2013-04-16 14:56:35

Benedikto XVI akumbukwa katika Ibada ya Misa Takatifu anapoadhimisha miaka 86 ya kuzaliwa kwake


Baba Mtakatifu Francisko Jumanne, tarehe 16 Aprili 2013 ameadhimisha Ibada ya Misa kwenye Kikanisa cha Domus Sanctae Marthae kwa nia ya kumwombea Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, ili Mwenyezi Mungu aendelee kumlinda, kumtunza na kumfariji katika maisha yake ya: sala na tafakari ya kina kwa ajili ya mafao na ustawi wa Kanisa. Ibada hii ni kwa ajili ya Maadhimisho ya Miaka 86 tangu alipozaliwa Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita.

Katika Ibada hii ya Misa Takatifu, Papa alitafakari kuhusu baadhi ya watu wanavyoweka vizingiti dhidi ya Roho Mtakatifu, kiasi hata cha kuwauwa Manabii, hali ambayo inaendelea hata katika ulimwengu mamboleo. Roho Mtakatifu anawasukuma waamini kusonga mbele ikiwa kama wanataka. Roho Mtakatifu anawawezesha waamini kuishi kwa umoja, upendo na mshikamano wa dhati, kwani ni nguvu ya Mungu inayotenda kazi miongoni mwa watu wake. Roho Mtakatifu ni faraja kwa waamini wanaoteseka sehemu mbali mbali za dunia.

Jubilee ya Miaka 50 ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican iwe ni changamoto kwa Mama Kanisa kusoma alama za nyakati ili kufuata ule msukumo ulioletwa na Roho Mtakatifu, hata ukawafanya Mababa wa Mtaaguso Mkuu wa Pili wa Vatican kutaka kuleta mabadiliko ya dhati katika maisha na utume wa Kanisa ulimwenguni. Anawaalika waamini kumwachia nafasi Roho Mtakatifu ili aweze kutenda kazi yake ndani mwao katika mchakato wa Uinjilishaji Mpya; kwani wataweza kuwa huru kama watoto wateule wa Mungu.

Waamini wajifunze kuwa wanyenyekevu kwa Roho Mtakatifu, wajitahidi kuchuchumilia utakatifu wa maisha, changamoto kwa waamini wote.







All the contents on this site are copyrighted ©.