Imani kwa Kanisa na umuhimu wake katika maisha ya kijamii
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican inaendelea kukuletea ujumbe wa Baraza la Maaskofu
Katoliki Tanzania katika kipindi cha Kwaresima sanjari na Maadhimisho ya Mwaka wa
Imani. Leo tunaangalia kuhusu: Imani kwa Kanisa na umuhimu wa kuipyaisha imani hiyo.
Imani kwa Mungu
na kwa Neno lake 1. “Nasadiki kwa Mungu mmoja”. Msingi wa imani yetu ni Mungu katika
Nafsi Tatu; yaani, Baba, Mwana na Roho Mtakatifu. Mungu anayetupatia zawadi ya imani
anatutaka tumtolee shukrani kwa kuiishi zawadi hii tukiwa tumeunganika naye katika
Utatu wake Mtakatifu. Katika Injili ya Yohane, Yesu alipowaasa wafuasi wake wasikitendee
kazi chakula kiharibikacho (Rej. Yn 6: 27) wao waliuliza wakitaka kujua wafanye nini
basi: “Tufanyeje ili tupate kuzitenda kazi za Mungu?” (Yn 6:28). Hili ni swali ambalo
tunaweza kulifanya kuwa letu katika kipindi hiki cha Mwaka wa Imani, na bila shaka,
katika maisha yetu yote. Yesu anawajibu akisema: “Hii ndiyo kazi ya Mungu: mmwamini
yeye aliyetumwa na yeye” (Yn 6:29). Humo ndimo ulimo utimilifu wote wa mpango wa Mungu
anayejidhihirisha katika Utatu Mtakatifu. “Kukiri imani katika Utatu Mtakatifu – Baba,
Mwana na Roho Mtakatifu – ni kuamini katika Mungu mmoja ambaye ni Upendo (rej. 1 Yn
4:8): Baba, ambaye katika utimilifu wa wakati alimtuma Mwanae kwa ajili ya wokovu
wetu; Yesu Kristo, ambaye kwa fumbo la kifo chake na ufufuko aliukomboa ulimwengu;
Roho Mtakatifu, ambaye analiongoza Kanisa katika karne zote tunaposubiri ujio mtukufu
wa Bwana.”
2. Imani kwa Mungu inakuwa ni tendo linalotuinua kupitia tendo la
“utii wa imani”: “Utii wa imani lazima apewe Mungu anayejifunua (Rum 16:26; taz. Rum
1:5; 2Kor 10:5-6). Kwa imani mwanadamu hujikabidhi kikamilifu na kwa uhuru mikononi
mwa Mungu, akitoa kwa Mungu mwenye kufunua “heshima kuu ya akili na utashi”, na akikubali
kwa hiari ufunuo anaopewa na Yeye. Ili imani hii iweze kutekelezwa, mtu hana budi
kutanguliwa na kusaidiwa na neema ya Mungu. Kadhalika hana budi kuwa na msaada wa
ndani wa Roho Mtakatifu anayesukuma moyo na kumwelekeza kwa Mungu, na anayefunua macho
ya akili na anayewapa “watu wote utamu katika kuukubali na kuuamini ukweli”. Roho
Mtakatifu huyohuyo hukamilisha imani daima, kwa njia ya mapaji yake ili ufunuo ueleweke
kwa undani zaidi.”
3. Neno la Mungu linabaki kuwa ni msaada usiopimika unaotusaidia
kung’amua kujifunua huku kwa Mungu. Imani yetu katika Kristo hulishwa kwa neno la
Kristo mwenyewe. “Imani, chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la Kristo”
(Rum 10:17). Neno la Mungu linailisha imani yetu na kutupatia hakikisho la kile tusichokiona
na kukigusa sasa kupitia milango yetu mitano ya fahamu. Imani inakuwa ni mlango wa
sita wa fahamu ulio na umuhimu wa juu kwani inatusaidia kutamani yale ambayo jicho
halijapata kuona wala sikio kusikia (Rej. 1Kor 2:9). “Kwa maana kwa moyo mtu huamini
hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu” (Rum 10:10).
Imani
kwa Kanisa 4. “Nasadiki kwa Kanisa moja, takatifu, katoliki na la mitume”. Kanisa
linabaki kuwa “Mama na Mwalimu” wa imani na ni chombo cha kimungu kinachowaunganisha
watu na Mungu na baina yao. Kwa sababu hiyo Mt. Ireneo wa Lione anatukumbusha kuwa,
“Lilipo Kanisa, yupo Roho wa Mungu: alipo Roho wa Mungu lipo Kanisa na neema zote.”
Kwa maneno mengine ndio kusema, lilipo Kanisa la kweli lililoanzishwa na Kristo juu
ya msingi wa Mitume hapo imani ya kweli ipo, kwa sababu, “Kanisa la Mungu aliye hai”,
ni “nguzo na msingi wa kweli” (1Tim 3:15). Hata hivyo, ilipo imani hazikosekani changamoto.
Kwa sababu, “hatusadiki tu kwa Kanisa, bali wakati huo huo sisi nasi ni Kanisa.” Tunatambua
wazi kwamba huku kuwa Kanisa ni safari ya wongofu. Ni safari ya wongofu kwa kuwa ndani
ya Kanisa wadhambi na watakatifu wanapata nafasi, lakini wote wakialikwa kukua katika
njia ya wongofu. “Kanisa … ambalo huwakumbatia wakosefu ndani yake, na wakati uleule
ni takatifu na linahitaji kutakaswa, haliachi kamwe kutubu na kujitengeneza upya.” 5.
Safari yetu ya kukua katika imani ndani ya Kanisa inaifanya nafasi ya Kanisa kwa wokovu
kuwa ni ya muhimu sana. Umuhimu wake unatokana na ukweli kwamba lenyewe ni Mwili wa
Fumbo (Kol 1:18) wa Kichwa ambaye ni Kristo mwenyewe. Ndiyo maana, Kanisa “ni mwezi
wa kweli. Kutoka katika mwanga usiokuchwa wa nyota ya kidugu, linapata mwanga wa umilele
na wa neema. Kimsingi, Kanisa haliangazi mwanga ulio wake kwa asili, bali mwanga wa
Kristo. Kanisa linapata mng’ao wake kutoka kwenye jua la haki, ili baadaye liweze
kusema: mimi ninaishi, lakini si mimi bali Kristo anaishi ndani yangu (Gal 2:).” Ni
kutokana na uhusiano huu uliopo kati ya Kristo na Kanisa ndio maana Mt. Sipriano hasiti
kutusaidia kutambua kuwa; “Kama hatuna Kanisa kama mama, hatuwezi kuwa na Mungu kama
Baba.” Imani iliyo hai 6. Imani ambayo mwanzo wake ni Mungu mwenyewe, inapaswa
kuwa hai na kwa hulka yake, kila kilicho na uhai kinakua. Mitume walipoyasikia mafundisho
ya Yesu aliyeonya juu ya watu kuwa chanzo cha makwazo, Mitume wanaomba kuongezewa
imani: “Bwana, tuongezee imani” (Lk 17:5). Mahali pengine tunakutana ya Yesu anayemponya
yule kijana mwenye pepo. Pamoja na imani ya baba wa kijana huyu, bado alimwambia Yesu,
“ukiweza neno lolote, utuhurumie” (Mk 9:22). Yesu anamjibu akisema: “Yote yawezekana
kwake aaminiye” (Mk 9:23). Baba wa kijana anamalizia kwa kusema: “Naamini, nisaidie
kutoamini kwangu” (Mk 9:24). Haya yalikuwa baadhi ya matukio katika Injili ambayo
yanatufunulia ukweli kwamba, imani kwa asili yake inakua na inakua vema kama inakuzwa
kwa msaada wa neema ya Kristo. 7. Inapotokea kwamba kuna kutetereka katika makuzi
ya imani ni wajibu wetu kukumbushana na kuhimizana, ili tuweze kuamka na kusimama
tena katika imani. Huu ni mwaliko wa kurudi tena kwenye misingi ya imani na kujipima
ili kuona kama maisha yetu bado yamesimama katika msingi wa imani au tumeanza kupotoka.
Mtume Paulo akiwaandikia Wakorintho anawapa changamoto akisema: “Jijaribuni wenyewe
kwamba mmekua katika imani; jithibitisheni wenyewe. Au hamjijui wenyewe, kwamba Yesu
Kristo yu ndani yenu?” (2Kor 13:5). Mtume Paulo anawataka wajipime kuona ni kwa kiasi
gani na ni kwa namna gani waamini wa Korintho wamekua katika imani. Wakati kwa upande
mmoja imani hujaribiwa na Mungu, kwa upande mwingine Mtume Paulo anatushauri tujipe
nafasi za kujijaribu wenyewe ili tuone kama tunakua au tunadumaa katika imani. Zipo
namna nyingi za kujijaribu wenyewe katika imani, lakini njia ya uhakika kabisa ya
kujipima ni kuangalia ni kwa namna gani tunakua katika fadhila zile mbili zingine
za kimungu; yaani matumaini na mapendo.