Mwezi mmoja tangu Papa Francisko achaguliwe kuliongoza Kanisa Katoliki!
Baada ya waamini na watu wote wenye mapenzi mema kusali na kufunga kwa ajili ya kuwasindikiza
Makardinali waliokuwa kwenye mchakato wa uchaguzi wa Papa Mpya, hatimaye, tarehe 13
Machi 2013 usiku, moshi mweupe ukaonekana; uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro
ukafurika kwa umati wa watu kutoka sehemu mbali mbali za dunia, lakini bado kilibakia
kitendawili ni nani aliyechaguliwa?
Kardinali Polycarp Pengo, Rais wa Shirikisho
la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar katika mahojiano na Radio Vatican
aliwataka watu kutomwekea kizingiti Roho Mtakatifu na kwamba, uchaguzi wa Papa lilikuwa
ni tukio la Kikanisa.
Hatimaye, jina likatangazwa na watu wakamwona Papa Francisko,
akitabasamu na kuwapungia mkono, akiwa amevaa Msalaba wake wa siku zote kama Kardinali
kutoka Buenos Aires. Baada ya kuzungumza maneno machache ya shukrani, aliinamisha
kichwa kuomba sala kutoka kwa waamini na watu wenye mapenzi mema waliokuwa wamefurika
kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, kwa kitambo kidogo, ukimya ukatawala
na watu wakasali kwa ajili yake.
Siku iliyofuatia, Baba Mtakatifu Francisko
asubuhi na mapema aliondoka kwenda kutoa heshima zake kwa Bikira Maria Mama wa Mungu
na Kanisa kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria mkuu, lililoko mjini Roma pamoja na kulipa
deni la pango kwa kipindi chote alichokuwa amekaa kwenye nyumba ya Makleri, Roma.
Jioni, Baba Mtakatifu Francisko akaadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili
ya Kanisa akishirikiana na Makardinali wote walioshiriki katika mchakato wa uchaguzi
wa Papa mpya kwenye Kikanisa cha Sistina, kilichoko hapa mjini Vatican. Katika mahubiri
yake alikazia mambo makuu: kutembea kwa pamoja, wakijitahidi kujenga Kanisa la Kristo
kwa njia ya ushuhuda unaokumbatia Fumbo la Msalaba, kama kielelezo cha Wafuasi wa
Kristo.
Tarehe 15 Machi 2013, Baba Mtakatifu akakutana na kuzungumza na Makardinali
walioshiriki kwenye Conclave, akawashukuru wote na kupata nafasi ya kuzungumza na
kila mmoja wao. Aliwataka Makardinali kusimama kidete na kamwe wasikatishwe tamaa
na ukakasi pamoja na magumu ya maisha bali waendelee kumtumainia Roho Mtakatifu anaendelea
kulitegemeza Kanisa. Aliwataka kuwa na ujasiri wa kubainisha mbinu mpya za Uinjilishaji,
ili Kristo aweze kufahamika, kuabudiwa, kupendwa na kutumikiwa.
Tarehe 16 Machi
2013, Baba Mtakatifu alipata fursa ya pekee kukutana na hatimaye kuzungumza na umati
mkubwa wa waandishi wa habari kutoka sehemu mbali mbali za dunia, waliokuwa wamefurika
hapa mjini Vatican kufuatilia hatua kwa hatua mchakato wa uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu
Petro. Akawaambia kwamba, amepewa changamoto ya pekee ya kutowasahau maskini, akaona
Jina Francisko wa Assisi lilikuwa linaendana kabisa na utume wake mpya kama Khalifa
wa Mtakatifu Petro: changamoto ya kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini; amani pamoja
na utunzaji bora wa mazingira.
Nembo ya utume wa Baba Mtakatifu Francisko inasomeka
kwa maneno ya Kilatini "Miserando atque eligendo" "akamtazama kwa jicho la huruma,
akamchagua" Ni maneno ya Mtakatifu Beda katika mahubiri yake juu ya wito wa Mathayo
mtoza ushuru. Baba Mtakatifu ameendelea kukazia kuhuu huruma na upendo wa Mungu usiokuwa
na mipaka kwa waja wake. Mungu ni mwingi wa huruma, kamwe hachoki kusamehe, changamoto
kwa waamini kujifunza utamaduni wa kusamehe na kuwa na huruma.
Tarehe 19 Machi
2013 Baba Mtakatifu Francisko aliadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kama mwanzo wa utume
wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, Ibada ambayo ilikuwa na uwakilishi mkubwa wa
viongozi wa dini, madhehebu na wale wa Serikali bila kuwasahau wawakilishi wa maskini
kutoka Buenos Aires. Akawataka waamini na Viongozi wa Kimataifa kuwa ni watunzaji
bora wa jirani zao na mazingira na kwamba, madaraka ni kwa ajili ya huduma kwa wanyonge.
Kama Papa anatamani kuwa ni daraja linalounganisha watu mbali mbali sanjari na kulinda,
kutetea na kudumisha misingi ya haki, amani na majadiliano.
Mkazo huu ulijionesha
pia wakati Baba Mtakatifu alipokutana na kuzungumza na Wanadiplomasia na wawakilishi
wa nchi na mashirika ya kimataifa hapa mjini Vatican.
Tarehe 23 Machi 2013
Baba Mtakatifu Francisko kwa mara ya kwanza akakutana na Papa mstaafu Benedikto wa
kumi na sita, tukio ambalo litakumbukwa daima katika historia ya Kanisa Katoliki;
ndugu wawili katika huduma kwa Kristo na Kanisa lake wakakumbatiana, wakasali, wakazungumza
na kula kwa pamoja. Jumapili ya Matawi, Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro ukafurika
na umati wa vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia, akawaambia, kamwe wasikubali
kupokonywa matumaini yanayobubujika kutoka kwa Kristo!
Alhamisi kuu, Baba Mtakatifu
akaadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kubariki Mafuta Matakatifu, akawataka
Makleri wa Roma kutoka katika ubinafsi na undani wao, ili kwaendea wale walioko pembezoni
mwa Jamii: kiroho na kimwili; huko ndiko kuna watu wengi wanaoteseka zaidi. Kwa njia
hii, waamini wataweza kuwatambua na kumtambua Kristo kati yao! Alhamisi kuu jioni,
akaadhimisha Misa Takatifu; kumbu kumbu ya Siku ile Yesu alipoweka Sakramenti Takatifu
ya Daraja na Ekaristi Takatifu; sakramenti zinazomwilishwa katika huduma ya upendo.
Papa Francisko, akawaosha miguu watoto wa gereza la watoto watukutu la Casal del Marmo
lililoko mjini Roma.
Ijumaa kuu, katika Maadhimisho ya Njia ya Msalaba kuzunguka
Magofu ya Colosseo mjini Roma, Baba Mtakatifu akawakumbusha waamini kwamba, Msalaba
wa Yesu ni jibu la wema wa Mungu dhidi ya ubaya. Hii ni chemchemi ya matumaini ya
Kikristo yanayotangaza upendo wa Mungu kwa njia ya Ufufuko wa Kristo aliyeshinda dhambi
na mauti, ndivyo alivyowakumbusha waamini katika Kesha la Pasaka.
Akitoa baraka
na ujumbe wake kwa mji wa Roma na Dunia kwa ujumla "Urbi et Orbi", akawaalika waamini
kutoa nafasi kwa Yesu Kristo ili aweze kuwaletea mabadiliko ya ndani, ili waweze kuwa
ni vyombo vya huruma ya Mungu, ili haki, amani upendo na mshikamano viweze kutawala
dunia.
Katika Ibada za Misa Takatifu na waamini mbali mbali kwenye Kikanisa
cha Domus Sanctae Martha amekazia kwa namna ya pekee: majadiliano ya kiekumene; kipaumbele
kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii; changamoto ya Uinjilishaji
mpya kwa njia ya ushuhuda wa maisha na kwamba, waamini walei wanachangamotishwa kuyatakatifuza
malimwengu, daima wakijitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa Injili ya Kristo.
Baba
Mtakatifu anawaalika waamini kutoogopa bali wamfungulie Kristo malango ya mioyo na
maisha yao; wakitoka kifua mbele kumtangaza Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka
katika wafu. Akiwa kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano, Baba Mtakatifu
anawaalika waamini kushikamana Askofu wao ili kuwashirikisha wengine ile furaha ya
Kristo Mfufuka, kwani daima yuko pamoja nao katika hija ya maisha yao ya kila siku.
Kwa
ufupi, Baba Mtakatifu Francisko ni mtu wa maneno machache, lakini matendo yake yanazungumza
zaidi hata ya kile ambacho tumejaribu kuweka kwa muhtasari, Kanisa linapofanya kumbu
kumbu ya Mwezi mmoja, tangu Baba Mtakatifu Francisko alipochaguliwa kuliongoza Kanisa
Katoliki kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.
Imehaririwa na Padre Richard Mjigwa,
C.PP.S Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.