Chuo kikuu kinapaswa kuwa ni mahali pa matumaini kwa vijana wa kizazi kipya
Kardinali Tarcisio Bertone katibu mkuu wa Vatican katika maadhimisho ya Siku ya Chuo
Kikuu cha Kikatoliki cha Moyo Mtakatifu wa Yesu, Jumapili, tarehe 14 Aprili 2013,
amewasilishana salam na matashi mema kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko anayewataka
wadau mbali mbali kuendeleza ari na moyo uliopelekea hata Padre Agostino Gemelli,
akaanzisha Chuo hiki, ambacho kina umaarufu wa pekee nchini Italia kutokana na rejea
yake kwa majiundo makini kwa vijana wa kizazi kipya katika medani mbali mbali za maisha.
Maadhimisho haya yanayofanyika kila mwaka, yawe ni kielelezo anasema Kardinali
Bertone cha: umoja na mshikamano na wadau mbali mbali pamoja na vitivo vilivyoko chini
ya Chuo Kikuu cha Moyo Mtakatifu wa Yesu; daima wakiendelea kuwa waaminifu kwa malengo
na utambulisho wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki katika kuwaandaa vijana ili kukabiliana
na changamoto mbali mbali za maisha kwa njia ya majiundo makini, tafiti, semina na
machapisho yanayotolewa Chuoni hapo. Msukumo wa pekee ni kuwa karibu na vijana hasa
wakati huu wanapokabiliana na athari za myumbo wa uchumi kimataifa.
Kardinali
Bertone anakumbusha kwamba, mtikisiko huu umewagusa vijana wengi kiasi kwamba, wale
wanaojiunga na vyuo vikuu nchini Italia wamepungua kwa kiasi na wengi wanaohitimu
masomo yao hawana uhakika wa kupata fursa za ajira. Zote hizi ni changamoto zinazopaswa
kufanyiwa kazi kwa kina na mapana ili kupatiwa ufumbuzi wake kwa ajili ya ustawi na
maendeleo ya Italia na watu wake. Kuna haja ya kuendeleza mshikamano na Kanisa pamoja
na vyama vya kitume katika utekelezaji wa majukumu yake.
Kanisa limejitahidi
kutoa kipaumbele cha pekee katika maisha na utume wa vijana, likiwataka kukabiliana
na changamoto za maisha yao katika misingi ya imani, kwa kushiriki kikamilifu katika
maisha na utume wa Kanisa pamoja na kujizatiti katika masomo kwani hili ndilo jambo
la kwanza linalopaswa kupewa msukumo wa pekee.
Kardinali Bertone, anasema,
Baba Mtakatifu Francisko anawaalika vijana kuwa na ari na matumaini mapya na kwamba,
Chuo kikuu ni mahali ambapo vijana wanatua nanga ya matumaini yao kwa ustawi na maendeleo
ya leo na kesho iliyo bora zaidi. Utu na heshima ya binadamu, mafao ya wengi; uwiano
mzuri kati ya imani na uwezo wa mwanadamu wa kufikiri na kutenda ni kati ya mambo
yanayopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza, pamoja na kuzingatia maadili katika tafiti
kama sehemu ya majiundo makini ya vijana wa kizazi kipya.