Jumuiya ya Kimataifa na changamotoza uhuru wa kidini
Uhuru wa kidini ni kati ya changamoto kubwa zinazoikabili Jumuiya ya Kimataifa kwa
katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Ni mada ambayo
itajadiliwa na wadau kutoka sehemu mbali mbali za dunia tarehe 19 Aprili 2013, tukio
ambalo limeandaliwa na Kikundi cha Technology Entertainment Design, TED na kudhaminiwa
na Baraza la Kipapa la Utamaduni.
Mkutano huu unaotarajiwa kuwa na mvuto mkubwa
kwa wadau kutoka ndani na nje ya Italia utafanyika hapa mjini Roma. TED ni kati ya
mitandao yenye idadi kubwa ya watu wanaoogelea huko kutafuta habari makini. Inasadikiwa
kwamba, walau kila siku, kuna jumla ya watu zaidi ya millioni moja wanaotembelea katika
tovuti hii.
Mkutano huu wa aina yake, unatarajiwa kufunguliwa na Kardinali
Gianfranco Ravasi, Rais wa Baraza la Kipapa la Utamaduni. Ni mkutano unaowahusisha
viongozi kutoka katika medani mbali mbali za maisha, wakiwa na ujuzi, mang’amuzi na
mitazamo tofauti kuhusu: uhuru na dini.
Wajumbe watapembua kwa kina na mapana
umuhimu wa Jamii kuendelea kujadili kuhusu uhuru wa kidini; tofauti kati ya uhuru
na uhuru wa kidini; mchango wa dini katika maendeleo endelevu yanayogusa mahitaji
ya mtu mzima: kiroho na kimwili; uwezo wa mwanadamu kufikiri na kutenda. Wawezeshaji
wakuu katika mkutano huu ni wale ambao wamechaguliwa kwa umakini mkubwa baada ya kufanya
utafiti uliodumu kwa takribani mwaka mmoja.
Kardinali Gianfranco Ravasi atajadili
kwa kina na mapana mchango unaotolewa na Baraza la Kipapa mitarafu majadiliano ya
kidini na wale wasioamini, changamoto iliyotolewa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto
wa kumi na sita, aliyelitaka Baraza la Kipapa la Utamaduni kuendesha majadiliano na
watu mbali mbali ambao kimsingi hawana imani, lakini wangependa walau kufahamu habari
za Mwenyezi Mungu.