2013-04-16 15:13:57

Wananchi wa Boston, shindeni ubaya kwa wema!


Baba Mtakatifu Francisko ametuma salama za rambi rambi kwa Kardinali Seàm O' Malley, Askofu mkuu wa jimbo kuu la Boston, Marekani kutokana na mauaji ya kinyama yaliyotokea Jumatatu tarehe 15 Aprili 2013 wakati wa mashindano ya mbio za Marathon na kusababisha watu watatu kupoteza maisha na wengine 141 kulazwa hospitalini.

Ujumbe wa Baba Mtakatifu umeandikwa kwa niaba yake na Kardinali Tarcisio Bertone, Katibu mkuu wa Vatican. Anasema, anaungana na wote wanaomboleza kutokana na kuondokewa na ndugu, jamaa na marafiki zao. Anawakumbuka pia wote waliopatwa na majeraha ili waweze kupona haraka na kuendelea na shughuli zao. Anawaomba wasamaria wema kuendelea kutoa msaada wa hali na mali kwa waathirika wa tukio hili.

Kwa namna ya pekee Baba Mtakatifu anawaomba wananchi wa Marekani kushinda uovu kwa wema; daima wakijitahidi kujenga na kuimarisha haki, uhuru na usalama hata kwa kizazi kijacho.







All the contents on this site are copyrighted ©.