2013-04-15 16:15:43

Viongozi wa Watawa kutoka Marekani wakutana na kuzungumza na viongozi waandamizi kutoka Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa


Viongozi waandamizi kutoka Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa, Jumatatu tarehe 14 Aprili 2013 kwa mara ya kwanza wamekutana na kuzungumza na viongozi wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume kutoka Marekani.

Askofu mkuu Gerhard Ludwig Muller, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa amewashukuru Watawa wanawake kutokana na mchango wao katika sekta ya elimu, afya na huduma kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii.

Askofu mkuu Muller amewataka watawa kuendelea kuzingatia mafundisho yaliyotolewa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican: kwa kujenga na kuimarisha umoja na mshikamano unaobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake; kuendelea kuwa waaminifu kwa Mafundisho ya viongozi wa Kanisa, sanjari na kushirikiana kwa karibu zaidi na Mabaraza ya Maaskofu Katoliki, mintarafu sheria za Kanisa.

Askofu mkuu Muller amewaelezea kwa muhtasari mazungumzo yake na Baba Mtakatifu Francisko kuhusu marekebisho yanayopaswa kufanywa katika Shirikisho la Wakuu wa Mashirika. Lengo la mkutano kati ya viongozi waandamizi kutoka Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa na Viongozi wakuu wa Mashirika ya Kitawa ni kuendeleza mshikamano wa imani na upendo wa Kikristo, ili kuendelea kulitajirisha Kanisa kwa karama zao mbali mbali hata kwa kizazi kijacho.







All the contents on this site are copyrighted ©.