Balozi Mpya wa Vatican apokelewa kwa shangwe nchini Kenya
Askofu mkuu Charles Daniel Balvo, Balozi wa Vatican nchini Kenya, Ijumaa asubuhi aliwasili
rasmi nchini Kenya kuanza utume wake kama Balozi wa Vatican kwa kusema kwamba, anayo
furaha kubwa kutekeleza utume na dhamana yake miongoni mwa Familia ya Mungu Barani
Afrika na kwa namna ya pekee, nchini Kenya.
Anasema kabla ya kuondoka mjini
vatican alipata nafasi ya kukutana na kusalimiana na Baba Mtakatifu Francisko. Waamini
na watu wenye mapenzi mema sehemu mbali mbali za dunia wamempokea kwa mikono miwili
Baba Mtakatifu Francisko na wengi wanaonesha kuguswa na maisha na unyenyekevu wake.
Baba Mtakatifu amekuwa akiadhimisha Ibada za Misa Takatifu pamoja na kutembelea
makundi mbali mbali ya watu kama njia ya ujenzi wa Jumuiya inayoinjilisha kwa njia
ya ushuhuda wa maisha halisi. Baba Mtakatifu amemtia moyo kwa utume wake mpya nchini
Kenya.
Kardinali John Njue, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya ni kati
ya viongozi wakuu wa Kanisa waliofika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta
kumpokea Askofu mkuu Charles daniel Balvo, aliyeteuliwa na Baba Mtakatifu mstaafu
Benedikto wa kumi na sita mapema mwezi Januari kuwa Balozi Mpya wa Vatican nchini
Kenya.
Kardinali Njue anasema, Balozi wa Vatican amewasili wakati muafaka
kwani Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya linaanza mkutano wake wa Mwaka. Ni matumaini
yake kwamba, Askofu mkuu Balvo ataweza kupata nafasi ya kukutana na kuzungumza na
Maaskofu Katoliki wa kenya wakati wa mkutano wao. Kanisa nchini Kenya linamkaribisha
Balozi wa Vatican kwa mikono miwili ili kujenga na kudumisha umoja, udugu na mshikamano
wa Kikristo.