2013-04-15 11:59:39

Majadiliano ya kidini ni muhimu sana katika kudumisha amani duniani


Migogoro, malumbano na kinzani za kidini ni kati ya mambo yanayoendelea kuhatarisha amani, upendo na mshikamano katika Jumuiya ya Kimataifa. Hii ni migogoro inayofuka moshi kuanzia katika Jamii za watu na hatimaye, kuwasha moto mkubwa wa kinzani na migogoro ya kidini kimataifa.

Katika miaka ya hivi karibuni, kinzani kati ya waamini wa dini ya Kiislam na Kikristo imeendelea kusikika sehemu mbali mbali za dunia, kila upande ukidai kunyanyasika! Lakini ukweli wa mambo ni kwamba, kuna baadhi ya watu wanaopenda kutumia migogoro na kinzani za kidini kwa ajili ya mafao yao binafsi, hali ambayo inaleta maafa makubwa kwa Jamii husika.

Padre Makari Habibi, katibu muhtasi wa Papa Tawadros wa Pili, Patriaki wa Kanisa la Kiorthodox la Kikoptic nchini Misri anasema, kuna haja kwa Serikali ya Misri kuhakikisha kwamba, inalinda na kuheshimu uhuru wa kidini kama nguzo msingi ya kulinda na kudumisha misingi ya haki, amani na utulivu miongoni mwa Jamii. Hii inatokana na ukweli kwamba, asilimia kubwa ya wananchi wa Misri ni waamini wa dini ya Kiislam na waamini wa dini nyingine ni asilimia kidogo.

Mashambulizi dhidi ya waamini wa dini nyingine kwa kisingizio cha imani kali ni jambo ambalo kamwe haliwezi kuvumiliwa na wapenda amani duniani. Sheria inapaswa kuchukua mkondo wake kwa watu wanaovunja sheria za nchi kwa kufanya vitendo vya jinai vinavyohatarisha usalama wa maisha na mali za wananchi. Vyombo vya ulinzi na usalama viwe makini kuhakikisha amani na utulivu vinadumishwa ili kila mwananchi aweze kutekeleza wajibu wake kikatiba, kwani hii ndiyo Sheria Mama inayolinda uhuru wa kila mtu.

Viongozi wa dini wapewe fursa ya kufundisha dini shuleni. Padre Makari Habibi anasema, umefika wakati kwa Serikali ya Misri kutoa nafasi kwa Kanisa la Kiorthodox la Kikoptik Misri kuanza kufundisha dini shuleni kama sehemu ya mchakato wa majadiliano ya kidini miongoni mwa wanafunzi. Ni jambo ambalo haliwezi kukubalika kwa Kanisa la Kikoptik kuendelea kuwekwa pembezoni mwa Jamii ya wananchi wa Misri.

Kinzani na migogoro ya kidini ni kielelezo cha ukosefu wa utawala bora unaozingatia sheria na maadili ya uongozi, kwani kuna baadhi ya viongozi wanaendeleza chuki na uhasama wa kidini kwa ajili ya mafao yao ya kisiasa. Watu wanaopandikiza mbegu za chuki na uhasama wanapaswa kushughulikiwa na vyombo vya sheria mapema kabisa na wala wasingojee hadi mambo yanapoharibika na hivyo kuanza kurushiana mpira wa uwajibikaji.

Waamini wa Kanisa la Kikoptik nchini Misri, wanapaswa pia kupata uwakilishi katika taasisi zinazoendeshwa na kusimamiwa na Serikali na kamwe wasitengewe kana kwamba, wao si wananchi wa Misri wenye haki na wajibu wa kutekeleza.
Mchakato wa kutafuta wawakilishi katika Bunge la Misri unatarajiwa kuanza hapo tarehe 22 Aprili na kuhitimishwa mwezi Juni 2013. Hadi sasa kuna uwakilishi mdogo sana wa waamini wa Kanisa la Kikoptik nchini Misri kadiri ya taarifa zilizotolewa na Shirika la Habari za Kimissionari, FIDES.








All the contents on this site are copyrighted ©.