Mitume wa Yesu walitangaza kwa ari na ujasiri mkuu kuhusu ufufuko wa Kristo kwa kutambua
kwamba, walikuwa wanaongozwa na Kristo pamoja na Roho Mtakatifu
Kitabu cha Matendo ya Mitume kinaelezea kwa kina na mapana ujasiri uliooneshwa na
Petro pamoja na mitume wengine, licha ya kukatazwa kufundisha kwa jina la Yesu, lakini
bado waliendelea kutangaza Injili ya Kristo kwa ujasiri na uhodari mkubwa wakisema
kwamba, Yesu ambaye walimuua na kumtundika Msalabani, ndiye aliyefufuka kutoka katika
wafu na kwamba, ni Masiha kama walivyokuwa wametabiri Manabii katika Agano la Kale.
Wakuu
wa Makuhani walijitahidi bila mafanikio kuhakikisha kwamba, wanafutilia mbali Jumuiya
ya Wakristo wa kwanza iliyokuwa inaibuka kwa kasi ya ajabu. Mitume wakadhulumiwa lakini
hawakukata tamaa, wakaendelea kumtii Mwenyezi Mungu kwa kutambua kwamba, Yesu Kristo
Mfufuka ni Bwana na Mkombozi wa Ulimwengu na kwamba sasa amekaa kuume kwa Baba yake
wa mbinguni. Mitume ni mashahidi wa tukio hili. Licha ya mkong'oto wa nguvu, lakini
Mitume waliendelea kufurahi kwa sababu wamehesabiwa kuwa wamestahili kuaibishwa kwa
ajili ya jina la Kristo.
Ni maneno ya Baba Mtakatifu Francisko wakati wa tafakari
ya Sala ya Malkia wa Mbingu, Jumapili tarehe 14 Aprili 2013, kwenye Uwanja wa Kanisa
kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Anajiuliza swali la msingi, wafuasi wa kwanza
wa Yesu walipata wapi nguvu za kuweza kumtolea ushuhuda?
Walipata wapi furaha
na ujasiri wa kutangaza Injili ya Kristo licha ya vizingiti walivyokumbana na vyo?
Mitume wa Yesu walikuwa ni watu wa kawaida kabisa, lakini katika maisha na ushuhuda
wao waliweza kuujaza mji wa Yerusalemu mafundisho juu ya Yesu Kristo.
Baba
Mtakatifu anasema, hiki ni kielelezo kwamba, Yesu Kristo Mfufuka pamoja na Roho Mtakatifu
walikuwa pamoja nao, kiasi cha kuwawezesha kuhibiri kwa: ari, nguvu na ushujuaa mkubwa
kuhusu Ufufuko wa Yesu Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka katika wafu. Hawakuwa
na woga wa mtu au kitu chochote na kwamba, madhulumu kwao ilikuwa ni heshima iliyowawezesha
kufuata nyayo za Yesu kwa kumtolea ushuhuda wa maisha.
Baba Mtakatifu Francisko
anakazia kwamba, historia ya Wakristo wa Kanisa la mwanzo ni endelevu hata kwa Wakristo
wanaoishi katika ulimwengu mamboleo, kwamba, wao walimfahamu na kumwamini Yesu Kristo
sanjari na kuonja uwepo wake katika hija ya maisha yao na kwamba, nguvu ya Kristo
Mfufuka iliwasukuma kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya kushirikisha tukio la
Ufufuko wa Kristo. Wakristo waliweza kuvuka vikwazo na madhulumu kwa kuonesha upendo
na nguvu ya ukweli.
Baba Mtakatifu anakazia kwamba, upendo wa kidugu ni ushuhuda
wa dhati ambao waamini wanaweza kuutolea ili kuonesha kwamba, kweli Yesu Kristo Mfufuka
anaishi ndani mwao. Aliwaalika waamini kusali na kuwaombea Wakristo wanaoendelea kudhulumiwa
sehemu mbali mbali za dunia, ili kwa sala na sadaka zao waweze kuonja faraja kutoka
kwa Kristo Mfufuka. Bikira Maria aliombee Kanisa, ili kwa msaada wake liweze kutangaza
Injili ya Kristo kwa ari kubwa na ushujaa kwamba, kweli amefufuka nao wao ni mashahidi
wa tukio hili.
Mara baada ya Sala ya Malkia wa Mbingu, Baba
Mtakatifu alikumbushia kwamba, Jumamosi, Jimboni Venezia, Kardinali Angelo Amato alimtangaza
Padre Luca Passi kuwa ni Mwenyeheri. Yeye ni mwanzilishi wa Shirika la Walei wa Mtakatifu
Dorothea na Mwanzilishi wa Shirika la Watawa walimu wa Mtakatifu Dorothea. Amewaalika
waamini kumshukuru Mungu kwa ushuhuda ulioneshwa na Mwenyeheri Padre Luca Passi.
Baba
Mtakatifu alikumbushia pia kwamba, Baraza la Maaskofu Katoliki Italia lilikuwa linaadhimisha
Siku ya 89 ya Chuo Kikuu cha Moyo Mtakatifu wa Yesu, Chuo ambacho kilianzishwa na
Padre Agostino Gemelli kwa kupata msaasa kutoka kwa Wakristo na watu wenye mapenzi
mema. Chuo hiki kimetoa mchango mkubwa katika kuwaunda vijana ili waweze kuwajibika
na daima wakitafuta mafao ya wengi.
Anawaalika waamini kuendelea kuunga mkono
juhudi hizi ili ziweze kuwajengea uwezo vijana wa kizazi kipya katika kukabiliana
na changamoto za maisha.