2013-04-19 08:38:50

Hali ya usalama bado ni tete sana mjini Bangui


Askofu mkuu Dieudonnè wa Jimbo kuu la Bangui, Jamhuri ya watu wa Afrika ya kati anasema, machafuko ya kisiasa nchini humo yanaendelea kutishia usalama wa maisha na mali za watu. Kwa sasa kuna idadi kubwa ya wahamiaji wasiokuwa na makazi wamekimbilia kwenye Hospitali ya Bangui kwa ajili ya kupata hifadhi.

Askofu mkuu Dieudonnè anasema hali ni mbaya kwani watu hao waliokimbilia hospitalini hapo wanahitaji huduma muhimu ambazo kwa sasa hazipatikani. Wanasema, lengo lao ni walau kupata hifadhi ya maisha yao. Katika kundi hili, wengi wao ni wanawake, watoto na wazee.

Shirika la Misaada la Kanisa Katoliki nchini humo, Caritas linaendelea kutoa msaada wa hali na mali, lakini wanaanza kuzidiwa na idadi kubwa ya watu wanaohitaji msaada kutokana na vita ya wenyewe kwa wenyewe inayoendelea nchini humo na baadhi ya wanajeshi kuanza kupora mali za watu.

Hali ya usalama bado ni tete Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati, kiasi kwamba, Waziri mkuu Bwana Nicolas Tiangaye ameomba msaada wa kijeshi kutoka Ufaransa, ili kusaidia kulinda na kudumisha amani nchini humo. Wananchi wanaoishi mjini Bangui wanaendelea kusikia mirindimo ya risasi na mabomu kiasi kwamba, wanakosa amani na utulivu.

Askofu mkuu Nzapalainga anasema, kinachomsikitisha zaidi ni kuona jinsi ambavyo watoto wadogo, akina mama na wazee wanavyoteseka kwa kukosa msaada. Baadhi ya vituo vya kulelea watoto yatima navyo pia vimeporwa na kuharibiwa vibaya.

Kanisa litaendelea kukazia misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano, watu wanapaswa kutambua kwamba, vita ni kwa ajili ya maangamizi ya mwanadamu na hakuna amani ya kudumu inayoweza kupatikana bila ya majadiliano, kwa kuheshimu na kuthamini utu wa mwanadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, kwa hakika amani ni jina jipya la maendeleo.







All the contents on this site are copyrighted ©.