpendwa, unayenisikiliza, katika Somo la Pili tunapata kumwona Mtakatifu Yohane yuko katika maono, anaona mkutano mkubwa ukizunguka kiti cha enzi na kila mwanamkutano amevaa mavazi meupe na anayo majani ya mitende. Mara moja anauliza ni nani hawa na mzee anajibu ni wale waliofua mavazi yao katika mwanakondoo, na sasa Mwanakondoo yuko katikati yao.

Mpendwa, Mtakatifu Yohane anataka kutuonesha matunda ya kazi ya kimisionari ambayo tutayapata hapo baadaye. Wale walio na mavazi meupe maana yake ni wale waliokubali kuishi mapendo kamili, mapendo ya ndani wakiongozwa na Bwana ambaye daima yuko nasi kwa njia ya Neno lake na kwa njia ya Sakramenti zake.

Ni wale ambao Bwana aliwajua sauti za ona wao wakajua sauti yake na hivi wanafurahi naye katika kiti cha enzi cha mbinguni. Wanafurahi na Mchungaji mwema ambaye hapotezi hata kondoo mmoja cha msingi ujue sauti yake na kumfuata.

Mpendwa, hawa ndugu ambao wanamzunguka mwanakondoo wanoneshwa katika alama ya mavazi meupe, ikiwa ni ishara ya furaha na utu wema. Katika kipindi cha Pasaka mama kanisa amechagua mavazi meupe akiashiria furaha tuipatayo kutoka ufufuko na ukiwa ni mwaliko wa furaha ya milele. Matawi ya mitende ni alama ya ushindi baada ya kazi yao nzito hapa duniani. Nawe katika maisha yako fanyeni yote vema na mbeleni kuna ushindi na vigelegele mbinguni.

Mpendwa, ndiyo kusema njaa na kiu ya haki hapa duniani tuiishiyo haitakuwepo mbinguni, kumbe mateso kama sehemu ya imani yetu yana mwisho tunapokutana na Bwana katika kiti chake cha enzi.

Mpendwa mwana wa Mungu ninakualika daima kuiga mfano wa Mt. Paulo kuvumilia magumu na matukano yatokanayo na imani, na ukisha vumilia yote sasa utaifuata sauti ya Mchungaji mwema itujiayo kila siku kwa njia ya Kanisa na mwisho kuna zawadi ya uzima wa milele.
Tumsifu Yesu Kristo.
Tafakari hii imeletwa kwako na Padre Richard Tiganya C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.