2013-04-12 15:19:15

Maandiko Matakatifu na Mapokeo ya Kanisa yameshikamana na kushirikiana kwani yote mawili yanabubujika kutoka katika chemchemi ya Kimungu


Uvuvio wa Roho Mtakatifu na ukweli katika Maandiko Matakatifu ni mada nyeti inayogusa undani wa maisha ya Kanisa zima kwani utume na maisha yake yote yanafumbatwa katika Neno la Mungu ambalo ni dira ya taalimungu na uwepo wa Kikristo. Maandiko Matakatifu ni ushuhuda wa Neno la Mungu uliowekwa katika maandishi na kuwa ni sehemu ya kumbu kumbu ya Kanuni ya tukio la Ufunuo.

Kwanza kabisa Neno la Mungu linatangulia na baadaye unafuatia ushuhuda ambao ni Biblia. Imani ya Kanisa inafumbatwa si tu katika Biblia bali katika Historia ya Wokovu inayojikita katika Nafsi ya Yesu Kristo, Neno wa Mungu aliyefanyika mwili pamoja na kutambua kazi ya Roho Mtakatifu anayeliongoza Kanisa ili liweze kufahamu ukweli wote.

Ni maneno ya Baba Mtakatifu Francisko wakati alipokutana na kuzungumza na Wajumbe wa Tume ya Kipapa ya Biblia waliokuwa wanafanya mkutano wao wa Mwaka, wakiongozwa na mada "Uvuvio wa Roho Mtakatifu na Ukweli wa Biblia". Baba Mtakatifu amewashukuru wajumbe hawa kwa kazi kubwa waliyoifanya wakati wote huu.

Anasema, kuna haja ya kuwa na ufahamu mpana zaidi wa Mapokeo hai ya Kanisa ambayo kwa njia ya Roho Mtakatifu na Mamlaka rasmi ya ufundishaji katika Kanisa; Mama Kanisa ametambua na kutamka wazi kwamba, Vitabu vya Kanuni ni Neno la Mungu linalotangazwa kwa Watu wake; kamwe hajaacha kulitafakari na kuendelea kugundua utajiri wake. Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican katika hati yake ya kichungaji Neno la Mungu, "Dei Verbum" unabainisha kwamba, "Kwa kweli hayo yote yanayohusu jinsi ya kufasiri Maandiko Matakatifu yapo chini ya uamuzi wa Mama Kanisa ambaye hutimiza amri ya Mungu na huduma yake ya kuhifadhi na kulifahamu Neno la Mungu." DV. 2.

Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kusema kwamba, "Kwa hiyo Mapokeo Matakatifu na Maandiko Matakatifu yameshikamana pamoja na kushirikiana. Kwa sababu yote mawili yanabubujika kutoka katika chemchemi ileile ya Kimungu na hivyo huungama na kuwa ni kitu kimoja na kuelekea lengo moja. Kwa kweli, Maandiko Matakatifu ndilo Neno la Mungu ambalo liliandikwa kwa uvuvio wa Roho wa Mungu. Neno la Mungu lililokabidhiwa kwa Mitume wa Kristo Bwana na Roho Mtakatifu linarithishwa li zima na Mapokeo Matakatifu kwa waandamizi wao, ili wakiangazwa na Roho wa ukweli, kwa njia ya kuhubiri kwao, walihifadhi kiaminifu, walifafanue na kulieneza. Hivyo Kanisa halichoti uhakika wake juu ya mambo yote yaliyofunuliwa kutokana na Maandiko Matakatifu peke yake. Kwa hiyo Maandiko Matakatifu na Mapokeo matakatifu lazima yapokelewe na kuheshimiwa kwa hisia sawa, za uchaji na heshima." DV. 9.

Baba Mtakatifu anaendelea kusema kwamba, wachambuzi wa Neno la Mungu hawana budi kuwa makini kwa kuhakikisha kwamba, wanaliweka katika imani ya Kanisa. Tafsiri ya Maandiko Matakatifu si juhudi za kisayansi za mtu binafsi, bali zinapaswa kuendana na ukweli wa Mapokeo hai ya Kanisa. Maandiko Matakatifu yamekabidhiwa kwa Jumuiya ya Waamini na kwa Kanisa la Kristo ili kurutubisha imani na kutoa dira ya maisha ya upendo. Kumbe kuna haja ya kuheshimu na kuthamini Maandiko Matakatifu pamoja na Mapokeo Matakatifu katika Familia ya Mungu.

Baba Mtakatifu amehitimisha hotuba yake kwa wajumbe wa Tume ya Kipapa ya Biblia kwa kuwashukuru na kuwapongeza kwa juhudi na kazi kubwa na yenye thamani waliyoitenda. Yesu Kristo Neno wa Mungu aliyefanyika Mwili, akafungua mioyo na akili za wafuasi wake ili waweze kuyafahamu Maandiko Matakatifu, awaongoze daima katika utume wao.

Bikira Maria, kielelezo cha unyenyekevu na utii kwa Neno la Mungu, awafundishe kupokea katika utimilifu wake utajiri mkubwa unaofumbatwa katika Maandiko Matakatifu, dhamana inayopaswa kutekelezwa si tu katika tafiti, bali katika sala na maisha yao yote kama waamini, hasa wakati huu, Mama Kanisa anapoendelea kuadhimisha Mwaka wa Imani, ili kwamba, utume wao usaidie mwanga wa Maandiko Matakatifu kung'ara mioyoni mwa waamini.







All the contents on this site are copyrighted ©.