Ujumbe kutoka Hispania wakutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican
Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu, tarehe 15 Aprili 2013 amekutana na kuzungumza
na Bwana Mariano Rajoy Brey, Waziri mkuu wa Hispania pamoja na ujumbe wake. Baadaye,
waliweza kukutana na kuzungumza pia na viongozi waandamizi kutoka Vatican chini ya
uongozi wa Kardinali Tarcisio Bertone, katibu mkuu wa Vatican.
Viongozi hawa
kwa pamoja wamejadili kwa kina mapana kuhusu hali ngumu inayowakabili wananchi wa
Hispania kwa wakati huu, kama ilivyo pia kwa nchi nyingine za Jumuiya ya Ulaya, hali
ambayo imepelekea ukosefu wa fursa za ajira kwa familia na idadi kubwa ya vijana ambao
kwa sasa wanakosa matumaini kwa leo na kesho iliyobora zaidi.
Katika kipindi
hiki kigumu, Kanisa limeendelea kutoa mchango wa pekee kwa kutumia Mashirika yake
ya Misaada kama vile Caritas Hispania na mengineyo ili kuwasaidia watu walioathirika
zaidi. Kwa pamoja wameona kwamba, kuna umuhimu wa kuendeleza majadiliano ya Kijamii
kwa wahusika wote kwa kuheshimiana, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa tunu msingi
za maisha ya kijamii na kiutu; haki, amani, upendo, mshikamano na mafao ya wengi.
Viongozi
hawa wawili wamepongeza ushirikiano uliopo kati ya Hispania na Vatican, uliofikiwa
kunako mwaka 1979, pande hizi mbili zilipowekeana sahihi mkataba wa ushirikiano, ambao
umeendelea kudumishwa mwaka hadi mwaka. Wamegusia suala tata la ndoa na familia na
umuhimu wa majiundo ya kidini. Taarifa inabainisha kwamba, Baba Mtakatifu pamoja na
mgeni wake wamejadili pia masuala ya kimataifa na kwa namna ya pekee hali inavyojionesha
Amerika ya Kusini.