2013-04-18 07:57:44

Changamoto kwa vijana wa kizazi kipya kutoka Jangwani kwenye utupu ili kumkimbilia Kristo!


Jangwa ni mahali pakavu, mahali pasipo na maji, mahali pasipo na mmea, mahali pasipo na watu, ni mchanga na vumbi tupu. Usiombe rafiki yangu ukajikuta jangwani. RealAudioMP3
Yaani hakuna tumaini, ni mahangaiko kila kona, ukijikuta mahali pa namna hii na hauna mpango wa kuondoka jangwani hapo basi fahamu kuwa kifo kimebisha hodi. Na iwapo unaendelea kujifanya ngangali na kubaki hapo, ufungue usifungue kifo kitakusomba msobemsobe.
Najua woga umekuingia, unajiuliza tunaelekea wapi na mada hii leo. Jipe moyo mtu wangu, huu si unabii wa maafa, ukiisikia sauti yangu hewani basi jua nakuletea ujumbe wenye tumaini, nakuletea uzima. Na leo ujumbe wangu kwako kijana ni huu: toka jangwani penye imani haba uingie katika nchi ya uzima ya ufalme wa mwana wa Mungu. Basi karibu sana ndugu msikilizaji katika kipindi cha vijana leo.
Mnamo 2005 katika Misa yake ya kwanza akiwa Khalifa wa Mtakatifu Petro, Baba Mtakatifu staafu Benedikto wa kumi na sita, aliwaalika wachungaji na waamini wote kuongoza safari kutoka jangwani kuelekea mahali palipo na uhai, kwa yule anayetupatia uzima, tena uzima tele. Safari hii tunaihitaji sana, na haswa ndio lengo la mwaka huu wa imani. Kuinuka na kuvumbua upya safari ya imani yetu. Kutoa mwanga zaidi unaolenga kukuza furaha na ari mpya ya kukutana na Kristo. Leo tutafakari hiyo sehemu ya kwanza ya kuvumbua safari hiyo na kuelekea penye uzima, halafu juma lingine tutatafakari kule kukutana na Kristo.
Kijana unajikuta jangwani pale ambapo humwamini Mwenyezi Mungu, au pale ambapo imani yako ni ya juu juu tu. Unababaisha babaisha katika kuamini kwako. Labda huendi kabisa Kanisani kusali, ama ukienda hausali kwa moyo, mawazo na moyo wako vinakuwa pengine kabisa. Haushiriki kikamilifu katika shughuli mbali mbali kikanisa. Hujitoi kikamilifu. Pengine umeacha au hauna kabisa utaratibu wa kusali pamoja nyumbani.
Unategemea zaidi watu na vitu vingine kuliko kumtegemea Mungu. Umejiachia katika maisha ya starehe na dhambi na kujikuta umejiwekea vizuizi kupokea Ekaristi Takatifu. Umekuwa mtu wa dhuluma, rushwa, ulaghai, umbeya, uongo, uchonganishi na uovu wa aina mbali mbali. Iwapo upo katika hali yeyote ya namna hii basi tambua kuwa upo jagwani, hauna uzima ndani yako na hautaupata iwapo utabaki hivyo.
Lakini kama una penda uzima, badilika sasa, tafakari vema juu ya maisha yako na chukua uamuzi wa kubadilika. Ungama na mrudie Bwana wako. Anza kuishi kikamilifu imani yako ya kikristo. Anza safari yako ya ukombozi. Safari hii ya kutoka jangwani siku zote ni ngumu na utasongwa na vishawishi vingi. Kila unapopiga hatua utashawishika kurudi tena kwenye mazoea yako ya awali. Pengine utajisikia kushawishika kuonja kidogo tu, mara ya mwisho halafu basi; utashawishika kusema aaah.. mbona wengine wanafanya, tena wanazidi kufanikiwa kwa mtindo huo.
Usidanganyike rafiki yangu, hautakuwa na uzima kwa mtindo huo. Haya mambo ya dunia ni ya kupita, nasi tupo tu safarini, tupo katika hija kuelekea mbinguni penye uzima tele. Na ukianza kuishi kwa imani thabiti ndani ya Kristo, utaupata uzima huo ungali hapa duniani. Badilika, chukua hatua. Anza safari yako kumwelekea Kristo, mwokozi na rafiki yako wa kweli.
Safari za jangwa namna hii unahitaji sana uaminifu katika Sala, kusoma, kulitafakari na kulimwilisha Neno la Mungu, kusoma ya kujitahidi kuyafahamu Mafundisho tanzu ya Kanisa, kusikiliza mawaidha ya viongozi wetu kiroho, kupokea Sakramenti, kutubu mara kwa mara, kuongea na mababa wa kiroho na wakubwa wanaoweza kukushauri vema. Toka jangwani mpwendwa, twende kwa Bwana, twende kwenye uzima.
Mpaka juma lijalo tena. Karibu tena utege sikio Studio za Radio Vatican, ni sauti ile ile ya kinabii ikuleteayo tumaini na faraja, Padre Celestine Nyanda.








All the contents on this site are copyrighted ©.