Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya tatu ya Kipindi cha Pasaka
Mpendwa mwana wa Mungu tunaendelea katika furaha ya Pasaka, furaha kwa ajili ya kukombolewa
toka katika utumwa wa shetani. Tayari tuko Dominika ya tatu ya Kipindi cha Pasaka,
na ujumbe wa Neno la Mungu kwa kifupi unatuambia kuwa, Neno la Kristo mfufuka linaongoza
Jumuiya ya Kikristo.
Mpendwa tunaona
katika Somo la kwanza kuwa Jumuiya ya kwanza ya Kikristo ilikabiliana na upinzani
mkubwa lakini wakitii Neno la Mungu wanasima kidete na wanabaki imara pamoja na mateso
watakayoteseka. Tunamwona Mtakatifu Petro kiongozi mkuu wa Jumuiya akisema, yatupasa
kumtii Mungu kuliko binadamu. Kama ambavyo Kristo mbele ya Wayahudi alionekana mkorofi,
ndivyo ambavyo Mitume wanaonekana mbele ya Jumuiya hiyo. Pengine hata leo Wakristo
tunaonekana hivyo mbele ya watu tunapodai haki na kutii ukweli wa Mungu.
Lakini,
Je, ukweli ndo huo wa kuonekana wakorofi? Hapana, Mitume hawakuwa katika mlengo wa
ukorofi bali katika kupambana na uovu kinyume na haki, kinyume na Injili ya wokovu,
Injili ya ukweli. Kwa kuwa Bwana alimtii Baba yake na akaweza kwa njia ya utii huo
kutupatia wokovu, vivyo na Mitume wakafuata nyayo zake, nasi yatupasa bila kurudi
nyuma kuitikia mwaliko wa Mungu unaotujia kila siku kwa njia ya Neno lake.
Katika
kutii lazima tutambue mambo muhimu ya kufanya, jambo la kwanza ni kwamba Yesu Kristo
ndiye aliyechinjwa sadaka na yuko katika kiti cha enzi na kwa namna hiyo anao uwezo
wote wa kujibu maswali na hoja zote zitokazo katka moyo wa mwanadamu. Yeye ni Mwanga
wa kujua matukio yanayotukia katika historia. Jambo hili liliwaongoza Mitume na Jumuiya
ya kwanza katika kukabiliana na upinzani katika utume wao wa kuendeleza kazi ya Bwana.
Kwa kujua hilo waliweza kusema yatupasa kumtumikia Mungu na si shetani wala mwanadamu.
Katika
Injili Bwana anawatokea mara ya tatu Mitume na bado hawamtambui! Hiki ni kichekesho.
Katika Injili ya Luka 5: 1-11 alishawaambia kuwa mtakuwa wavuvi wa watu, inashangaza
bado wako katika uvuvi! Kwa nini wanarudia kazi yao ya zamani? Laonesha hali ya mwandamu
ya kutaka kurudi katika dhambi! Baada ya ufufuko alishawatokea mara ya kwanza na
mara ya pili na bado hawajaweza kumtambua, ni kweli utambuzi wa Bwana unadai hatua
kwa hatua na hivi watafikia kilele cha utambuzi wa Bwana baadaye.
Mpendwa,
jambo hili si la ajabu kwetu, kwa maana nasi kila Dominika katika Misa Yesu yu pamoja
nasi lakini bado wakati fulani anapotokea tunajikuta katika hali ya kutomtambua. Hata
hivyo mwaliko kwetu unakujia kwa njia ya Neno lake ni kwamba lazima tuongozwe na Neno
hilohilo ili kufikia ukamilifu wa ukweli.
Mpendwa msikilizaji, tunapoongozwa
na Neno la Kristo mfufuka yatupasa kufikiri na kutafakari sana ili daima tupige hatua
mbele badala ya kurudi nyuma. Katika Injili ya leo zipo alama ambazo Bwana anazitumia
ili tupate kuelewa vema maongozi yake. Tunaona katika chombo yaani mtumbwi kuna watu
saba, na namba saba katika Biblia ni namba huwakilisha ukamilifu, kumbe Mitume wanawakilisha
wafuasi wa Kristo ambao wanapaswa wapambane na nguvu za giza katika umoja na ukamilifu
wao.
Nguvu za giza ambazo wanapaswa kupambana nazo zinaoneshwa kwa alama ya
bahari. Na kwa namna hiyo kuwavua watu kama Bwana anavyosema ni kuwatoa katika nguvu
za giza, ili waingie katika nguvu ya upendo. Hiyo ndiyo Pasaka yaani kumfuata Bwana
ambaye yuko juu ya ardhi akiwaalika watu wamfuate. Mitume walivua samaki na kukosa,
hili latuonesha hali ya kujitenga na Mungu haitupatii neema na zawadi mbalimbali za
Kimungu bali kubaki katika baa la njaa yaani ukosefu wa neema zake, na kinyume chake
ni kukaa na Mungu.
Mpendwa mwana wa Mungu, wanapomsikiliza Bwana na kusadiki
wanapata samaki wengi na namba ya samaki waliowapata yaani 153 yatuonesha ukamilifu
wa Jumuiya, na hivi kazi ya Jumuiya ya Kikristo ni kuvua watu wote pasipo kumbakiza
hata mmoja na kwa namna hiyo kuwapeleka kwa Bwana.
Tunaendelea kuona alama
nyingine ambazo ni za maana katika kuelewa na kulifuata Neno la Mungu. Bwana yuko
nchi kavu na ametayarisha samaki na mkate, hii ni alama yakwamba mwisho wa safari
Kristu amewatayarishia watoto wake chakula cha uzima, furaha ya mbinguni, furaha ya
milele. Mitume saba waliokuwa katika chombo wanaleta samaki kwa Bwana, yaani ndivyo
kila mmoja wetu atakavyodaiwa kuwasilisha kwa Mungu matunda ya kazi yake ya kitume
hapa duniani. Mkate utaletwa na Bwana na si Mitume kumbe yeye ndiye Ekaristi Takatifu,
ndiye atupatiaye Komunio ya uzima, chakula cha Mkristo akisafiri kwenda mbinguni.
Neno
la Mungu ni zawadi na taa ya maisha yetu, hutupa mwongiozo na kwa njia yake tunapata
mwongozo jinsi ya kusimamia taifa lake. Akitaka kumkabidhi Mt. Petro mamlaka ya juu
katika Kanisa atamwita na kumwuliza mara tatu, alama ya ukamilifu, akisema Je Petro
wanipenda? Na jibu la Mt. Petro ni jibu la upole na unyenyekevu ndiyo Bwana wewe wajua
kuwa nakupenda.
Na kisha jibu hilo Bwana anamwambia lisha kondoo wangu! Bwana
alimwuliza Bwana mara tatu akitaka kuthibitisha imani ya Mtume Petro na uongofu mkamilifu
maana kabla ya mateso ya Bwana alimkana mara tatu! Anataka na kudai upendo usi ona
sheria, upendo unaozidi yaani kujitoa pasipo kulazimishwa kwa ajili ya wengine. Katika
wajibu huo wa Mt. Petro huko mbele umejaa mateso na kufungwa hata kufa msalabani kwa
ajili ya Bwana na kondoo wake. Sisi tukiongozwa na Neno la Mungu wito wetu ni kuchunga
familia ya watu wa Mungu.
Mpendwa msikilizaji nikutakie furaha ya Pasaka endelevu,
ukiliweka Neno la Mungu mbele yako daima na hivi ukichunga kondoo uliokabidhiwa, ukijua
kuwa kuna mateso katika maisha ya kumfusa Bwana kwa upendo mkamilifu, lakini tumaini
likiwa katika Bwana na ukakika ni kwa nia ya Injili yake.
Tumsifu Yesu Kristo.
Tafakari
hii imeletwa kwako na Pd. Richard Tiganya C.PP.S.