2013-04-16 08:44:07

Bara la Asia linapaswa kusikilizwa, kufahamika, kuthaminiwa na kupendwa ili kuendelea kutoa mchango wake katika Uinjilishaji Mpya


Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu, Jumatatu tarehe 15 Aprili 2013 amefungua kongamano la kimataifa linaloongozwa na kauli mbiu "Kulisikiliza Bara la Asia: njia za imani, jamii na dini kati ya mapokeo na usasa".

Katika hotuba yake amezungumzia kuhusu mang'amuzi na uzoefu wake wa takribani miaka ishirini na miwili aliyolitukia Kanisa Barani Asia, akiwa katika utume wake wa kidiplomasia. Akiwa Barani Asia aliguswa na huduma za Uinjilishaji wa kina unaogusa mtu zima: kiroho na kimwili zinazotolewa na Kanisa Barani Asia, licha ya ukweli kwamba, waamini wanakabiliwa na madhulumu ya kidini, changamoto ya kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini na kiekuemene.

Kongamano hili ni sehemu ya changamoto zilizotolewa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, wakati huu wa Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, ili waamini waweze kutolea ushuhuda amini wa imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Bara la Asia limekuwa na mchango mkubwa katika ustawi na maendeleo ya binadamu hasa katika masuala ya kidini na kitamaduni.

Ustaarabu huu unaendelea kukabiliana na mabadiliko makubwa na ya haraka yanayojitokeza katika medani mbali mbali za maisha kama sehemu ya mchakato wa ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Mawasiliano ya kijamii ni ya haraka sana kiasi cha kuvuka mipaka na vikwazo vilivyokuwepo miaka kadhaa iliyopita. Kuna mwingiliano mkubwa wa masuala ya uchumi, biashara na watu kutoka sehemu moja hadi nyingine.

Pamoja na maendeleo yote haya, lakini bado hakuna uwiano sawa wa maendeleo na wakati mwingine, dini zimekuwa ni chanzo cha kinzani na migogoro ya Kijamii. Bara la Asia linakabiliana na changamoto nyingi, lakini anasema Kardinali Filoni linapaswa kusikilizwa, kufahamika, kuthaminiwa na kupendwa, kama walivyofanya Wamissionari wa kwanza waliojitosa bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutangaza Habari Njema ya Wokovu.

Kongamano hili linahitimishwa tarehe 17 Aprili 2013.







All the contents on this site are copyrighted ©.