2013-04-17 10:06:44

Vyombo vya mawasiliano ya kijamii visaidie kujenga na kuimarisha utamaduni wa haki na amani


Signis ni Shirikisho la Vyama vya Mawasiliano vya Kanisa Katoliki Duniani, lililoanzishwa kunako mwaka 2001, lakini linahistoria yake inayofanya rejea hadi kwenye miaka 1928.

Hili ni Shirika ambalo linawaunganisha wanachama wake katika imani na utamaduni wa amani; ili kusimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu; kwa kudumisha misingi ya haki, amani na upatanisho. Hadi sasa lina wanachama kutoka katika nchi 140 kwa kuwashirikisha wanachama wanaofanya utume wao katika Radio, Luninga, Sinema pamoja na njia nyingine za kisasa za mawasiliano ya jamii.

Lengo la Signis ni kushirikiana na wanataaluma hawa, ili kumwilisha mwanga wa Injili katika tamaduni mbali mbali, ili kuwajengea watu uwezo wa kusimama kidete kulinda na kutetea haki, amani, upendo, msamaha na upatanisho, mchakato ambao unawashirikisha vijana kwani hawa ndio wadau wakuu wa matumizi ya njia za mawasiliano.

Katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni Mashariki ya Kati imekuwa ni Uwanja wa vita, kinzani na migogoro ya kijamii, kielelezo kwamba, jamii inataka mabadiliko ya kisiasa. Lakini watu wanahitaji pia kujenga na kudumisha utamaduni wa majadiliano, upatanisho, haki na amani. Hizi ni kati ya changamoto ambazo zinaendelea kuwakabili wananchi wanaotoka Mashariki ya Kati.

Mji mkuu wa Beirut, Lebanon, ni mahali ambapo kuna mkusanyiko mkubwa wa vijana wenye ndoto na matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi. Hapa ndipo Signis imeamua kuadhimisha mkutano wake mkuu utakaoanza hapo tarehe 20 hadi tarehe 23 Oktoba, 2013, wakiongozwa na kauli mbiu "Vyombo vya habari kwa ajili ya utamaduni wa amani, kutengeneza taswira kwa kushirikiana na kizazi kipya".

Signis inabainisha kwamba, kwa kuadhimisha mkutano wake mkuu wa mwaka mjini Beiruit, wanapenda kuonesha mshikamano wao wa dhati kwa wananchi wa Mashariki ya Kati ambao wanakabiliana na hali ngumu ya maisha kutokana na machafuko ya kisiasa yanayoendelea kusababisha maafa makubwa. Signis inataka kuwajengea vijana wa kizazi kipya matumaini ya utamaduni wa majadiliano, haki na amani pamoja na kusimama kidete kulinda na kudumisha haki msingi za binadamu.

Akizungumza na waandishi wa habari hivi karibuni, Askofu mkuu Claudio Maria Celli, Rais wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano ya Jamii anaipongeza Signis kwa uamuzi huu wa busara unaotambua na kuthamini mchango wa vyombo vya mawasiliano ya jamii katika ujenzi wa utamaduni wa amani duniani. Hii ni changamoto pia kuendeleza majadiliano ya kidini ili amani na utulivu viweze kutawala huko Mashariki ya Kati, kwa kuheshimu ukweli na haki sawa kwa wote.

Askofu mkuu Claudio Maria Celli anabainisha kwamba, Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, kwa kutambua na kuthamini mchango wa njia za mawasiliano ya kisasa katika jamii, anawaalika waamini kufanya tafakari ya kina kuhusu umuhimu wa maendeleo haya ya sayansi na teknolojia ya habari kama jukwaa la Uinjilishaji Mpya. Mitandao ya Kijamii inawakutanisha mamillioni ya watu kwa muda mfupi kabisa, kumbe, kuna haja kwa watu kuhakikisha kwamba, wanatumia mitandao hii kwa ajili ya maendeleo endelevu ya binadamu: kiroho na kimwili.







All the contents on this site are copyrighted ©.