2013-04-17 14:36:28

Hakuna ufufuko pasi na Msalaba; Kupaa kwenda mbinguni bila ya utii kwa Mwenyezi Mungu!


Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 17 Aprili 2013, akiwa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, aliendelea na Katekesi katika Maadhimisho ya Mwaka wa Imani kwa kuchambua Kanuni ya Imani, kipengele kinachozungumzia kuhusu Yesu Kupaa mbinguni. Katika Kanuni ya Imani waamini wanasali kwamba "Akapaa mbinguni, amekaa kuume kwa Baba.

Mwinjili Luka anawaalika waamini kulitafakari fumbo la Kupaa kwa Bwana mbinguni mintarafu maisha ya Yesu hapa duniani, lakini kwa namna ya pekee, kwa kupanda kwenda Yerusalemu ili kukabiliana uso kwa uso na Fumbo la Msalaba; yaani: mateso, kifo na ufufuko wake kama kielelezo cha utii kwa mapenzi ya Baba yake wa mbinguni.

Mwinjili Luka anakazia mambo makuu mawili: kabla ya kurudi ili kushiriki katika utukufu wa Baba yake wa Mbinguni, Yesu Mfufuka aliwabariki wafuasi wake. Hapa Baba Mtakatifu Francisko anabainisha kwamba, Yesu anajionesha kuwa ni Kuhani wa milele. Ni Mungu kweli na mtu kweli, anayeendelea kuwaombea wafuasi wake mbele ya Baba yake wa mbinguni.

Jambo la pili anasema Baba Mtakatifu ni kwamba, Mwinjili Luka anasimulia jinsi ambavyo Mitume wa Yesu walivyorudi mjini Yerusalemu wakiwa na furaha kubwa. Walitambua kwamba, hata kama Yesu Mfufuka alikuwa ametoweka mbele ya macho yao kimwili, lakini bado anaendelea kuliongoza Kanisa lake, hadi ukamilifu wa dahari.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini wanapoendelea kulitafakari Fumbo la Kupaa kwa Bwana mbinguni, wawe pia ni mashahidi wa furaha ya ufufuko wa Kristo, uwepo wake endelevu miongoni mwa wafuasi wake na ushindi wa Ufalme viwe ni vielelezo vya utakatifu na upendo.

Baba Mtakatifu Francisko ametambua uwepo wa Maaskofu kutoka Uingereza, Mapadre na Majandokasisi kutoka Chuo Kikuu cha Kipapa cha Amerika ya Kaskazini pamoja na mahujaji kutoka katika nchi zinazozungumza lugha ya Kiingereza.

Amewahakikishia waamini kwamba, hata katika magumu na mahangaiko yao ya ndani, watambue kwamba, Yesu Kristo Mfufuka yuko pamoja nao daima katika hija na familia, mahali pa kazi; nyakati za furaha na majonzi, ili ulimwengu uweze kuonja upendo wa Mungu.

Baba Mtakatifu Francisko amewapongeza waamini kutoka katika Madhabahu ya Mtakatifu Andrea Bobola yaliyoko Varsavia, Poland, waliofika mjini Roma ili kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa Maadhimisho ya Jubilee ya miaka 75 tangu Mtakatifu msimamizi wao alipotangazwa kuwa Mtakatifu. Mtakatifu Bobola alikuwa ni Padre Myesuit na Mfia dini.

Ni Padre aliyejitosa kimaso maso kwa ajili ya imani na upatanisho wa Kanisa na ndugu katika imani. Maombezi yake mbele ya Mwenyezi Mungu yalisaidie Kanisa kuwa na umoja na amani.

Baba Mtakatifu pia ametambua uwepo wa Mapadre na Watawa wanaofanya kumbu kumbu ya Miaka 75 tangu mwanzilishi wao Mtakatifu Giovanni Leonardi alipotangazwa kuwa Mtakatifu. Anawataka waamini kutoa maisha yao kwa ajili ya huduma ya Injili.

Amewaombea vijana na wanafunzi waliokuwa wamefurika kwa wingi kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, ili wawe tayari kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya kumfuasa Kristo; wagonjwa wapokee mahangaiko yao kwa utulivu na wanandoa wapya waendelee kukua na kukomaa katika utakatifu, wakijitahidi kufuata mfano wa Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu.







All the contents on this site are copyrighted ©.