Askofu mkuu Lebulu asema, amani inasimikwa katika ukweli, uhuru, upendo na msamaha!
Amani ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayomwajibisha binadamu katika maisha na
vipaumbele vyake. Kanisa linapoadhimisha Kumbu kumbu ya Jubilee ya miaka 50 tangu
Baba Mtakatifu Yohane wa XXIII alipochapisha Waraka wa kichungaji, Pacem In Terris,
Amani Duniani linakumbusha kwamba: Waraka huu ulibainisha haki na wajibu wa kila mtu
katika kulinda na kutetea haki na amani duniani, kwa kusoma alama za nyakati.
Askofu mkuu
Josephat Lebulu wa Jimbo kuu la Arusha Tanzania katika mahojiano maalum na Radio Vatican
kuhusu kumbu kumbu ya Jubilee ya Miaka 50 ya Waraka wa Kichungaji wa Amani Duniani
anasema, angependa kukazia mambo makuu manne: Ukweli, uhuru, upendo na msamaha dhana
iliyokaziwa kwa namna ya pekee na Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa pili, hakuna amani
pasi na msamaha. Amani ya kweli inaonesha uhusino wa dhati kati ya mwanadamu na Muumba
wake, Mazingira na watu wanaomzunguka.
Kuna uhusiano kati ya amani na uchumi,
siasa na maendeleo endelevu yanyogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Mambo
yote haya yakiwekwa pamoja yanakuwa ni viashilia vya amani katika Jamii husika. Kwa
vile binadamu wanakosa na kukosehana, kumbe, hawana budi kujenga utamaduni wa kusameheana
ili kujenga na kuimarisha misingi ya haki na amani.
Askofu mkuu Lebulu anasema,
katika kipindi cha miaka 50 iliyopita, amani imeendelea kukumbana na vitisho vingi.
Hii ni amani inagusa maisha na utume wa Kanisa pamoja na Jamii kwa ujumla wake. Sababu
msingi za kukosa amani ni: ubinafsi, uchu wa mali na madaraka; malumbano na kinzani
za kidini na kwamba, upendo na ukweli ni tunu ambazo zimepungua kwa kiasi kikubwa
katika Jamii nyingi, kiasi kwamba, watu wanaona hata hsida ya kusameheana. Lakini
Mwenyeheri Yohane Paulo wa pili anasema, kusamehe ni changamoto kwa watu wanaoishi
katika ulimwengu wa utandawazi.
Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na
sita katika Waraka wake wa Mlango wa Imani anasema imani haina budi kujikita katika
mapendo, kwani amani ya kweli inategemea kwa namna ya pekee imani ya Jamii husika.
Askofu mkuu Lebulu anasema kwamba, tunu hizi msingi katika maisha ya mwanadamu zinaendelea
kupungua siku hadi siku.
Kanisa linapaswa kuwa ni ishala ya amani na sehemu
ya mchakato wa mapambano dhidi ya umaskini wa kipato, hali na maisha ya kiroho. Kanisa
lisaidie kumletea mwanadamu maendeleo endelevu, kila mtu atekeleze wajibu wake katika
maboresho ya maisha ya mwanadamu ili: haki, amani, upendo na mshikamano wa kweli viweze
kutawala duniani.