Jumuiya ya Kimataifa inaalikwa kuchukua hatua madhubuti ili kukomesha mauaji ya watu
wasiokuwa na hatia nchini Syria
Viongozi mbali mbali wa kidini nchini Uingereza wameendelea kusali kwa ajili ya kuombea
amani na utulivu nchini Syria kwani mateso ya wananchi wa Syria kwa sasa yamevuka
kiwango cha uvumilivu wa kibinadamu.
Tangu mwaka 2011, zaidi ya Wakristo 1,000
wameuwawa kikatili; Makanisa, shule na zahanati zipatazo 40 zimeharibiwa kutokana
na machafuko ya kidini yanayoendelea nchini Syria. Hakuna amani wala usalama kiasi
kwamba, Ukanda wa Mashariki ya Kati uko hatarini kwa sasa. Kwa miaka mingi Syria ilikuwa
inatoa hifadhi kwa wakimbizi na wahamiaji kutoka Lebanon, Iraq na katika nchi nyingine
jirani, lakini sasa hakuna tena amani wala usalama.
Haya yamo kwenye ujumbe
wa Patriaki Gregorios wa tatu kutoka Syria anayewaalika viongozi mbali mbali wa kidini
kuombea amani na kwamba, viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa wanapaswa kutoa kipaumbele
cha pekee, ili kuokoa maisha ya watu wengi kutokana na vita inayoendelea nchini Syria.
Wananchi wa Syria wanapaswa kuchukua maamuzi magumu yaani kuendelea kubaki
nchini mwao ili kukabiliana na kifo uso kwa uso au kukimbia ili kusalimisha maisha
yao!