2013-04-17 07:40:16

Ujenzi wa Kituo cha Familia Takatifu Kimataifa waanza


Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili katika Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani iliyofanyika mjini Rio de Janeiro kunako mwaka 1997, alisema kwamba, angependa kukumbukwa katika uongozi wake kama mtu ambaye alijitoa kimasomaso kwa ajili ya kulinda na kutetea tunu bora za maisha ya kifamilia. Hapo wazo la kuanzisha Kituo cha Familia Kimataifa mjini Yerusalemu, likakua na kuanza kushika kasi taratibu.

Wazo hili likamwilishwa na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, kunako tarehe 14 Mei 2009 wakati wa hija yake ya kichungaji kwenye Nchi Takatifu; siku hiyo akaweka jiwe la msingi pale mjini Galileya. Ujenzi ukaendelea kushika kasi na kwa namnaya pekee wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Saba ya Familia Kimataifa iliyofanyika Jimbo Kuu la Milano, mwezi juni 2012, mradi huu ukawa umeanza kutekelezwa rasmi.

Baraza la Kipapa la Familia likaukabidhi mradi huu kwa Mheshimiwa Salvatore Martìnez, Rais wa Chama cha Kitume cha Uamsho wa Roho Mtakatifu nchini Italia.

Haya yamesemwa na Askofu mkuu Vincenzo Paglia, Rais wa Baraza la Kipapa la Familia katika uzinduzi wa Kituo cha Familia Takatifu Kimataifa mjini Yerusalemu kitakachokuwa ni mfano na kielelezo cha ujenzi na uimarishaji wa tunu msingi za maisha ya kifamilia.

Hapa watu wataweza kuchota kutoka katika chemchemi ya Familia Takatifu, tasaufi ya maisha ya kifamilia, mikakati ya kichungaji ya familia na kituo maalum cha kuonesha mshikamano wa upendo na familia ambazo zinakabiliana na hali ngumu ya maisha: kiroho na kimwili.Huu ni mwendelezo wa mikakati ya Baraza la Kipapa la Familia linalotaka kuwekeza zaidi katika majiundo ya maisha bora ya kifamilia, ili familia ziweze kusimama kidete kulinda na kutetea dhamana na utume wao ndani ya Kanisa na Jamii kwa ujumla.

Askofu mkuu Vincenzo Paglia anasema Familia inapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza, kwa kuhakikisha kwamba, Familia inapata fursa ya kusoma, kutafakari na kulimwilisha Neno la Mungu katika matendo ya huruma. Kwa maneno mengine, Neno la Mungu linapaswa kuwa ni kiini cha maisha ya kifamilia. Bila kuwa na familia madhubuti, Jamii itaweza kuyumba sana.

Kwa bahati mbaya, katika ulimwengu wa maendeleo ya sayansi na teknolojia na utandawazi familia imekuwa ni kati ya taasisi zinazokabiliwa na kinzani kutoka kila upande, na matokeo yake, familia nyingi zimejikuta zinaogelea katika migogoro na hali ya kukata tamaa kiasi cha kushindwa kutekeleza dhamana na wajibu wake barabara.

Kwa upande wake, Dr. Salvatore Martìnez wakati anazungumza na Waandishi wa Habari amebainisha kwamba, mradi huu unapania kumwilisha kwa namna ya pekee, Mafundisho ya Kanisa kuhusu Familia, ili kujenga na kuimarisha tunu bora za maisha ya kifamilia, kiutu na kijamii, ili familia za Kikristo ziweze kujitosa kimasomaso katika azma ya Uinjilishaji mpya hasa katika Nchi Takatifu. Kwa maneno mengine Kituo cha Kimataifa cha Familia Takatifu kinapania kuwa ni "Injili ya Familia Kimataifa".

Ujenzi wa Kituo cha Familia Takatifu Kimataifa unatarajiwa kukamilika katika kipindi cha miaka miwili na nusu, ikiwa kama mambo yote yatakawenda kama ilivyopangwa kwa gharama ya Euro millioni kumi na mbili. Pamoja na kuwa na vyumba vya mikutano kimataifa; Kituo hiki pia kitakuwa na Kikanisa chenye uwezo wa kuketisha watu mia tano. Kituo pia kitakuwa na vyumba mia moja kwa ajili ya kutoa hifadhi kwa familia zitakazokuwa zinafanya hija ya maisha ya kiroho kwenye Nchi Takatifu.

Dr. Martìnez anasema kwamba, kwa hakika Kituo cha Familia Takatifu Kimataifa kitakuwa ni mahali muafaka kabisa pa uenezaji wa Injili ya Familia Kimataifa. Tukio hili limehudhuriwa na viongozi mbali mbali wa Kanisa kutoka katika Nchi Takatifu waliokuwa hapa mjini Vatican.

Uamuzi wa Baraza la Kipapa la Familia kuwekeza katika Nchi Takatifu ni changamoto ya kuendelea kuchota tunu msingi za maisha ya kifamilia kutoka katika Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu, ili kujenga na kuimarisha misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano wa dhati, kwa kutambua kwamba, Familia ni chombo cha kwanza cha kulinda na kutetea amani.







All the contents on this site are copyrighted ©.