2013-04-18 10:21:05

Kanisa halina budi kuwa na sera na mikakati inayolenga kuimarisha shughuli za kimissionari kwa ajili ya Uinjilishaji


Baba Mtakatifu Francisko ameandika ujumbe kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Argentina wanaoendelea na mkutano wao wa mwaka, unaotarajiwa kufungwa rasmi hapo tarehe 20 Aprili 2013 kwa kuwataka kuweka sera na mikakati ya kichungaji yenye mwelekeo wa kimissionari, daima wakifanya rejea kwenye hati za Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Amerika ya Kusini uliofanyika mjini Aparecida, "kutweka hadi kilindini".

Baba Mtakatifu anaomba msamaha kwa kutoweza kuhudhuria kwenye mkutano wa Baraza la Maaskofu Katoliki Argentina kutokana na majukumu aliyokabidhiwa hivi karibuni na Mama Kanisa. Kwa namna ya pekee, anawataka Maaskofu kuonesha ujasiri wa kutoka ndani na kuwaendelea wale waliotawanyika sehemu mbali mbali za Argentina, watu wenye kiu na hamu ya kutaka kukutana na Yesu kristo Mkombozi wa Ulimwengu.

Kanisa linalojiangalia lenyewe limepitwa na wakati, changamoto kwa viongozi wa Kanisa wakishirikiana na waamini kutweka hadi kilindini ili kuweza kukabiliana na changamoto zinazoendelea kujitokeza katika ulimwengu wa utandawazi uliosheheni ukanimungu pamoja na mmong'onyoko wa maadili na utu wema. Ni wakati kwa Mama Kanisa kujifunga kibwebwe na kujitosa ulimwenguni ili kuwainjilisha walimwengu, waone na kuonja utamu wa Injili.

Baba Mtakatifu anahitimisha ujumbe wake kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Argentina kwa kuwaomba waendelee kumwombea katika maisha na utume wake; ajifunze zaidi na zaidi kusikiliza kile ambacho Mwenyezi Mungu anataka kwa ajili ya Kanisa lake na wala si kwa ajili ya kutekeleza matakwa yake binafsi.

Wakati huo huo, Baraza la Maaskofu Katoliki Argentina katika mkutano wake wa Mwaka linabainisha kwamba, ili kuweza kuleta mageuzi ya kweli katika mfumo wa haki, kuna haja ya kufanya tafakari ya kina, itakayowashirikisha wadau mbali mbali, ili kila mtu kwa nafasi na dhamana yake aweze kuchangia mawazo kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi nchini Argentina. Mambo haya hayana budi kugusa: Haki, Demokrasia na Katiba ya Nchi ambayo kimsingi ni sheria Mama.

Rais Cristina Fernandez Kirchner wa Argentina amekwisha toa maelekezo ya muswada wa sheria unaopaswa kufanyiwa mabadiliko makubwa nchini humo ili watu kwa njia ya kidemokrasia waweze kuonana na wadau wa sheria, mawaziri na watumishi wengine wa Serikali: Ukweli na uwazi katika utekelezaji wa majukumu ya mahakama; uwezekanao wa wananchi kupima ufanisi wa mihimili mikuu ya nchi yaani: Bunge, Mahakama na Serikali.

Baraza la Maaskofu Katoliki Argentina linasema kwamba, haya mambo yanapaswa kuangaliwa kwa umakini mkubwa vinginevyo demokrasia inaweza kugeuzwa kuwa ni uwanja wa fujo na vurugu za kijamii.







All the contents on this site are copyrighted ©.