Mshikamano wa upendo na maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii
Mfuko wa Papa ulianzishwa na Hayati Kardinali John Krol aliyeishi kunako mwaka 1910
hadi mwaka 1996 na una Makao yake Makuu mjini Philadelphia, Pennsylvania, Marekani.
Lengo lilikuwa ni kumjengea uwezo wa kiuchumi Baba Mtakatifu ili kuonesha mshikamano
wa upendo na huduma kwa waamini sehemu mbali mbali za dunia.
Kila mwaka wanajinyima
na sadaka hii wanaikusanya na kumpelekea Baba Mtakatifu kwa ajili ya mahitaji ya Kanisa
katika kupambana na umaskini wa kipato na maisha ya kiroho kama alivyosema Baba Mtakatifu
Francisko alipokutana na wajumbe wa Mfuko wa Papa mjini Vatican. Wajumbe hawa walipokutana
na Baba Mtakatifu wamemchangia katika kapu lake kiasi cha dolla za Kimarekani 8, 600,
000. Tangu mwaka 1990 hadi leo, jumla ya dolla za Kimarekani millioni 85 zimechangwa
na wanachama wa Mfuko wa Papa.
Hayo yamebainishwa na Kardinali Donald William
Wuerl, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Washington, DC., Marekani ambaye pia ni Rais wa
Taasisi za Misaada za Kanisa Katolikinchini Marekani. Anasema, hizi ni juhudi kidogo
zinazopania kwa namna ya pekee kumsaidia Baba Mtakatifu kuweza kutekeleza utume wake
hasa zaidi miongoni mwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii. Mfuko
wa Papa umetoa fedha kwa ajili ya kusaidia majiundo ya Makleri, Watawa na Waamini
Walei.
Kardinali Donald William Wuerl anasema, wanaendelea kuifanyia kazi changamoto
ya Kanisa kuwa ni maskini kwa ajii ya kuonesha mshikamano wa upendo na maskini katika
mchakato wa kupambana na umaskini wa kipato na maisha ya kiroho.