Tokeni kifua mbele kumtangaza na kumshuhudia Kristo Mfufuka!
Mama Kanisa anawajibu na dhamana ya kuwakuza na kuwalea watoto wake katika misingi
ya imani, maadili na utu wema, tayari kutoa ushuhuda wa imani hii kwa Kristo na Kanisa
lake; wakitoka kifua mbele kwenda kutangaza Habari Njema ya Wokovu, ili watu waweze
kumfahamu, kumpenda na kumtumikia Kristo, ili siku moja waweze kufika kwake mbinguni.
Huu ndio muhtsari wa tafakari ya kina iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko
katika Maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu iliyofanyika kwenye Kikanisa cha Domus
Sanctae Marthae na kuhudhuriwa na Wafanyakazi wa Benki ya Vatican. Itakumbukwa kwamba,
tangu Baba Mtakatifu alipochaguliwa kuwa Khalifa wa Mtakatifu Petro ameendelea bado
kuishi na kusali na waamini mbali mbali kwenye Kikanisa cha Domus Sanctae Marthae
kama sehemu ya kufahamiana pia na wafanyakazi mbali mbali wanaotoa huduma mjini Vatican.
Mwanzoni, Wakristo wa mwanzo walibahatika kuishi kwa amani, umoja na upendo
kati yao, wakishirikishana na kumegeana utajiri wa Neno la Mungu na kazi ya mikono
yao. Lakini madhulumu yalipoanza kujitokeza, walijikuta wakisambaratika sehemu mbali
mbali za dunia ya wakati ule na huu ukawa ni mwanzo wa Uinjilishaji wa Mataifa. Baba
Mtakatifu Francisko anakumbusha kwamba, daima Kanisa limeendelea kujengeka na kuimarika
katika misingi mikuu mitatu: amani, upendo na madhulumu.
Ni wakristo waliokuwa
wamebatizwa na kuimarishwa kwa njia ya Roho Mtakatifu, waliojitosa ulimwenguni ili
kuwainjilisha walimwengu, wakati ambapo Mitume wa Yesu na viongozi wengine wa Kanisa
walikuwa mjini Yerusalemu wakipambana na dhuluma hizi mbele ya viongozi wa Serikali.
Wakristo walikuwa wamebeba ndani mwao amana ya imani, iliyowafanya kuaminiwa na wenyewe
kuwa na uwezo wa kutenda miujiza na watu wengi wakajazwa furaha ya kusikia Habari
Njema ya Wokovu ikitangazwa masikioni mwao.
Ile nguvu ya Ubatizo na Roho Mtakatifu
viliwajaza Wakristo wa mwanzo ujasiri wa pekee kabisa, kiasi kwamba, wakachangamotishwa
Kuinjilisha kwa ari na moyo mkuu. Neno la Mungu katika kipindi hiki cha Pasaka kuhusu
maisha ya Wakristo wa kwanza, liwe ni changamoto ya kutoka kwa ujasiri kutangaza Injili
ya Kristo kwa maneno, lakini zaidi kwa njia ya ushuhuda wa maisha, daima wakijitahidi
kuwa ni waaminifu kwa Kristo, Roho Mtakatifu na Kanisa.
Baba Mtakatifu anaonya
kwamba, Kanisa si kama "Babysitter" aliyepewa dhamana ya kubembeleza mtoto na hatimaye,
kusinzia na kulala usingizi mzito. Wakristo wamepewa dhamana na wajibu wakati walipopokea
sakramenti ya Ubatizo, changamoto iliyoko mbele yao ni kutekeleza wajibu na dhamana
hii kwa ari na ujasiri mkuu.