2013-04-13 12:09:50

Mheshimiwa Padre Godfrey Igwebuike Onah ateuliwa na Papa kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki Nsukka, Nigeria


Baba Mtakatifu Francisko tarehe 13 Aprili 2013 amekubali ombi la Askofu Francis Emmanuel Ogbonna Okobo wa Jimbo la Nsukka, Nigeria kutoka madarakani. Baba Mtakatifu amemteua Mheshimiwa Padre Godfrey Igwebuike Onah, Makamu wa Gombera, Chuo Kikuu cha Kipapa cha Urbaniana na mshauri katika Sekretarieti ya Sinodi ya Maaskofu kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki la Nsukka, Nigeria.

Askofu mteule Godfrey Onah alizaliwa tarehe 18 Agosti 1956 mjini Enugu. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kipadre, akapewa Daraja takatifu la Upadre tarehe 28 Julai 1984 kama Padre wa Jimbo Katoliki la Enugu na kunako mwaka 1990 lilipoanzishwa Jimbo Jipya la Nsukka, akahamia huko.

Katika maisha na utume wake kama Padre amekuwa ni Paroko Msaidizi, Jalim, Mtafiti na Padre mshauri wa Chama cha Kitume cha Utamaduni wa Kanisa. Amewahi kuwa mkurugenzi wa taasisi ya tafiti na tamaduni ya Kitivo cha Falsafa, Chuo Kikuu cha Kipapa cha Urbaniana, Roma.

Tangu mwaka 2003 hadi mwaka 2008 ameshiriki katika Maadhimisho ya Sinodi za Maaskofu hapa mjini Roma. Kunako mwaka 2008 akateuliwa kuwa ni Makamu wa Gombera, Chuo Kikuu cha Kipapa cha Urbaniana, kilichoko mjini Roma.







All the contents on this site are copyrighted ©.