Kikanisa kilichopo kwenye Uwanja wa Ndege ni mahali muafaka pa maadhimisho ya Mafumbo
ya Kanisa
Dhamana na utume wa washauri wa maisha ya kiroho katika viwanja vya ndege vya kiraia
ni kuhakikisha kwamba, wanajitahidi kumpeleka Mwenyezi Mungu kwa wafanyakazi hawa
na kuwasaidia wafanyakazi hao waweze kukutana na Mwenyezi Mungu katika utume wao.
Ni changamoto ya kujenga utamaduni wa kumsikiliza Mungu na kusikilizana wao
kwa wao, ili kwa pamoja waweze kutangaza Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia.
Yesu ni Neno wa Mungu aliyefanyika mwili, akakaa kati ya watu wake.
Hii ni
changamoto iliyotolewa na Kardinali Antonio Maria Vegliò, Rais wa Baraza la Kipapa
la wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi, wakati wa ufunguzi wa Semina ya Nane kwa
ajili ya Wafanyakazi wa Viwanja vya Ndege vya kiraia, inayofanyika mjini Cracovia,
nchini Poland. Semina imefunguliwa rasmi tarehe 15 Aprili na inatarajiwa kuhitimishwa
rasmi hapo tarehe 18 Arpili 2013.
Kardinali Vegliò anabainisha kwamba, Mwenyezi
Mungu katika historia ya maisha ya mwanadamu amezungumza naye kwa njia ya: Manabii,
lakini kwa wakati huu anazungumza naye kwa njia ya Yesu Kristo, Neno wa Mungu aliyefanyika
mwili. Kumbe, kila Andiko lenye pumzi ya Mungu, lafaa kwa mafundisho, na kwa kuwaonya
watu makosa yao, na kwa kuwaongoza, na kuwaadabisha katika haki; ili mtu wa Mungu
awe kamili, amekamilishwa apate kutenda kila tendo jema.
Baba Mtakatifu Francisko
bado anaendelea kuwaalika waamini na watu wenye mapenzi mema kujitaabisha kusikiliza
Neno la Mungu, ili kumpatia Kristo hifadhi katika maisha ya waamini, changamoto ya
watu kulindana na kutunza mazingira kwa ajili ya mafao ya wengi. Kusikiliza kwa makini
Neno la Mungu kuna wawajibisha waamini kutenda kadiri ya maagizo na utashi wa Mungu,
ili kufananana na Kristo kwa nguvu ya Roho Mtakatifu waliyempokea.
Neno la
Mungu ni amana kubwa ya imani katika maisha na utume wa Kanisa. Linapaswa kutangazwa
na kushuhudiwa katika matendo adili. Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, yawasaidie waamini
anasema Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, kumwilisha Imani katika
matendo ya huruma, kama sehemu ya ushuhuda wa imani kwa Kristo na Kanisa lake. Neno
la Mungu likisomwa na kutafakariwa sanjari na Mafundisho ya Kanisa linaonesha utajiri
mkubwa wenye uwezo wa kufundisha na kuwapatia watu hekima, ujuzi na maarifa.
Kardinali
Antonio Maria Vegliò anawaalika wafanyakazi katika sekta ya usafiri wa anga kujifunza
kutoka kwa Bikira Maria katika kusikiliza Neno la Mungu kwa makini na kulihifadhi
katika sakafu ya mioyo yao, ili liweze kuzaa matunda ya huduma ya upendo, kama alivyofanya
Bikira Maria.
Mama Kanisa anaendelea kuchangamotishwa kutoka na kwenda pembezoni
mwa Jamii ili kuwatangazia watu Habari Njema ya Wokovu, kwani huko ndiko ambako kuna
idadi kubwa ya watu wanaoteseka kutokana na ukosefu wa haki msingi za binadamu, ujinga,
umaskini, ukanimungu na dhambi, kama anavyobainisha Baba Mtakatifu Francisko.
Liturujia
ni mahali muafaka ambapo Mwenyezi Mungu anazungumza na waja wake. Hii ni changamoto
kwa washauri wa maisha ya kiroho kwa wafanyakazi wa sekta ya usafiri wa anga kujenga
utamaduni wa kuadhimisha Ibada ya Neno la Mungu katika Vikanisa vilivyoko kwenye Viwanja
vya Ndege. Pale inapowezekana, Ibada ya Misa Takatifu iadhimishwe pia. Mwenyeheri
Yohane Paulo wa pili aliwahi kusema kwamba, Kikanisa kilichopo kwenye Uwanja wa Ndege
ni mahali muafaka pa kuweza kuadhimsiha Mafumbo ya Kanisa.
Kardinali Antonio
Maria Veglio anahitimisha hotuba yake kwa wahudumu wa maisha ya kiroho kwenye viwanja
vya ndege kwa kuhimiza kwamba, utangazaji wa Neno la Mungu unajenga na kuimarisha
umoja unaowaletea waamini furaha ya kweli inayobubujika kutoka katika Fumbo la Utatu
Mtakatifu. Hii ni furaha ambayo ni zawadi kutoka kwa Kristo mwenyewe. Huu ni mwaliko
kwa Wakristo kuwa ni watangazaji wa Injili wanaotaka kufikisha Injili ya Kristo kwa
wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii: kiroho na kimwili.