2013-04-11 15:40:10

Waziri mkuu wa Msumbiji akutana na kuzungumza na Papa Francisko, mjini Vatican


Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 11 Aprili 2013 amekutana na kuzungumza na Bwana Alberto Clementino Vaquina, Waziri mkuu wa Msumbiji ambaye baadaye pia amekutana na Kardinali Tarcisio Bertone, Katibu mkuu wa Vatican pamoja na viongozi wengine waandamizi kutoka Vatican.

Waziri mkuu wa Msumbiji amemtakia heri na matashi mema Baba Mtakatifu Francisko kwa kuchaguliwa kwake kuliongoza Kanisa. Katika mazungumzo baina ya viongozi hawa wawili, wamegusia uhusiano mzuri uliopo kati ya Vatican na Msumbiji, ulioimarishwa kwa namna ya pekee kwa kutiliana sahihi mkataba wa ushirikiano kati ya nchi hizi mbili, hapo tarehe 7 Desemba 2011 na kuridhiwa baada ya mwaka mmoja.

Wamepongeza mchango mkubwa unaotolewa na Kanisa Katoliki nchini Msumbiji katika nyanja mbali mbali za maendeleo na ustawi wa wananchi. Kanisa linaendelea kuchangia kwa namna ya pekee katika sekta ya elimu, afya na maendeleo jamii, amani na utulivu.

Mwishoni Baba Mtakatifu pamoja na mgeni wake Waziri mkuu wa Msumbiji Bwana Alberto Clementino Vaquina wamezungumzia kwa ufupi changamoto na matatizo yanayoukabili Ukanda wa Afrika Mashariki kwa ujumla.







All the contents on this site are copyrighted ©.