2013-04-17 08:11:55

Mshikamano wa upendo na wananchi wa Zimbabwe na Afrika ya Kusini


Askofu Declan Lang wa Jimbo Katoliki Clifton, Uingereza, hivi karibuni amehitimisha hija ya kichungaji ya juma zima, nchini Zimbabwe na Afrika ya Kusini, ili kujionea mwenyewe uhai wa imani miongoni mwa Wakristo katika nchi hizi mbili, lakini kwa namna ya pekee nchini Zimbabwe ambako wananchi wake wanajiandaa kwa uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu.

Anasema, nchini Zimbabwe, Baraza la Maaskofu Katoliki Zimbabwe limefanya kazi kubwa katika kuhamasisha utawala bora, haki, amani na upatanisho wa kitaifa, kama inavyojionesha kwenye Waraka wao wa kichungaji uliotolewa hivi karibuni, kwa kuonesha kwa kina na mapana njia ambayo kimsingi inapaswa kufuatwa na wananchi wa Zimbabwe, wanasiasa na wapenda amani ili nchi iweze kuwa na amani, utulivu na maendeleo endelevu.

Askofu Declang Lang anasema, akiwa nchini Afrika ya Kusini amejionea mwenyewe uhai wa Kanisa katika kuhamasisha maendeleo endelevu pamoja na ushiriki wa Kanisa katika medani mbali mbali za kijamii. Amefurahishwa na uhai wa Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo, huduma kwa watoto yatima, wagonjwa wa Ukimwi, wenye ulemavu, maskini na wale wanaoishi katika mazingira hatarishi. Huduma hizi zinatolewa kwenye Jimbo kuu la Capetown, Afrika ya Kusini.

Kuna uhai mkubwa wa imani, kwani akiwa Jimbo kuu la Harare ameshiriki na kuona jinsi ambavyo waamini walivyokuwa wanaishuhudia imani yao katika Maadhimisho mbali mbali ya Ibada ya Misa Takatifu. Kwa hakika anasema Askofu Declan Lang wa Jimbo Katoliki la Clifton kwamba, kushiriki kwake katika maisha na utume wa Kanisa Barani Afrika wakati wa Kipindi cha Pasaka, limekuwa ni tukio la pekee kabisa katika maisha na utume wake.







All the contents on this site are copyrighted ©.