2013-04-12 08:31:13

Padre Luca Passi kutangazwa Mwenyeheri tarehe 13 Aprili 2013


Kardinali Angelo Amato, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la kuwatangaza waamini kuwa wenyeheri na watakatifu, kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 13 Aprili 2013 ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumtangaza Padre Luca Passi, mwanzilishi wa Shirika la Watawa Walimu wa Mtakatifu Dorothea kuwa Mwenyeheri. Ibada hii itafanyika kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Marco, Jimbo kuu la Venezia.

Kardinali Amato anasema, Padre Luca alizaliwa kunako tarehe 22 Januari 1789. Ni mtoto wa kwanza kati ya watoto kumi na mmoja wa Mzee Enrico Passi na Mama Caterina Corner, aliyekuwa anaitwa na majirani zake "Mama wa Maskini". NI Familia iliyokuwa imejengeka katika msingi thabiti wa imani, maadili na utu wema. Familia ilikuwa na uwezo mkubwa kiuchumi, lakini utajiri wa Familia haukuwa ni kizuizi kwa Padre Luca kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya Mungu na jirani kwa njia ya wito na sadaka ya maisha ya Kipadre. Katika maisha na utume wake kama Padre, alitumia utajiri wa familia kwa ajili ya kuwasaidia maskini zaidi na kuyatakatifuza malimwengu.

Ni Padre aliyekuwa makini na mwenye mvuto, aliyeweza kuhibiri kwa kitambo kirefu bila kuchoka wala kuwachosha wasikilizaji wake. Alikuwa anaaalikwa kwenye Parokia mbali mbali ili kuhubiri Neno la Mungu; akatenga muda wa kuendesha mafungo ya kiroho katika kipindi cha Kwaresima na miezi ya Ibada kwa Bikira Maria. Alishiriki katika kuendesha novena, hija na Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu kwa muda wa masaa arobaini. Daima alipokuwa anahitimisha utume wake, aliwakumbusha waamini kwamba, Mwenyezi Mungu anawataka wawe ni watakatifu.

Katika mahubiri yake, alikuwa na litania ya mambo ambayo yanaweza kumsaidia mwamini kuwa ni Mkristo kweli kwa njia ya ushuhuda wa maisha yake; kila mtu kadiri ya maisha, wito na taaluma yake. Alikuwa na neno la ushauri kwa Watu wa Ndoa na Familia; Mapadre na Watawa, Vijana na Watoto. Kila mtu alimpatia ushauri kadiri ya hali yake na wengi waliupokea na kuridhika nao!

Mwenyeheri Padre Luca Passi wakati wa mahubiri yake, aliwaacha wasikilizaji wake wakiwa wameshika tama kwa kusikiliza kwa umakini mkubwa. Wengi waliweza kutubu na kuongoka, wakabadilisha maisha yao na kuwa ni watu wema zaidi. Waamini waliokuwa wavivu kuhudhuria Ibada ya Misa Takatifu, waliguswa na kuonja huruma, upendo na msamaha wa Mungu katika maisha yao na kuanza mchakato wa kutafuta Mlango wa Kanisa. Waamini wengi walijitahidi kutubu na kumpokea Yesu katika Sakramenti Takatifu ya Ekaristi.

Mwenyeheri Padre Luca Passi alikuwa na utume wa pekee kabisa miongoni mwa vijana. Ili kufanikisha lengo hili alianzisha Shirika la Mtakatifu Dorothea ili kuimarisha imani, matumaini na mapendo ya vijana kwa Mwenyezi Mungu. Hawa ni vijana ambao hawakubahatika kupata elimu, kumbe hii ilikuwa ni fursa ya kuwapatia majiundo ya maisha ya kiroho. Alijitaabisha kuhakikisha kwamba, anawajengea vijana uwezo wa kiuchumi na kimaadili kwa kuanzisha Shirika la Mtakatifu Raffaele, msaada mkubwa kwa vijana waliokuwa wanaishi vijijini.

Kilele cha maisha na utume wa Mwenyeheri Padre Luca Passi ni hapo tarehe 6 Agosti 1838, akiwa Venezia, mahali alipoanzisha Shirika la Masista Walimu wa Mtakatifu Dorothea, Shirika ambalo hadi leo hii liko imara na linasonga mbele kuwasindikiza na kuwasaidia vijana kwenda kwa Yesu Kristo.

Kardinali Angelo Amato anasema, Mtakatifu Dorothea ni shahidi aliyeyamimina maisha yake kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake, kunako karne ya tatu. Lakini muda mfupi kabla ya kuuwawa na watesi wake, alikuwa amefanikiwa kuwaongoa vijana wawili ambao kutokana na madhulumu waliyokuwa wanakabiliana nayo, walishindwa na kuanza kumkana Kristo. Hata yule askari aliyekuwa amepewea dhamana ya kuwadhulumu, alitubu na kumwongokea Kristo.

Kardinali Angelo Amato anasema, hata vijana wanahamasishwa kuwa ni Wamissionari wa Kristo kwa vijana wenzao, kama alivyokuwa Mtakatifu Dorothea nchini kwake, Uturuki.







All the contents on this site are copyrighted ©.