2013-04-15 08:50:34

Wakristo wanaalikwa kutangaza, kushuhudia na kumwabudu Mwenyezi Mungu


Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili jioni, tarehe 14 Aprili 2013, alitembelea na kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Paulo, nje ya kuta za Roma. Alipowasili, alipokelewa na viongozi wa Kanisa na Serikali na baadaye akaelekea kwenye kaburi la Mtakatifu Paulo, hapo alibaki kwa kitambo kidogo akisali na baadaye, alianza maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu.

Katika mahubiri yake, Baba Mtakatifu aliwashukuru wote kwa kusema kwamba, alikuwa na furaha ya pekee kabisa kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kaburi la Mtakatifu Paulo, mwalimu wa mataifa aliyetangaza Injili ya Kristo na kuishuhudia kwa kuyamimina maisha yake na kumwabudu kwa moyo wake wote.

Katika somo la kwanza Baba Mtakatifu anasema, Mitume waliamriwa kwa nguvu kutofundisha kwa jina la Yesu wala kutangaza ujumbe wake, lakini Petro na mitume wengine wakajibu kwa ushujaa wakisema, ilikuwa imewapasa kumtii Mungu kuliko wanadamu. Mitume wakasonga mbele kwa ari na moyo mkuu bila kuogopa madhulumu wala vitisho, wakitangaza Injili ya Kristo.

Baba Mtakatifu anawauliza waamini nyakati hizi, Je, wako tayari kutangaza Neno la Mungu katika medani mbali mbali za maisha yao? Kwenye Familia na watu wanaoambatana nao kila siku ya maisha yao? Imani inakuja kwa kusikiliza na ina imarishwa kwa kutangazwa.

Mitume wa Yesu walitangaza Injili ya Kristo sanjari na kujitahidi kuwa ni waaminifu kwa Kristo aliyeyagusa na hatimaye kubadili maisha yao, akawapatia mwelekeo mpya, kiasi kwamba, wakathubutu kuyamimina maisha hayo kama ushuhuda kwa Kristo. Mtume Petro alipewa dhamana na Kristo kuwachunga na kuwalisha Kondoo wake, changamoto kwa viongozi wa Kanisa anasema Baba Mtakatifu kuhakikisha kwamba, wanatekeleza mapenzi ya Mungu, kwa kutolea ushuhuda wa imani yao kwa Kristo na Kanisa lake bila ya kujibakiza hata kidogo.

Baba Mtakatifu anasema Injili inapaswa kutangaza na kushuhudiwa, wajibu na dhamana ya Wakristo wote. Kila mwamini anapaswa kujiuliza moyoni mwake ni kwa jinsi gani anavyomshuhudia Kristo katika maisha yake, kwa kutambua kwamba, ushuhuda huu unatofautiana kadiri ya: wito na mazingira, lakini kila mmoja anapaswa kuchangia kadiri ya nafasi yake na uhalisia wa maisha yake ya kila siku. Kwa mfano katika kujenga na kudumisha urafiki na uhusiano mwema ndani ya familia na maeneo ya kazi.

Baba Mtakatifu anasema, kila siku kuna watakatifu wanaotekeleza wajibu wao kimya kimya pasi na majigambo na kwamba, kila mwamini anaweza kushiriki utakatifu. Katika ulimwengu mamboleo kuna watu ambao wanaendelea kuteseka kama ilivyokuwa wakati wa Mitume Petro na Paulo kwa ajili ya Injili. Kuna baadhi ya waamini wanadiriki hata kuyamimina maisha yao ili kuendelea kuwa waaminifu kwa Kristo na Kanisa lake.

Kwa hakika, Injili ya Kristo inatangazwa kwa ushuhuda amini wa maisha. Watu wanapaswa kuona na kusikia Injili inayotangazwa na Wakristo kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao, ili waweze kumpatia Mungu sifa na utukufu. Hii ni changamoto ya kutangaza Injili kwa njia ya maisha; watu waone yale yanayohubiriwa yakiwa yamemwilishwa katika matendo kama kielelezo makini cha ushuhuda wa Kanisa.

Baba Mtakatifu Francisko anasema kuwa yote haya yanawezekana ikiwa kama waamini wanamfahamu vyema Yesu Kristo na kuendelea kufuata ile njia aliyowaonesha. Kutangaza na kuishuhudia Injili inawezekana ikiwa kama wafuasi wa Kristo watathubutu kuwa karibu naye kama walivyofanya Mitume wake kwa njia ya majadiliano ya maisha, ili hatimaye, waweze kumwabudu Mwanakondoo wa Mungu aliyechinjwa, anayestahili kuabudiwa na kutukuzwa. Waamini wajenge utamaduni wa kumwendea Mwenyezi Mungu kwa kumwomba, kumtukuza, kumshukuru lakini zaidi kwa kumwabudu.

Kuabudu anasema Baba Mtakatifu kuna maanisha kujifunza kukaa na kujadiliana na Mwenyezi Mungu; kuonja na kutambua uwepo wake wa daima pamoja na kumpatia kipaumbele cha kwanza. Ni mwaliko wa kumwamini kwa kutambua kwamba, ndiye kiongozi muhimu wa maisha ya kila mwamini, kwani Yeye ni Mungu wa maisha na historia ya binadamu.

Hii ni changamoto ya kuvua ile miungu mikubwa na midogo, ambayo waamini wanaitumia kama kimbilio lao, ili kujipatia uhakika wa usalama wa maisha: miungu hii inaweza kuwa uchu wa mafanikio, madaraka na kazi; hali ya kujiona ni bora zaidi kuliko wengine, tatizo la kujiamini kupita kiasi bila kusahau dhambi za mazoea. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kuchunguza dhamiri zao ili kubainisha ile miungu inayowanyima nafasi ya kumwabudu Mungu wa kweli na kumpatia kipaumbele cha kwanza katika maisha yao.

Baba Mtakatifu Francisko alihitimisha mahubiri yake kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Paulo nje ya kuta za Roma, kwa kuwataka waamini kumfuasa Kristo kwa ujasiri na uaminifu, kwani amewaonesha upendeleo wa pekee kwa kuwachagua kuwa wafuasi wake. Anawataka kumfuasa kwa maneno na ushuhuda wa uhalisia wa maisha ya kila siku.

Mwenyezi Mungu anawachangamotisha kuvua miungu uchwara na kuanza kumwabudu Mungu wa kweli. Dhamana hii inaweza kutekelezwa kwa kutangaza, kushuhudia na kumwabudu. Bikira Maria Mama wa Mungu na wa Mitume awaombee na kuwasaidia Wakristo katika hija yao ya ufuasi wa Kristo.

Mara baada ya Maadhimisho ya Misa Takatifu, Papa alikwenda kutoa heshima yake kwa kwa Sanamu ya Bikira Maria Mama wa Mungu, ambayo kunako tarehe 22 Aprili 1541, Mtakatifu Inyasi wa Loyola na wafuasi wake wa kwanza waliweka nadhiri zao za daima, tukio muhimu sana katika kuanzishwa kwa Shirika la Wayesuit.







All the contents on this site are copyrighted ©.