Waziri mkuu Pinda abainisha vipaumbele vya Serikali ya Tanzania kwa mwaka 2013/2014
Ifuatayo ni hotuba ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda wa Tanzania kuhusu mapitio na mwelekeo
wa kazi za Serikali ya Tanzania na makadirio ya matumizi ya fedha ya Ofisi ya Waziri
mkuu na Ofisi za Bunge kwa Mwaka 2013/2014
UTANGULIZI
Masuala ya Jumla Mheshimiwa
Spika, naomba kutoa Hoja kwamba kutokana na Taarifa zilizowasilishwa leo na Wenyeviti
wa Kamati za Katiba, Sheria na Utawala; Kamati ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa;
na Kamati ya Uchumi, Viwanda na Biashara na Kamati ya Masuala ya UKIMWI na Dawa za
Kulevya ndani ya Bunge lako Tukufu ambazo zimechambua Bajeti ya Mafungu ya Ofisi ya
Waziri Mkuu, Bunge lako sasa lipokee na kujadili Taarifa ya Mapitio ya Utekelezaji
wa Kazi za Serikali kwa mwaka 2012/2013 na Mwelekeo kwa mwaka 2013/2014. Vilevile,
naliomba Bunge lako Tukufu likubali kupitisha Makadirio ya Matumizi ya Fedha ya Ofisi
ya Waziri Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Taasisi
zilizo chini yake pamoja na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2013/2014.
Mheshimiwa Spika, awali ya yote napenda kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Jakaya
Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa anayoifanya
kwa maslahi ya Nchi yetu. Mheshimiwa Rais ameiletea Tanzania sifa, heshima na kuiwezesha
kutambulika zaidi Kimataifa katika Nyanja mbalimbali. Ziara ya kihistoria ya Mheshimiwa
Xi Jinping, Rais wa Jamhuri ya Watu wa China aliyoifanya Nchini tarehe 24 hadi 25
Machi 2013 ni ushahidi tosha wa kazi nzuri ya Mheshimiwa Rais ya kukuza ushirikiano
wenye maslahi ya kiuchumi kati ya Nchi yetu na Nchi nyingine. Katika ziara hiyo, Mikataba
16 ya ushirikiano katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ilitiwa saini. Utekelezaji
wa Miradi hiyo utachochea uwekezaji na hivyo kuongeza kasi ya ukuaji uchumi na kupunguza
umaskini.
Mheshimiwa Spika, nawapongeza Waheshimiwa
Wabunge waliochaguliwa kuwa Wenyeviti na Makamu Wenyeviti wa Kamati za Kudumu za Bunge.
Vilevile, nawapongeza Waheshimiwa Wabunge waliochaguliwa kuiwakilisha Tanzania katika
Taasisi mbalimbali za Kitaifa na Kimataifa. Ni matumaini yangu kwamba wote walioteuliwa
na kuchaguliwa watatumia nafasi hizo kwa manufaa ya Bunge na kwa maendeleo ya Watanzania
kwa ujumla. Hongereni Sana!
Mheshimiwa Spika, niwashukuru
sana Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala inayoongozwa
na Mheshimiwa Pindi Hazara Chana, Mbunge wa Viti Maalum na Kamati ya Tawala za Mikoa
na Serikali za Mitaa inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Hamisi Andrea Kigwangalla, Mbunge
wa Nzega. Nawashukuru pia Wajumbe wa Kamati ya Uchumi, Viwanda na Biashara inayoongozwa
na Mheshimiwa Mahmoud Hassan Mgimwa, Mbunge wa Mufindi Kaskazini na Kamati ya Masuala
ya UKIMWI na Dawa za Kulevya inayoongozwa na Mheshimiwa Lediana Mafuru Mng’ong’o Mbunge
wa Viti Maalum. Kamati hizo zimetoa mchango mkubwa wakati wa uchambuzi wa Makadirio
ya Mapato na Matumizi ya Fedha ya Mafungu ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Ofisi ya Waziri
Mkuu - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Mfuko wa Bunge. Aidha, nawashukuru
Wajumbe wa Kamati zote za Kudumu za Bunge lako Tukufu kwa ushauri waliotoa wakati
wa kupitia Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara, Mikoa, Wakala, Idara za Serikali
Zinazojitegemea na Mamlaka za Serikali za Mitaa. Maoni na Ushauri wao utazingatiwa
wakati wa kukamilisha mjadala wa Bajeti ya Serikali na utekelezaji wake. Mheshimiwa
Spika, katika kipindi cha mwaka 2012/2013, kumekuwa na majanga na matukio mbalimbali
yaliyosababisha vifo, majeruhi na uharibifu wa mali. Miongoni mwa matukio hayo ni
ajali mbaya ya Jahazi la Sunrise iliyotokea Wangwi katika Bahari ya Hindi mwezi Januari
2013 na ajali mbalimbali za vyombo vingine vya usafiri ambapo watu walipoteza maisha
na wengine kupata majeraha. Hivi karibuni pia tumeshuhudia ajali mbaya ya kuporomoka
kwa jengo la ghorofa 16 Jijini Dar es Salaam ambalo limesababisha vifo vya watu
34 na tukio linguine ni vifo 13 vilivyotokana na kufukiwa na kifusi cha
‘moram’ katika machimbo ya Mushono Jijini Arusha. Aidha, tumempoteza ghafla
Mbunge mwenzetu, Mheshimiwa Salim Hemed Khamis, Mbunge wa Chambani na baadhi yetu
tumepoteza Ndugu, wakiwemo wazazi na watoto kutokana na sababu mbalimbali. Wote nawapa
Pole Sana!
Mzunguko Mpya wa Bajeti Mheshimiwa Spika,
kuanzia mwaka wa fedha 2013/2014, tumekubaliana kuanza Mzunguko Mpya wa Bajeti ambao
utatuwezesha kukamilisha mjadala wa Bajeti ya Serikali mapema. Lengo ni kwamba
ifikapo tarehe 30 Juni ya kila mwaka, taratibu zote za kuandaa, kuchambua na kupitisha
Bajeti ya Serikali ziwe zimekamilika na utekelezaji wa Bajeti kuanza ifikapo
tarehe 1 Julai. Tofauti na miaka ya nyuma ambapo Bajeti ya Serikali ilikuwa ikijadiliwa
na kupitishwa kwanza na kufuatiwa na Bajeti za Kisekta, sasa makadirio na matumizi
ya Wizara yatajadilwa kwanza na hatimaye kuhitimishwa na majadiliano ya kina ya Bajeti
ya Serikali. Moja ya faida kubwa ya utaratibu huu mpya ni kwamba, mwaka mpya wa fedha
unapoanza utekelezaji wa kazi za Serikali unaanza mara moja. Utaratibu huo utawawezesha
Waheshimiwa Mawaziri na Wabunge pamoja na Watendaji wa Serikali kurejea katika kazi
zao na kusimamia kikamilifu utekelezaji wa Bajeti na Mpango wa Maendeleo. Kwa kuwa
tunaanza kwa mara ya kwanza kutumia utaratibu huo hazitakosekana dosari chache ambazo
zitafanyiwa kazi kadri tunavyoendelea kuutumia.
Nawaomba Waheshimiwa
Wabunge kutumia fursa hii kutoa maoni na ushauri utakaosaidia kuboresha Bajeti ya
Serikali ili iwe bora zaidi na yenye maslahi makubwa kwa wananchi wetu.
Mheshimiwa Spika, maandalizi ya Bajeti yamezingatia Ilani ya Uchaguzi ya
Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2010; Mpango wa Kwanza wa Maendeleo wa Miaka Mitano;
Malengo ya Maendeleo ya Milenia na Awamu ya Pili ya Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza
Umaskini. Katika mwaka 2013/2014, Serikali itaendelea kuimarisha usimamizi wa rasilimali
chache tulizonazo ili kutekeleza Miradi ya Maendeleo ya Kipaumbele ambayo itachochea
ukuaji wa haraka wa uchumi.
Mheshimiwa Spika, nachukua
fursa hii kumpongeza sana Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Bwana Ludovick
Utouh, pamoja na wafanyakazi wote wa Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi kwa kazi nzuri wanayoifanya
ya kusimamia rasilimali za Serikali. Matunda ya kazi hii yameonekana hadi nje ya Nchi
na ndiyo maana Ofisi hii sasa imepandishwa hadhi kutoka Daraja la Kwanza hadi la Tatu
kwa vigezo vinavyotumiwa na Muungano wa Ofisi za Ukaguzi wa Hesabu za Serikali katika
Bara la Afrika kwa Nchi zinazotumia Lugha ya Kiingereza.
HALI YA SIASA Mheshimiwa Spika, Nchi yetu imepiga hatua ya kuridhisha katika kuimarisha
Demokrasia ya Vyama vingi. Kwa ujumla hali ya kisiasa Nchini ni tulivu na Vyama vya
Siasa vinaendelea kutekeleza majukumu yake. Idadi ya Vyama vya Siasa vyenye usajili
wa kudumu imefikia 20 baada ya Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC) kupata
usajili wa kudumu. Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMA) kilipata usajili wa muda na
zoezi la uhakiki wa wanachama linaendelea. Chama cha Movement for Democratic and Economic
Change kilifutwa baada ya kukosa sifa za kupata usajili wa kudumu.
Mheshimiwa Spika, ili Demokrasia Nchini izidi kuimarika na Wananchi washiriki
kikamilifu kwenye siasa, Viongozi wote wa Vyama vya Siasa wana wajibu mkubwa wa kuendesha
Siasa za kistaarabu zinazozingatia maadili ya Kitanzania na kufuata Sheria, Kanuni
na Taratibu. Wito wangu kwa Vyama vyote ni kuendelea kuvumiliana na kutohamasisha
siasa za chuki au vurugu ambazo zitatugawa na kuhatarisha Amani, Utulivu na Umoja
wetu ambao umewekezwa kwa miaka mingi. Mwenye Macho haambiwi Tazama. Wote ni mashahidi
wa matatizo makubwa ambayo yamezikumba Nchi zilizoingia katika siasa za chuki na vurugu.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Ofisi ya
Msajili wa Vyama vya Siasa itaandaa mapendekezo ya kufanya mapitio ya Sheria ya Vyama
vya Siasa ya mwaka 1992 na Sheria ya Gharama za Uchaguzi ya mwaka 2010. Aidha, itaendelea
na usajili wa Vyama vya Siasa, kutoa elimu ya Demokrasia kwa Wananchi na kuboresha
Baraza la Vyama vya Siasa. Hatua hizo zitazidi kuimarisha Demokrasia ya Vyama Vingi
Nchini.
ULINZI NA USALAMA
Hali ya Mipaka ya Nchi Mheshimiwa
Spika, kwa ujumla hali ya mipaka ya Nchi yetu ni shwari na Wananchi wanafanya shughuli
zao bila vikwazo. Katika kuimarisha usalama wa mipaka yetu, Viongozi wa Mikoa ya Kagera,
Kigoma, Rukwa na Tanga wamefanya vikao vya ujirani mwema na wenzao wa Mikoa
ya mipakani mwa Nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Rwanda, Burundi, Zambia
na Kenya. Pamoja na hali nzuri ya usalama wa mipaka yetu, bado tunakabiliwa na changamoto
ya Wahamiaji haramu wanaotumia Nchi yetu kama mapito ya kuelekea Nchi nyingine
au kufanya makao Nchini. Ili kukabiliana na tatizo hilo, Serikali inaendesha misako
ya kuwabaini, kuwakamata na kuwafikisha kwenye Vyombo vya Sheria. Serikali pia, imeendelea
kutoa elimu kwa Wananchi wa Mikoa ya mipakani ili kutoa taarifa za Wahamiaji haramu.
Natoa wito kwa Wananchi wote kushirikiana na Serikali kuwabaini na kuwafichua wahamiaji
haramu na wale wanaowasafirisha ili wachukuliwe hatua stahiki za Kisheria.
Hali
ya Uhalifu Nchini Mheshimiwa Spika, Jeshi la Polisi kwa kushirikiana
na jamii kupitia dhana ya Ulinzi Shirikishi inafanya kazi nzuri ya kudhibiti vitendo
vya uhalifu Nchini. Jumla ya makosa makubwa ya jinai yaliyotolewa taarifa katika Vituo
vya Polisi Nchini yalipungua kutoka 69,678 mwaka 2011 hadi 66,255 mwaka 2012. Katika
kipindi cha Januari hadi Februari 2013 makosa ya jinai yalikuwa 10,548 ikilinganishwa
na makosa 10,989 yaliyoripotiwa katika kipindi kama hicho mwaka 2012. Jeshi la Polisi
pia limedhibiti kwa kiasi kikubwa uingizaji wa silaha haramu ambapo jumla ya silaha
405 zilikamatwa katika operesheni mbalimbali kati ya Januari na Desemba 2012. Natumia
fursa hii kulipongeza Jeshi la Polisi kwa kazi nzuri ya kutekeleza kikamilifu dhana
ya Ulinzi Shirikishi na kuwahamasisha Wananchi kuhusu Utii wa Sheria bila Shuruti.
Aidha, napenda kuwakumbusha Wananchi wote kwamba, suala la Ulinzi na Usalama wa Nchi
yetu ni jukumu letu sote. Ni wajibu wetu kutoa taarifa za vitendo vya uhalifu kwa
Jeshi letu ili hatua za kudhibiti vitendo hivyo zichukuliwe.
Mauaji
ya Kishirikina
Mheshimiwa Spika, pamoja na juhudi za Serikali
za kuwahudumia wazee na watu wenye ulemavu, siku za karibuni kumeibuka tena dalili
za vitendo vya ukatili dhidi ya wazee, wanawake na walemavu wa ngozi katika baadhi
ya Mikoa kwa sababu za kishirikina. Ukatili huo siyo tu unyama uliopindukia kwa Binadamu
wenzetu bali pia unaondoa sifa kubwa ya jamii yetu ya kupendana pasipo kujali
rangi, dini au kabila. Nitumie fursa hii kuwahakikishia ndugu zetu wenye ulemavu
wa ngozi, akina mama na wazee kwamba, Serikali haitavumila kuona ukatili wowote unafanywa
dhidi yao.
Naziagiza Kamati za Ulinzi na Usalama za Mikoa na Wilaya
zote Nchini kwa kushirikiana na Jamii kuwabaini na kuwafikisha kwenye Vyombo vya Sheria
wale wote wanaojihusisha na vitendo hivyo viovu.
Migogoro ya Dini Mheshimiwa
Spika, Serikali imetoa uhuru kwa Wananchi wake kuabudu, kila mtu kwa Dini anayoitaka.
Hata hivyo, hivi karibuni kumejitokeza migongano na chokochoko za kidini ambazo zimeanza
kueneza chuki miongoni mwetu. Chokochoko zinazojitokeza si dalili nzuri kwa mustakabali
wa Nchi yetu inayopenda kudumisha Amani, Utulivu na Umoja wa Kitaifa.
Uzoefu
wa Mataifa mbalimbali umeonesha kwamba chokochoko za kidini zimesababisha machafuko
makubwa na kutoweka kwa amani katika Nchi hizo. Tukumbuke kwamba yakitokea machafuko
ya namna hiyo na kuvurugika kwa amani na utulivu, hakuna atakayesalimika. Hivyo, natoa
wito kwa Viongozi wa Madhehebu ya Dini kuelimisha Waumini wao kuthamini na kuheshimu
dini za wengine na kuepuka vitendo vyovyote vinavyoamsha hisia za chuki miongoni mwa
wafuasi wa Dini mbalimbali.
Mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa Mheshimiwa
Spika, katika mwaka 2012/2013, Serikali iliahidi kukarabati na kujenga Makambi kwa
ajili ya kuchukua Vijana watakaojiunga na mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa kwa mujibu
wa Sheria. Ninayo furaha kuliarifu Bunge lako tukufu kuwa Serikali ya Chama Cha Mapinduzi
imetekeleza ahadi ilizotoa mwaka jana kwa ufanisi mkubwa. Mafunzo ya JKT kwa mujibu
wa Sheria yameanza mwaka huu kwa kuchukua Vijana 4,711 sambamba na Vijana 5,893 wa
kujitolea wakiwemo baadhi ya Waheshimiwa Wabunge. Nitumie fursa hii kuwapongeza Waheshimiwa
Wabunge vijana waliojiunga na mafunzo ya JKT mwaka huu. Katika mwaka 2013/2014, Serikali
itaendelea kuchukua vijana kwa ajili ya mafunzo ya JKT kwa Mujibu wa Sheria.
SHUGHULI
ZA UCHAGUZI, BUNGE, VITAMBULISHO VYA TAIFA, SENSA NA MUUNGANO
Tume ya Taifa
ya Uchaguzi Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012/2013, Tume ya Taifa
ya Uchaguzi iliendesha Chaguzi Ndogo za Madiwani katika Kata 29 Tanzania Bara ili
kujaza nafasi wazi za Viti vya Udiwani. Katika chaguzi hizo, Chama Cha Mapinduzi kilishinda
Viti 22, CHADEMA Viti 5 na CUF na TLP Kiti kimoja kimoja. Vilevile, Tume ilifanya
teuzi 15 ili kujaza nafasi zilizokuwa wazi za Udiwani wa Viti Maalum. Katika uteuzi
huo, CCM ilipata viti 10, CHADEMA viti vinne na TLP kiti kimoja. Katika mwaka 2013/2014,
Tume ya Taifa ya Uchaguzi itaboresha Daftari la Wapiga Kura ambapo Awamu ya Kwanza
itakamilika mwezi Desemba, 2013. Uboreshaji huo utawezesha kuchapishwa kwa Daftari
la Wapiga Kura kwa ajili ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2014 na Uchaguzi Mkuu
wa mwaka 2015.
Maandalizi ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Mheshimiwa Spika, uchaguzi wa Serikali za Mitaa ngazi ya Vitongoji, Vijiji
na Mitaa unatarajiwa kufanyika mwezi Oktoba 2014. Kazi za awali za uchaguzi huo zinaendelea
kufanyika ikiwa ni pamoja na kupitia upya Kanuni za Uchaguzi zitakazojumuisha maoni
ya wadau mbalimbali. Ili kufanikisha uchaguzi huo, Halmashauri zote Nchini zinatakiwa
kuanza maandalizi mapema kwa kupitia na kuhakiki orodha ya Vitongoji, Vijiji na Mitaa.
Baada ya kuhakiki orodha hiyo, maombi mapya ya kugawa Vitongoji, Vijiji au Mitaa yawasilishwe
katika ngazi husika kabla ya tarehe 31 Desemba 2013 kwa kuzingatia Sheria na Taratibu
zilizopo.
Shughuli za Bunge Mheshimiwa Spika, katika
mwaka 2012/2013, Bunge limeendelea kutekeleza majukumu yake ya kuisimamia na kuishauri
Serikali katika nyanja mbalimbali. Aidha, Bunge limefanya Mikutano mitatu, kupitisha
Miswada minne ya Sheria na kuridhia Maazimio nane. Katika kuboresha utendaji wa
Kamati za Kudumu za Bunge, Wajumbe wa Kamati hizo walipatiwa mafunzo ya kuwajengea
uwezo ili kumudu majukumu yao vizuri katika nyanja za utafiti, uchambuzi wa Miswada,
Sera na Bajeti, utunzaji wa kumbukumbu na taratibu za uendeshaji wa Bunge. Vilevile,
kuanzia tarehe 4 hadi 7 Desemba 2012 Bunge liliandaa kwa mafanikio Mkutano wa Umoja
wa Mabunge Duniani uliofanyika Dar es Salaam ukiwa na kauli mbiu ya “Vita dhidi ya
Ukatili wa Wanawake”.
Mheshimiwa Spika, ili kuimarisha
utendaji na kuongeza ufanisi, Kamati za Kudumu za Bunge zimefanyiwa mabadiliko makubwa
kwa kuunda Kamati mpya ya Bajeti na kugawanya baadhi ya Kamati. Iliyokuwa Kamati
ya Nje, Ulinzi na Usalama imegawanywa mara mbili na kuwa Kamati ya Mambo ya Nje na
Kamati ya Ulinzi na Usalama. Kamati ya Sheria, Katiba na Utawala imegawanywa na
kuwa Kamati ya Sheria, Katiba na Utawala na Kamati ya Tawala za Mikoa na Serikali
za Mitaa. Vilevile, Kamati zilizokuwepo awali nazo zimeundwa upya na baadhi kuongezewa
majukumu. Ni imani yangu kwamba Kamati hizo, zitatekeleza wajibu wake kikamilifu kwa
maslahi ya Taifa.
Muungano Mheshimiwa Spika, katika
mwaka 2012/2013, Serikali imeendelea kuratibu masuala yote ya Muungano na yasiyo ya
Muungano kwa lengo la kudumisha Muungano na ushirikiano wa Serikali zote mbili. Katika
kudumisha ushirikiano huo, Kikao cha Kamati ya Pamoja ya SMT na SMZ cha kushughulikia
Masuala ya Muungano kilifanyika na kujadili Hoja zinazohusu utafutaji na uchimbaji
wa mafuta na gesi asilia; ushiriki wa Zanzibar katika Taasisi za Nje na katika Jumuiya
ya Afrika Mashariki; Ongezeko la gharama za umeme wa TANESCO kwa ZECO; Usajili wa
vyombo vya moto, malalamiko ya wafanyabiashara wa Zanzibar kutozwa kodi mara mbili
na mgawanyo wa mapato.
Mabadiliko ya Katiba Mheshimiwa
Spika, Tume ya Mabadiliko ya Katiba inaendelea kuratibu, kukusanya na kuchambua maoni
ya Wananchi ili kupata Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayotokana
na ridhaa ya Wananchi wenyewe ifikapo mwaka 2014. Katika mwaka 2012/2013, Tume imekusanya
maoni ya Wananchi kupitia njia mbalimbali na kuanza uchambuzi wa maoni yaliyotolewa
ili kuandaa Rasimu ya Katiba. Tume pia, imeanza maandalizi ya kuunda Mabaraza ya Katiba
katika Ngazi ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa na Mabaraza ya Katiba yanayojumuisha
Asasi, Taasisi na Makundi Maalum ya Watu. Mabaraza hayo yatakuwa na jukumu la kupitia
na kutoa maoni juu ya Rasimu ya Katiba iliyoandaliwa na Tume. Mabaraza ya Katiba yatawashirikisha
na kuwakutanisha wawakilishi kutoka makundi mbalimbali ya wananchi katika jamii.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Tume itaratibu,
Mikutano ya Mabaraza ya Katiba Mpya, kuchambua maoni ya Mabaraza ya Katiba na
kuandaa Rasimu ya Katiba Mpya itakayowasilishwa katika Bunge Maalum la Katiba. Vilevile,
itachapisha Katiba iliyotokana na maoni ya Bunge Maalum la Katiba kwa ajili ya kupigiwa
Kura ya Maoni. Naipongeza sana Tume ya Mabadiliko ya Katiba kwa kazi nzuri waliyoifanya
hadi sasa. Nawasihi Watanzania wote kuendelea kutoa ushirikiano kwa Tume ili iweze
kukamilisha kazi hii muhimu kwa Taifa letu.
Sensa ya Watu na Makazi 2012 Mheshimiwa Spika, mwaka 2012 ulikuwa ni mwaka wa Sensa ya Watu na Makazi
ambayo ni ya tano kufanyika tangu kuasisiwa kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Matokeo yanaonesha kuwa idadi ya watu Nchini imeongezeka kutoka watu milioni 34.5
mwaka 2002 hadi milioni 44.9 mwaka 2012. Hilo ni ongezeko la watu Milioni 10.4 kwa
kipindi cha miaka kumi, sawa na ukuaji wa wastani wa Asilimia 2.7 kwa mwaka. Kwa ujumla
matokeo ya Sensa yanaonesha kasi ya ongezeko la watu ni kubwa ikilinganishwa na kasi
ya ukuaji wa Pato la Taifa. Kwa kutambua changamoto hiyo, Serikali pamoja na mambo
mengine inaendelea kutekeleza Sera ya Idadi ya Watu ya mwaka 2006 kwa kuelimisha Wananchi
kuhusu umuhimu wa Uzazi wa Mpango. Nitumie fursa hii kulikumbusha Bunge lako Tukufu
na Watanzania kazi ya uchambuzi wa takwimu inaendelea ili kupata mchanganuo wa kina
zaidi utakaoiwezesha Serikali kupanga vizuri Mipango yake ya Maendeleo. Katika mwaka
2013/2014, Serikali itasambaza taarifa mbalimbali za Sensa ya Watu na Makazi zenye
mchanganuo wa kitakwimu na kuhamasisha matumizi yake katika tafiti na kuandaa Mipango
ya Maendeleo katika ngazi zote.
Vitambulisho vya Taifa Mheshimiwa
Spika, Tarehe 07 Februari 2013, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania alizindua rasmi Mfumo wa Utambuzi na Usajili wa Watu, Jijini
Dar es Salaam. Vilevile, tarehe 13 Februari 2013, Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamedi Shein,
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, alizindua Zoezi hilo kwa upande
wa Zanzibar. Kuzinduliwa rasmi kwa mfumo huo ni mwanzo wa utoaji wa Vitambulisho vya
Taifa ambavyo vitasaidia kuwatambua na kuwahudumia Wananchi ipasavyo. Zoezi la utoaji
wa Vitambulisho vya Taifa linaendelea kwa watumishi wa umma waliokuwa wamesajiliwa
na kuhakikiwa. Zoezi la kuingiza taarifa za Wananchi 220,000 kwa ajili ya kupatiwa
Vitambulisho vya Taifa katika Wilaya ya Kilombero iliyoteuliwa kuwa Wilaya ya mfano
limekamilika na uchambuzi wa taarifa za Wakazi wa Dar es Salaam 2,159,822 waliojiandikisha
zinaendelea. Aidha, Wakaazi wa Zanzibar 160,645 na Wageni 180 wameandikishwa. Kazi
ya Utambuzi na Usajili wa Watu katika Mikoa mbalimbali Nchini inaendelea sambamba
na utoaji wa Vitambulisho kwa wale walioandikishwa na kuhakikiwa.
MASUALA
YA UCHUMI
Hali ya Uchumi Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012,
Pato halisi la Taifa lilikua kwa Asilimia 6.9 ikilinganishwa na ukuaji wa Asilimia
6.4 mwaka 2011. Sekta zilizochangia zaidi katika ukuaji huo ni pamoja na Mawasiliano,
Fedha, Viwanda, Ujenzi, Madini, Biashara na Utalii. Kutokana na ukuaji huo, Wastani
wa Pato la Mtanzania umeongezeka kutoka Shilingi 869,436 mwaka 2011 hadi Shilingi
995,298 mwaka 2012, sawa na ongezeko la Asilimia 12.6. Mfumuko wa Bei umepungua kutoka
Asilimia 19.4 mwezi Februari 2012 hadi Asilimia 9.8 mwezi Machi 2013. Kupungua
kwa Mfumuko wa Bei kumechangiwa na jitihada za Serikali za kuongeza usambazaji wa
vyakula kwenye masoko, kupunguza ujazi wa fedha kwenye soko, kudhibiti upandaji wa
bei ya mafuta ya petroli na kuimarika kwa upatikanaji wa umeme viwandani ikilinganishwa
na mwaka 2011/2012.
Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano
Mheshimiwa Spika, Serikali inatekeleza Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano
ambao ulipitishwa na Bunge lako Tukufu Mwaka 2011/2012. Katika kutekeleza Mpango huo,
Tume ya Mipango imeweka utaratibu wa kuchambua kwa kina maandiko ya miradi yote
ya kisekta ili kuhakikisha kwamba imezingatia vipaumbele ambavyo sote tumekubaliana.
Baada ya uchambuzi huo, ndipo fedha hutolewa kwa ajili ya utekelezaji. Pamoja na utaratibu
huo, Serikali imeona ni muhimu kuongeza kasi ya utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo
kwa kuanzisha Mfumo imara zaidi wa kupanga Vipaumbele, kufuatilia na kutathmini Utekelezaji
wa Miradi ya Kimkakati ya Maendeleo. Mfumo huo ambao utasimamiwa na Chombo Maalum
(President’s Delivery Bureau) chini ya Ofisi ya Rais, Ikulu, unazingatia uzoefu wa
Nchi ya Malaysia. Chini ya Mfumo huo, Miradi ya kipaumbele itakayotekelezwa itatengewa
fedha za kutosha na usimamizi wa kina utafanyika kuhakikisha kwamba malengo yaliyowekwa
yanafikiwa.
Mheshimiwa Spika, ili Mfumo huo ufanikiwe
inabidi kwanza wadau wote wakubaliane kimsingi vipaumbele ambavyo vitatoa matokeo
makubwa na ya haraka na kisha wataalamu kutoka Serikalini, Sekta Binafsi na Mashirika
Yasiyo ya Kiserikali kukaa pamoja na kuchambua kwa undani vipaumbele hivyo, namna
ya kuvitekeleza, kubaini watekelezaji na kuibua viashiria vya kupima matokeo. Tayari
zoezi hilo la awali limefanyika ambapo maeneo sita ya kwanza ya kipaumbele yamefanyiwa
uchambuzi wa kina kwa utaratibu unaojulikana kama Maabara (Labs). Utaratibu huo wa
maabara unatoa fursa kwa wataalam na watunga Sera kukaa pamoja, kufikiri na kuendesha
majadiliano ya wazi hadi pale wanapokubaliana kwamba ufumbuzi wa tatizo umepatikana.Maeneo
yaliyojadiliwa katika awamu ya kwanza ni Nishati na Gesi Asilia, Uchukuzi, Kilimo,
Elimu, Maji na Kupanua wigo wa Mapato ya Serikali. Baada ya uchambuzi huo kukamilika,
matokeo yake ikiwemo miradi iliyoandaliwa pamoja na Bajeti ya utekelezaji itawekwa
hadharani ili kila Mtanzania ajue kitakachofanyika, kutoa maoni na kufuatilia kwa
kina utekelezaji.
Mheshimiwa Spika, ili kuhakikisha
kwamba kunakuwepo na uwajibikaji wa kutosha katika kutekeleza vipaumbele vya Kitaifa,
Chombo kitakachoanzishwa (President’s Delivery Bureau) kitakuwa na jukumu la kuhakikisha
kwamba kila Waziri wa Kisekta na Watendaji Wakuu wanawajibika kusimamia utekelezaji
wa miradi ya kipaumbele na pia kufanya tathmini za mara kwa mara kupima matokeo. Napenda
kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba, Mawaziri wanaosimamia maeneo sita ambayo tumeanza
nayo walitoa ahadi kwamba watakuwa mstari wa mbele kusimamia kwa weledi utekelezaji
wa miradi ya Sekta zao. Ahadi hizo walizitoa wakati wa uzinduzi wa awamu ya kwanza
ya mfumo wa maabara uliofanywa na Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 22 Februari 2013. Ni matumani yangu kuwa,
utaratibu huo utasaidia sana kuimarisha uwajibikaji, ufuatiliaji na hatimaye kupata
matokeo ya haraka ambayo yatasaidia uchumi kukua kwa kasi zaidi na hivyo kupunguza
umaskini miongoni mwa watu wetu. Ni vyema ieleweke wazi kwamba, maeneo ya kipaumbele
yaliyochaguliwa yatapata sehemu kubwa ya fedha za maendeleo. Hii ndiyo maana ya dhana
ya kupanga ni kuchagua na haina maana kwamba kazi nyingine za uendeshaji wa Serikali
zitasimama. Katika Mwaka 2013/2014, kutafanyika uchambuzi wa kina wa maeneo mengine
ya kipaumbele ambayo yatasaidia Serikali kupanga Bajeti ya Maendeleo kwa mwaka 2014/2015.
Maendeleo
ya Sekta Binafsi na Uwekezaji Mheshimiwa Spika, Serikali inaratibu
utekelezaji wa Mpango Kazi wa Kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji Nchini.
Lengo ni kuimarisha ushiriki wa Sekta Binafsi katika shughuli za uwekezaji na Biashara
Nchini. Katika utekelezaji wa Mpango Kazi huo, Serikali imeazimia kupunguza muda unaotumika
kupitisha mizigo Bandarini na Mipakani kwa kuanzisha utaratibu wa kubadilishana taarifa
zinazohusu mizigo kwa njia za kielektroniki kabla mizigo haijafika kwenye Vituo vya
Forodha. Vilevile, Kamati za Pamoja (Joint Border Post Committees) zimeundwa kwenye
Vituo vya Mipakani vya Tunduma, Kabanga, Mutukula, Holili, Sirari na Namanga. Kupitia
Kamati hizo wadau wote wanaoshughulika na utoaji huduma mipakani hufanya kazi kwa
pamoja.
Mheshimiwa Spika, Serikali imekamilisha Mkakati
na Mpango Kazi wa Utekelezaji wa Sera ya Ubia baina ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi
(PPP). Vilevile, Mwongozo wa Utendaji kwa ajili ya kutekeleza Sera, Sheria na Kanuni
za Ubia baina ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi umekamilika. Aidha, Serikali imefanya
tathmini ya Sera zinazohusu Uwekezaji kwa kutumia Mfumo wa Tathmini unaotumiwa na
Shirika la Kimataifa la Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo (OECD). Taarifa ya tathmini
ya Sera hizo itachangia katika kufanya mapitio ya Sera ya Taifa ya Uwekezaji ya mwaka
1996 pamoja na Sheria yake ya mwaka 1997. Nazihimiza Wizara na Taasisi za Serikali
kuongeza juhudi katika kuainisha miradi inayokidhi vigezo vya kutekelezwa kwa utaratibu
wa PPP ili Nchi iweze kunufaika na fursa zinazotokana na utaratibu huo.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuratibu majadiliano baina ya Sekta
ya Umma na Sekta Binafsi ili kuibua fursa zilizopo na kupata ufumbuzi wa changamoto
za kisera, kisheria na kitaasisi zinazokwamisha biashara na uwekezaji. Kutokana na
umuhimu wa majadiliano hayo, Tanzania itakuwa mwenyeji wa Mkutano wa Kimataifa wa
“Majadiliano ya Ushirikiano kwa Manufaa ya Wote wa mwaka 2013” (Global 2013 Smart
Partnership Dialogue) utakaofanyika mwezi Julai 2013, Jijini Dar es Salaam. Maandalizi
ya Mkutano huo yanaendelea ambapo Mkutano maalum kwa Wakuu wa Mikoa, Wilaya na Makatibu
Tawala wa Mikoa ulifanyika mjini Dodoma mwezi Novemba 2012. Katika Mkutano huo, washiriki
walipata uelewa wa pamoja wa dhana ya majadiliano ya ushirikiano kwa manufaa ya wote
yatakayowasaidia kusimamia majadiliano katika maeneo yao.
Mheshimwa
Spika, Serikali imetoa mwongozo kwa Mabaraza ya Biashara ya Mikoa na Wilaya kuendesha
majadiliano katika maeneo yao ili matokeo ya majadiliano hayo yatumike kikamilifu
wakati wa majadiliano ya Kimataifa mwezi Julai 2013. Uzoefu wa Nchi ambazo zimeandaa
majadiliano kama hayo umeonesha kwamba kuna manufaa makubwa yakiwemo kubaini wagunduzi
na wabunifu, kuibua fursa mpya za teknolojia na uwekezaji na pia kupata uzoefu wa
Mataifa mengine katika masuala mbalimbali. Natoa wito kwa Mabaraza ya Biashara ya
Mikoa na Wilaya kuendesha majadiliano katika maeneo yao na kujiandaa kikamilifu kushiriki
katika Mkutano huo.
Mheshimiwa Spika, katika
kipindi cha Januari 2012 hadi Desemba 2012, Kituo cha Uwekezaji Tanzania kilisajili
Miradi 869 yenye thamani inayokadiriwa kufikia Shilingi Bilioni 30,866. Kati ya miradi
hiyo, Miradi 469 sawa na Asilimia 54 ni miradi ya wawekezaji wa ndani, Miradi 195
sawa na Asilimia 22 ni ya ubia kati ya wawekezaji wa ndani na Nje na Miradi 205, sawa
na Asilimia 24 ni ya wawekezaji kutoka Nje. Usajili wa miradi hiyo umeongeza ajira
Nchini ambapo zaidi ya Watanzania 174,412 walipata ajira kwenye miradi hiyo. Tathmini
ya thamani ya uwekezaji kisekta inaonesha kwamba katika mwaka 2012 miradi ya Sekta
ya Kilimo inaongoza ikiwa imechangia Shilingi Bilioni 14,226 ikifuatiwa na Sekta ya
Uzalishaji Viwandani iliyochangia Shilingi Bilioni 4,672. Sekta hizo zinafuatiwa
na Sekta ya Mawasiliano iliyochangia Shilingi Bilioni 4,663 na Sekta ya Nishati iliyochangia
Shilingi Bilioni 2,110. Pamoja na mafanikio hayo, bado kuna changamoto kubwa ya kufanya
kazi kama Timu moja katika kuvutia wawekezaji. Ili kuweza kuvutia wawekezaji katika
hali endelevu, ni muhimu sana Sera na Sheria za Uwekezaji zikatoa Mwongozo ambao
unatabirika kwa muda mrefu.
Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Mheshimiwa Spika, Serikali imeratibu na kufanya tathmini ya Mifuko mbalimbali
ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi. Mifuko hiyo ni pamoja na Mfuko wa Uwezeshaji wa Mwananchi,
Mpango wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na Kuongeza Ajira, SIDO, SELF, Agriculture
Input Trust Fund na Presidential Trust Fund. Mifuko mingine ni Mfuko wa Maendeleo
ya Vijana, Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake, Mfuko wa Udhamini wa Mikopo kwa Mauzo ya
Nje na Mfuko wa Kudhamini Taasisi za Fedha Kutoa Mikopo kwa Miradi Midogo na ya Kati.
Katika Makubaliano yaliyofikiwa baina ya Serikali na Taasisi za Fedha zilizoteuliwa
kutoa mikopo kwa wajasiriamali ni kwamba Taasisi hizo zikopeshe mara tatu zaidi ya
dhamana iliyotolewa na Serikali. Katika kutekeleza makubaliano hayo, hadi Desemba
2012 Mpango wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na Kuongeza Ajira ulitoa mikopo kwa Wajasiriamali
76,546 yenye thamani ya Shilingi Bilioni 50.06. Urejeshaji wa mikopo hiyo umefikia
wastani wa Asilimia 82. Aidha, katika kipindi hicho, Mfuko wa Uwezeshaji wa Mwananchi
umetoa mikopo ya Shillingi Bilioni 8.6 kwa Mikoa 11, Wilaya 27, Vyama vya Akiba na
Mikopo (SACCOs) 49 na Wajasiriamali 8,497. Ufuatiliaji wa maendeleo ya Mifuko mbalimbali
ya Uwezeshaji unaonesha kuwa Wananchi waliopata mikopo wameweza kupiga hatua za kimaendeleo
kwa kuongeza tija na uzalishaji katika shughuli zao na hatimaye kuongeza kipato na
kuboresha hali zao za maisha.
Mheshimiwa Spika, utekelezaji
wa awamu ya pili ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) ulikamilika mwaka 2012. Tathmini
ya utekelezaji imeonesha kwamba TASAF imetoa mchango mkubwa katika kuwezesha utekelezaji
wa miradi mingi ya maendeleo Vijijini iliyoibuliwa na Wananchi. Katika utekelezaji
wa awamu hiyo, jumla ya Miradi 1,010 yenye thamani ya Shilingi Bilioni 20 iliibuliwa
na kuwezeshwa katika Wilaya za Tanzania Bara na Zanzibar. Aidha, mafunzo ya ujasiriamali
yalitolewa kwa Vikundi 1,778 vyenye wanachama 22,712 katika Halmashauri 44 kwa lengo
la kuviimarisha ili kuongeza ufanisi zaidi katika shughuli zao.
Mheshimiwa Spika, kutokana na mafanikio hayo, tarehe 15 Agosti 2012, awamu
ya tatu ya TASAF ilizinduliwa Mjini Dodoma na Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete,
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Awamu hiyo itakayogharimu jumla ya Shilingi
Bilioni 440 inatekeleza Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini Zilizo Katika Mazingira
Hatarishi. Mpango huo unalenga kuziwezesha kaya maskini kupata chakula na kujiongezea
fursa za kipato kwa kuzipatia fedha ili kumudu mahitaji ya msingi kama vile lishe
bora, huduma za afya na elimu. Mpango huo utakaotekelezwa kwa awamu katika Halmashauri
zote Tanzania Bara na Zanzibar, umeanza kwa utambuzi wa Kaya maskini katika Vijiji
20 vya Halmashauri ya Bagamoyo ambapo jumla ya Kaya 3,056 zimetambuliwa. Zoezi hilo
linaendelea kwenye Halmashauri nyingine 13 na ifikapo Juni 2014, Halmashauri zote
Nchini zitafikiwa.
UZALISHAJI MALI
Kilimo cha Mazao ya Chakula
na Biashara Mheshimiwa Spika, Serikali inatekeleza mipango na mikakati
mbalimbali ya kuongeza tija na uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara. Hatua hizo
ni pamoja na kutekeleza Azma ya KILIMO KWANZA, Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo
(ASDP), Mpango wa Utoaji wa Ruzuku ya Pembejeo na Dawa za Kilimo, Programu ya Kuendeleza
Kilimo katika Ukanda wa Kusini mwa Tanzania (SAGCOT), Programu Kabambe ya Kuendeleza
Kilimo Barani Afrika (Comprehensive Africa Agriculture Development Programme – CAADP)
na kuboresha huduma za ugani na utafiti katika Sekta ya Kilimo. Hatua nyingine ni
pamoja na kuvutia Wawekezaji katika Sekta ya Kilimo, kuhimiza Kilimo cha Umwagiliaji,
kuongeza fursa za upatikanaji wa zana bora za kilimo hasa matrekta, kuimarisha masoko
na kurahisisha upatikanaji wa mitaji kutoka Vyombo vya Fedha, hususan kupitia Dirisha
la Kilimo katika Benki ya Maendeleo Tanzania.
Mheshimiwa
Spika, napenda kulifahamisha Bunge lako Tukufu kuwa jitihada za kuendeleza Kilimo
zimeanza kuleta matumaini hasa katika kuongeza upatikanaji wa Pembejeo za Kilimo na
kuongeza tija na uzalishaji. Kwa mfano, katika mwaka 2012/2013, Tani 226,092 za
mbolea zilifikishwa kwa Wakulima 3,792,000 Nchini na upatikanaji wa mbegu bora
ulifikia Tani 30,443 ikilinganishwa na Tani 28,612 zilizozalishwa mwaka 2011/2012.
Kutokana na ongezeko la matumizi ya mbolea na Wakulima kuzingatia Kanuni za Kilimo
Bora, tija anayopata mkulima katika zao la mahindi chotara kwa sasa ni Wastani wa
Tani 3.9 kwa hekta na tija ya uzalishaji wa zao la mpunga ni Tani 3.8 kwa hekta katika
maeneo ya umwagiliaji.
Mheshimiwa Spika, Serikali
ilianza kutekeleza Mpango wa utoaji ruzuku ya mbolea na mbegu bora kwa kutumia utaratibu
wa Vocha mwaka 2008/2009. Pamoja na mafanikio yaliyopatikana kutokana na utaratibu
huo, hasa kuongezeka kwa upatikanaji na matumizi ya mbolea na mbegu bora pamoja
na tija katika uzalishaji wa mazao ya kilimo, mpango huo umekuwa na changamoto
kadhaa. Changamoto zilizojitokeza ni pamoja na mbolea na Vocha kuchelewa kufika kwa
walengwa; uteuzi wa Mawakala usiozingatia vigezo na udanganyifu uliofanywa na baadhi
ya Mawakala kwa kushirikiana na Watumishi wasio waaminifu pamoja na Wajumbe wa Kamati
za Pembejeo katika ngazi mbalimbali za utekelezaji. Serikali imechukua hatua kwa kufanya
ukaguzi maalum kwenye maeneo yaliyokuwa na upungufu huo na waliobainika kuhusika na
udanganyifu wamefikishwa kwenye Vyombo vya Sheria.
Mheshimiwa
Spika, mwaka jana Serikali iliahidi kufanya mapitio ya Mfumo wa utoaji wa mbolea ya
ruzuku na mbegu bora kwa kutumia utaratibu wa Vocha ili kuondoa upungufu uliojitokeza.
Napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa, Serikali imeboresha mfumo huo na kuanzia
mwaka 2013/2014 ruzuku ya pembejeo za kilimo itatolewa kwa Mikopo kupitia Vikundi
vya Wakulima.
Umwagiliaji Mheshimiwa Spika, katika
mwaka 2012/2013, Serikali imepanua eneo la Kilimo cha Umwagiliaji Nchini. Miongoni
mwa kazi zilizotekelezwa ni pamoja na ujenzi wa miundombinu katika skimu 21 za umwagiliaji
zenye eneo la hekta 19,567. Kazi nyingine zinazoendelea ni kukamilisha ujenzi wa Mabwawa
matano ya Umwagiliaji ya Mahiga (Kwimba); Inala (Tabora); Lwanyo (Mbarali); Mesaga
(Serengeti) na Dongobesh (Mbulu). Miradi mingine iliyotekelezwa ni Skimu 34 zenye
eneo la Hekta 17,824 kwa kutumia Mfuko wa Wilaya wa Kuendeleza Umwagiliaji. Katika
mwaka 2013/2014, Serikali itaanza ujenzi wa mabwawa matatu ya Idodi (Iringa); Manyoni
(Singida) na Masengwa (Shinyanga Vijijini).
Kilimo cha Matunda na
Mboga Mheshimiwa Spika, Kilimo cha matunda na mboga kina mchango
mkubwa katika ukuaji uchumi, fursa za ajira, lishe na kupunguza umaskini. Kwa kuzingatia
umuhimu huo, Serikali inatekeleza Mkakati wa Kitaifa wa Kuendeleza Mazao ya Bustani
wa mwaka 2010/2011 – 2020/2021. Utekelezaji wa Mkakati huo unaolenga kukuza uwekezaji
katika mnyororo wa thamani wa mazao ya bustani; ujenzi wa miundombinu; uhifadhi bora
wa Mazao ya Bustani; ujenzi na utafutaji wa masoko; na ukuzaji rasilimali watu umeanza
kuonesha matokeo mazuri. Uzalishaji wa mazao ya bustani umeongezeka kutoka Tani milioni
4.1 mwaka 2009/2010 hadi Tani milioni 5.1 mwaka 2012/2013 na mauzo ya mazao hayo nje
ya Nchi yameongezeka kutoka Shilingi Bilioni 159.8 mwaka 2009 hadi Bilioni 602.1 mwaka
2012. Mafanikio haya ni ya kuridhisha ingawa bado kuna fursa kubwa ya kuongeza tija
na ufanisi katika sekta hii. Tayari tunao Mwongozo wa Kilimo cha Embe ambao utatuwezesha
kuongeza tija na uzalishaji wa zao hilo. Miongozo ya Uzalishaji bora wenye tija kwa
mazao mengine ya bustani itaandaliwa. Katika mwaka 2013/2014, Serikali itatoa mafunzo
ya teknolojia za uzalishaji wa miche bora ya mazao ya bustani hususan kwa vikundi
vya Vijana.
Mwenendo Wa Bei Za Mazao Makuu Mheshimiwa
Spika, mwenendo wa bei za mazao makuu ya biashara Nchini ambayo ni Pamba, Kahawa,
Chai, Tumbaku, Korosho, Katani na Pareto umekuwa ukibadilika mara kwa mara kwa kutegemea
bei za Soko la Dunia. Mabadiliko hayo yanawaathiri sana wakulima wetu pale bei zinaposhuka.
Kutokana na hali hiyo, Serikali ilikutana na Wadau wa mazao makuu asilia ya biashara
Nchini ili kuangalia uwezekano wa kuanzisha Mfuko Maalum wa kufidia bei za Mazao kwa
wakulima pale zinaposhuka (Price Stabilization Fund). Lengo ni kuwawezesha wakulima
kupata bei nzuri ya mazao na kuwaepusha na hasara inayotokana na kushuka kwa bei hizo
katika masoko ya kimataifa na pia kuwahamasisha wakulima kuendelea kulima mazao husika.
Serikali kwa kushirikiana na Wataalam kutoka Bodi Sita za mazao inayafanyia kazi maoni
ya wadau kuhusu kuanzisha Mfuko Maalum wa Kufidia Bei za mazao.
Mheshimiwa Spika, mwezi Septemba na Novemba 2012, niliongoza Mikutano mikubwa
iliyolenga kuwaleta pamoja Watunga Sera, Washirika wa Maendeleo na Wawekezaji ili
kujadili fursa na changamoto mbalimbali za Sekta ya Kilimo. Katika Mikutano hiyo,
wadau waliandaa na kukubaliana Mpango Kazi ulioainisha majukumu yatakayotekelezwa
na kila mdau ili kuongeza uwekezaji katika Ukanda wa SAGCOT. Majukumu ya Serikali
ni pamoja na upimaji ardhi kwa ajili ya kilimo, ujenzi wa miundombinu ya msingi
na kuondoa vikwazo vinavyokwamisha uwekezaji katika Sekta ya Kilimo. Serikali imechukua
hatua kwa kuainisha na kuweka mipaka ya ardhi kwa kuanzia na Wilaya za Kilombero,
Ulanga na Rufiji. Zoezi hilo la kuanisha ardhi limelenga kutoa kipaumbele cha kwanza
katika upatikanaji wa ardhi kwa ajili ya wakulima wadogo. Hadi sasa ardhi ya Vijiji
100 katika Wilaya ya Kilombero imepimwa.
Mheshimiwa
Spika, wawekezaji wengi wa ndani na nje ya Nchi wameonesha mwamko mkubwa wa kuwekeza
katika ukanda wa SAGCOT. Msisitizo wa Serikali ni kwamba kila mwekezaji mkubwa atakayewekeza
atalazimika kuwa na Mpango wa kuendeleza na kushirikiana na wakulima wadogo. Hatua
hiyo itamsaidia mkulima mdogo kupata teknolojia mpya, uhakika wa pembejeo, miundombinu
ya umwagiliaji pamoja na soko la uhakika. Tayari utaratibu wa namna hiyo umeanza kuonesha
matokeo mazuri Wilayani Kilombero.
Mheshimiwa Spika,
katika hatua nyingine, Washirika wa Maendeleo ambao ni Shirika la Maendeleo la Marekani,
Umoja wa Ulaya na Shirika la Maendeleo la Uingereza wamekubali kusaidia ujenzi wa
barabara yenye urefu wa Kilometa 103 kwa kiwango cha lami ambayo itaunganisha Mikumi
na Ifakara katika Bonde la Kilombero. Hatua za awali za ujenzi wa barabara hiyo zimeanza.
Kukamilika kwa barabara hiyo muhimu kutafungua fursa zaidi za uwekezaji na kurahisisha
usafiri na usafirishaji wa mazao ya wakulima. Nitumie fursa hii kuwashukuru kwa dhati
Washirika wetu hao wa Maendeleo kwa kukubali kusaidia utekelezaji wa mradi huo.
Miundombinu
ya Masoko ya Mazao Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu
wa kuendeleza miundombinu ya masoko ya mazao kama moja ya mkakati madhubuti wa kumrahisishia
mkulima kufikisha mazao yake sokoni na kuongeza bei ya mazao hayo. Chini ya Programu
ya Miundombinu ya Masoko, Uongezaji Thamani na Huduma za Kifedha Vijijini, Serikali,
imekamilisha usanifu na kutangaza zabuni za ujenzi wa barabara zenye jumla
ya Kilometa 210.8 katika Halmashauri za Mbulu, Njombe, Iringa Vijijini, Kahama, Lushoto,
Rufiji, Songea Vijijini na Singida Vijijini. Aidha, zabuni kwa ajili ya ujenzi wa
maghala mawili katika Halmashauri za Wilaya ya Iringa Vijijini na Njombe zimetangazwa
na taratibu za ujenzi wa ghala katika Halmashauri ya Mbulu zinakamilishwa. Katika
mwaka 2013/2014, Serikali itaendelea na ujenzi wa barabara na miundombinu mingine
ya masoko Tanzania Bara na Zanzibar.
Maendeleo ya Sekta ya Mifugo Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012/2013 Serikali imeanza kutekeleza Programu
ya Miaka Mitano ya Kuendeleza Sekta ya Mifugo (2011/2012 – 2015/2016). Programu hiyo
inalenga kuwa na Sekta ya Mifugo ya kisasa itakayoongeza ukuaji wa Sekta kutoka Asilimia
2.3 hadi 4.5 kwa mwaka ifikapo mwaka 2016. Ili kufikia malengo hayo, Serikali pamoja
na mambo mengine, imezielekeza Halmashauri zote Nchini kufanya tathmini ya uwezo wa
ardhi katika maeneo yao ili kufuga kulingana na uwezo wa eneo lililopo.
Mheshimiwa Spika, Serikali pia imeboresha huduma za uhamilishaji pamoja
na kutoa Ruzuku ya Dawa za Kuogesha Mifugo Lita 92,323 zenye thamani ya Shilingi
Bilioni 1.5 ambazo zimesambazwa katika Mikoa yote ya Tanzania Bara. Hatua hiyo imekwenda
sambamba na kujenga Majosho Mapya 14 na kukarabati Majosho 20 katika Mikoa ya
Arusha, Iringa, Kagera, Lindi, Mara, Mbeya, Mwanza, Katavi, Rukwa, Ruvuma, Simiyu,
Singida, Geita na Tanga. Vilevile, Serikali imetoa mafunzo ya unenepeshaji mifugo
kwa Wafugaji wanaozunguka Ranchi za Taifa. Pia, Miradi 13 ya unenepeshaji mifugo imeibuliwa
kupitia Mipango ya Maendeleo ya Kilimo ya Wilaya katika Mikoa ya Arusha, Dodoma, Manyara,
Mwanza, Shinyanga na Singida. Hatua hiyo imeongeza idadi ya Ng’ombe walionenepeshwa
kutoka 132,246 mwaka 2011 hadi Ng’ombe 150,000 mwaka 2012. Aidha, Vijiji 781 vya
Halmashauri za Wilaya 80 katika Mikoa ya Iringa, Mbeya, Morogoro, Pwani, Katavi, Rukwa,
Ruvuma na Singida vimepimwa ili kuepusha migogoro ya mara kwa mara kati ya wafugaji
na watumiaji wengine wa ardhi.
Mheshimiwa Spika,
katika mwaka 2013/2014, Serikali itaendelea kutekeleza Programu ya Kuendeleza Sekta
ya Mifugo ili itoe mchango mkubwa zaidi katika uchumi. Aidha, itakamilisha ujenzi
wa Mfumo wa Utambuzi na Ufuatiliaji Mifugo ambao unatarajiwa kuanza kazi mwezi Agosti
2013. Vilevile, itaimarisha uhamilishaji Nchini kwa kuzalisha Dozi za mbegu bora za
uhamilishaji.
Maendeleo ya Sekta ya Uvuvi Mheshimiwa
Spika, katika mwaka 2012/2013, Serikali imeanza kupitia Sera ya Taifa ya Uvuvi ya
mwaka 1997 na kuandaa Mkakati wa utekelezaji. Lengo ni kuihuisha Sera hiyo ili iendane
na mabadiliko ya Kiuchumi na Kijamii yaliyojitokeza pamoja na kuzingatia maendeleo
ya Sayansi na Teknolojia katika Sekta ya Uvuvi. Katika mwaka 2013/2014, Serikali itakamilisha
kupitia Sera ya Taifa ya Uvuvi ya mwaka 1997 na kuendelea kuimarisha usimamizi wa
rasilimali za uvuvi. Aidha, Vikundi vya Ulinzi Shirikishi vya Kudhibiti Uvuvi Haramu
na Vituo vya Doria vitaimarishwa. Serikali pia itaendelea kusimamia shughuli za ukuzaji
wa viumbe kwenye maji ikiwa ni pamoja na kuanzisha vituo vipya vya kuzalisha vifaranga
vya samaki.
Ufugaji Nyuki Mheshimiwa Spika, Uzalishaji
wa Asali na Nta kwa miaka ya hivi karibuni unatupa moyo kwamba, Ufugaji wa Nyuki unaweza
kuwa ni shughuli ya kiuchumi inayoweza kuwaongezea Wananchi wetu kipato na kuwaondolea
umaskini. Katika kipindi cha miaka minne iliyopita 2009 - 2012, uzalishaji wa Asali
ulifikia Wastani wa Tani 8,747 na Nta Tani 583. Katika juhudi za kuongeza uzalishaji,
Serikali imetoa elimu ya ufugaji nyuki katika Wilaya za Kahama (Vijiji 7), Chunya
(Vijiji 4), Same (Vijiji 2), Manyoni (Vijiji 3), Singida (Vijiji 2) na Kibondo (Vijiji
13). Aidha, Mizinga 500 imesambazwa katika Wilaya za Ruangwa, Mtwara, Newala, Tunduru
na Namtumbo ambapo kila Wilaya ilipata Mizinga 100. Pamoja na juhudi hizo, Hekta 56,290
zimepimwa kwa ajili ya kutenga hifadhi za nyuki katika Vijiji mbalimbali Nchini.
Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia umuhimu wa Sekta ndogo ya Ufugaji Nyuki
kwa maendeleo ya Wananchi, niliahidi kwamba yatafanyika Maonesho Maalum ya Ufugaji
Nyuki. Maonesho hayo yamefanyika Kitaifa Jijini Dar es Salaam, tarehe 4 - 7 Oktoba
2012 katika Viwanja vya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambapo yalitanguliwa na Kongamano
lililofanyika tarehe 3 Oktoba 2012. Kauli Mbiu ya Maonesho ilikuwa ni “ASALI KWA
AFYA NA USTAWI”. Maonesho hayo yameleta chachu na matumaini makubwa ya kukua kwa biashara
ya mazao ya Nyuki kwani tangu kumalizika, Wafugaji Nyuki wa Tanzania wamepata soko
la kuuza zaidi ya Tani 100 za Asali Nchini Ujerumani. Aidha, Wajasiriamali wengi wamepata
Alama ya Utambulisho wa Biashara (Barcode) kwa ajili ya kutambulisha Asali yao. Vilevile,
kutokana na wananchi kuhamasika kufuga nyuki, Serikali imeanza kutengeneza mizinga
bora ipatayo 70,000, kuiwekea chambo na kuisambaza kwa wananchi kwa gharama nafuu.
Mheshimiwa Spika, kutokana na umuhimu wa Sekta ya Nyuki, kwa mara
ya kwanza Tanzania iliadhimisha siku ya Kitaifa ya Kutundika Mizinga, tarehe 4 Machi
2013 katika Hifadhi ya Aghondi iliyopo Wilayani Manyoni Mkoa wa Singida. Katika uzinduzi
huo, Wadau walipata nafasi ya kutambua fursa kubwa zilizopo katika Sekta hiyo na kujenga
mahusiano ya karibu ya kibiashara. Katika mwaka 2013/2014, Serikali itafanya mapitio
ya Sera ya Ufugaji Nyuki ya mwaka 1998 ili iendane na mabadiliko yanayotokea. Aidha,
mafunzo na vifaa kwa ajili ya ufugaji nyuki yatatolewa kwa lengo la kuongeza uzalishaji
wa Asali na Nta.
Maendeleo ya Viwanda Mheshimiwa
Spika, mchango wa Sekta ya Viwanda kwenye Pato la Taifa uliongezeka na kufikia Asilimia
9.7 mwaka 2012 ikilinganishwa na Asilimia 9.0 mwaka 2011. Viwanda vinavyoendelea vizuri
katika uzalishaji na kutoa mchango mkubwa ni pamoja na viwanda vya saruji, bia,
unga wa ngano, vinywaji baridi, sukari, rangi, nyaya za umeme na usindikaji wa
ngozi. Kwa upande wa SIDO, jumla ya Wajasiriamali 4,766 wamepatiwa mafunzo mbalimbali
ya kukuza ujuzi wao hususan katika usindikaji wa mafuta ya kupikia, ngozi,
ubanguaji wa korosho pamoja na kuhifadhi na kusindika vyakula vya aina mbalimbali.
Aidha,
SIDO ilitoa huduma za ugani kwa Wajasiriamali 6,779 ili kuboresha
shughuli za uzalishaji. Katika mwaka 2013/2014, Serikali itaendelea kubuni mikakati
mipya yenye lengo la kuendeleza na kuviwezesha viwanda vidogo na vya kati vya wajasiriamali
wa ndani pamoja na kuweka mazingira wezeshi ya ukuaji wa viwanda Nchini.
Mheshimiwa Spika, ili kuhamasisha Usindikaji wa Ngozi hapa Nchini na kuongeza
thamani ya zao la ngozi, mwezi Julai 2012, Serikali iliongeza Ushuru wa Ngozi Ghafi
zinazouzwa nje ya Nchi kutoka Asilimia 40 hadi 90 kwa kilo. Kutokana na hatua hiyo,
ngozi zinazosindikwa Nchini zimeongezeka kutoka vipande vya ngozi za Ng’ombe 166,773
na vipande vya ngozi za Mbuzi na Kondoo 778,023 kipindi cha Januari - Juni, 2012 hadi
vipande vya ngozi za Ng’ombe 343,860 na vipande vya ngozi za Mbuzi na Kondoo 1,173,875
kipindi cha Julai - Desemba, 2012. Ongezeko hilo linathibitisha kwamba hatua zilizochukuliwa
na Serikali zimeongeza usindikaji wa ngozi na kupanua wigo wa uzalishaji wa mazao
ya ngozi Nchini. Serikali itaendelea kusimamia mafanikio hayo na kuchukua hatua zaidi
zitakazoongeza usindikaji wa ngozi hapa Nchini.
Sekta ya Utalii Mheshimiwa Spika, Serikali imeandaa Mpango Mkakati wa kuifanya Mikoa ya
Dar es Salaam, Lindi, Mtwara na Tanga kuwa vituo vya utalii wa fukwe. Mikoa hiyo ina
fukwe za kipekee zinazovutia watalii na pia zinafaa kwa uwekezaji wa kitalii. Vilevile,
Serikali imevitangaza vivutio vya utalii katika soko la ndani na nje ya nchi kupitia
Vyombo vya Habari na maonesho ya ndani na Kimataifa. Kutokana na hatua hiyo, idadi
ya Watalii walioingia nchini mwaka 2012 imeongezeka na kufikia watalii 930,753 ikilinganishwa
na watalii 867,994 mwaka 2011. Aidha, mapato yatokanayo na utalii yameongezeka kutoka
Shilingi Bilioni 2,119 mwaka 2011 hadi Shilingi Bilioni 2,183 mwaka 2012.
Mheshimiwa Spika, matunda ya juhudi za kutangaza vivutio vya utalii
na pia kuhamasisha utalii wa ndani yamedhihirika baada ya Taasisi ya The Seven Natural
Wonders yenye Makao yake Nchini Marekani kuijumuisha Tanzania katika zoezi la kutafuta
Maajabu Saba ya Asili katika Bara la Afrika. Zoezi hilo lilishirikisha wataalam wengi
Duniani na kupigiwa kura na watu kutoka sehemu mbalimbali, wakiwemo Watanzania kwa
kutumia Tovuti. Matokeo ya zoezi hilo yalitangazwa tarehe 11 Februari 2013, Jijini
Arusha, ambapo Tanzania iliibuka mshindi kwa vivutio vitatu vya Maajabu Saba
ya Asili ya Afrika yakijumuisha Mlima Kilimanjaro, Ngorongoro Crater na Hifadhi ya
Taifa ya Serengeti. Napenda kutumia fursa hii kuwashukuru Watanzania wote wa ndani
na nje ya Nchi walioshiriki kupiga kura na hatimaye kutuwezesha kupata ushindi huo.
Aidha, namshukuru Dkt. Philip Imler ambaye ni mwanzilishi wa Taasisi ya The Seven
Natural Wonders aliyesimamia zoezi hilo. Pia, nayashukuru Makampuni yote yaliyofadhili
mashindano hayo na kutangaza vivutio vya Tanzania Barani Afrika na Duniani kote. Natoa
wito kwa Watanzania wote kuhakikisha kwamba tunavilinda, tunavitunza na kuviendeleza
vivutio hivyo kwa manufaa ya Taifa letu. Tutumie pia ushindi huo kutangaza zaidi utalii
wetu ili rasilimali hizi nzuri tulizo nazo ziendelee kuvutia watalii wengi na kuongeza
mapato yetu.
Sekta ya Madini
Mheshimiwa
Spika, wachimbaji wadogo wa madini wana mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa Nchi
yetu. Ili kuwaendeleza wachimbaji hao, Serikali imekamilisha Mkakati, Mpango Kazi
na Programu ya Mafunzo pamoja na kuwatengea maeneo wachimbaji wadogo kwa mujibu
wa Sheria. Maeneo hayo ni Mpambaa (Singida), Kilindi (Tanga), Dete na Melela (Morogoro),
Winza (Dodoma), Songwe (Mbeya), Nyakunguru (Mara), Nyamilonge na Ilagala (Kigoma),
Mihama (Katavi), Mwajanga (Manyara), Makanya (Kilimanjaro) na Mbesa (Ruvuma). Aidha,
Serikali imekusanya takwimu na taarifa muhimu za wachimbaji wadogo kote Nchini kwa
lengo la kuwatambua, kufahamu changamoto walizonazo na kujenga kanzidata (database).
Mheshimiwa Spika, Tanzania imekuwa Mwanachama kamili
wa Mpango wa Kimataifa Unaohimiza Uwazi katika Sekta ya Madini (Extractive Industries
Transparency Initiatives- EITI) baada ya kutimiza vigezo vilivyowekwa kimataifa katika
Sekta ya Madini. Hatua hiyo imeiwezesha Tanzania kuwa na mfumo thabiti wa utoaji taarifa
za malipo na mapato kutoka katika kampuni zinazojishughulisha na uchimbaji wa Madini,
Gesi Asilia na Mafuta ambao unamwezesha mwananchi kufahamu na kujadili mchango wa
Kampuni hizo katika Pato la Taifa. Katika mwaka 2013/2014, Serikali itaimarisha ukaguzi
kwenye uzalishaji na biashara ya madini pamoja na kuimarisha STAMICO ili itekeleze
majukumu yake kikamilifu.
HALI YA AJIRA NCHINI Mheshimiwa
Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kuongeza fursa za ajira kwa vijana wengi wanaoingia
kwenye soko la ajira kila mwaka. Kwa mujibu wa matokeo ya Utafiti wa Ajira na Kipato
Nchini wa mwaka 2010/2011, Ajira ziliongezeka kutoka 1,276,982 mwaka 2010 hadi Ajira
1,362,559 mwaka 2011, sawa na ongezeko la Asilimia 6.7. Ili kuongeza kasi ya ukuaji
wa ajira, Serikali inakamilisha Programu ya Kitaifa ya Kukuza Ajira kwa Vijana. Programu
hiyo ya miaka mitatu itaongeza fursa za Vijana 301,100 kuweza kujiajiri au kuajiriwa.
Msukumo zaidi utawekwa katika Miradi ya Kilimo, Viwanda Vidogo, Maeneo Maalum ya Kiuchumi
(EPZ na SEZ), Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano. Sambamba na hatua hiyo, Serikali itaendelea
kutoa mafunzo ya ujasiriamali kwa wanafunzi wa Vyuo vya Ufundi na vya Elimu ya Juu
ili kuwawezesha kujiajiri baada ya kuhitimu mafunzo yao.
HUDUMA ZA KIUCHUMI
Ardhi Mheshimiwa Spika, pamoja na Nchi yetu kuwa na ardhi ya kutosha na inayofaa
kwa Kilimo na uwekezaji mwingine, bado hatujakamilisha zoezi la uwekaji mipaka, kupima
na kutoa Hati kwa matumizi mbalimbali. Hali hiyo inachangia migogoro ya ardhi na kukwamisha
uwekezaji kwa kiasi kikubwa. Serikali imechukua hatua muhimu kwa kutumia teknolojia
ya kisasa itakayoharakisha zoezi la upimaji ardhi. Katika kutekeleza kazi hiyo, Awamu
ya Kwanza ya usimikaji wa Mtandao wa Alama za Msingi za Upimaji Ardhi Nchini (Geodetic
Control Network) imekamilika. Mikoa iliyohusika ni Pwani, Morogoro, Mara, Mwanza,
Kagera, Shinyanga, Lindi, Tabora na Dodoma. Tayari majaribio ya matumizi ya Alama
hizo yamefanyika katika Wilaya za Ngorongoro na Kilombero na kudhihirisha kuwa gharama
na muda wa kupima ardhi zimepungua. Awamu ya Pili ya usimikaji wa Alama hizo utaendelea
katika Mikoa iliyobaki na kuanza upimaji wa viwanja na mashamba kwa kutumia utaratibu
mpya wa upimaji wa ardhi.
Mheshimiwa Spika, ili
kuwa na mfumo endelevu wa utunzaji wa kumbukumbu za ardhi, Serikali imeanza ujenzi
wa Mfumo Unganishi wa Kuhifadhi Kumbukumbu za Ardhi. Mfumo huo utakaounganisha Ofisi
za Ardhi Nchini unategemewa kukamilika mwaka 2014 na utaiwezesha Tanzania kuwa na
kumbukumbu sahihi za ardhi. Vilevile, utaharakisha na kurahisisha utoaji wa maamuzi,
upimaji na utoaji wa Hati Miliki na hivyo kupunguza migogoro ya ardhi. Katika mwaka
2013/2014, Serikali itaendelea na ujenzi wa Mfumo Unganishi wa Kuhifadhi Kumbukumbu
za ardhi na kurahisisha upatikanaji wa ardhi kwa ajili ya uwekezaji.
Nishati Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kusogeza huduma ya nishati ya umeme
karibu na Wananchi ili kuharakisha maendeleo yao. Katika kutekeleza azma hiyo,
gharama za kuunganisha umeme wa njia moja kwa wateja wadogo Vijijini na
Mijini zimepunguzwa kwa wastani wa kati ya Shilingi Milioni 1,311,000 na Shilingi
114,000. Hatua hiyo imewezesha wananchi wengi kumudu gharama ya kuunganisha umeme
na kuongeza kasi ya usambazaji umeme Nchini. Serikali pia, imefikisha umeme katika
Makao Makuu ya Wilaya za Nkasi na Namtumbo, hivyo kufanya idadi ya Makao Makuu ya
Wilaya zenye umeme kuwa 117, sawa na Asilimia 88 ya Wilaya zote Nchini. Vilevile,
Serikali inatekeleza Programu Kabambe ya Kusambaza Umeme Vijijini ambapo wateja 8,046
wamelipiwa gharama za kuunganishiwa umeme kupitia Mfuko wa Nishati Vijijini. Aidha,
kazi ya kusambaza na kuboresha miundombinu ya umeme katika Mikoa ya Mtwara na Lindi
inaendelea kufanyika.
Mheshimiwa Spika, Sekta ndogo
ya Gesi Asilia inakua kwa kasi ambapo hadi kufikia Januari 2013, kiasi cha futi za
ujazo Trilioni 35 zimegundulika Nchini. Ili kusimamia rasilimali hiyo muhimu, Serikali
imeandaa rasimu ya Sera ya Gesi Asilia na kupata maoni kutoka kwa wadau mbalimbali.
Aidha, tarehe 8 Novemba 2012, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania alizindua mradi wa ujenzi wa miundombinu ya Gesi Asilia kutoka
Mtwara hadi Dar es Salaam. Mradi huo utaongeza uzalishaji wa umeme na kupunguza gharama
za umeme Nchini.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014,
Serikali itaendelea na ujenzi wa Mradi wa bomba la Gesi Asilia kutoka Mtwara hadi
Dar es Salaam na ujenzi wa Mitambo ya kuzalisha umeme wa Kinyerezi (MW 200). Vilevile,
itaanza kutekeleza Awamu ya Pili ya Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini na kufikisha
umeme wa gridi kwenye Makao Makuu ya Wilaya zisizokuwa na umeme.
Teknolojia
ya Habari na Mawasiliano Mheshimiwa Spika, Serikali inatekeleza
Mradi wa ujenzi wa Mkongo wa Mawasiliano wa Taifa wenye Awamu Tano. Awamu ya Kwanza
na ya Pili ya Ujenzi wa Mkongo huo wenye urefu wa Kilomita 7,560 imekamilika na kuunganisha
Makao Makuu ya Mikoa 24 ya Tanzania Bara. Kazi ya kuunganisha Kisiwa
cha Unguja na Mkongo huo kupitia Dar es Salaam itakamilika mwaka 2013. Tayari Makampuni
ya Simu na Mawasiliano ya hapa Nchini yameunganishwa kwenye Mkongo hatua ambayo imewezesha
upatikanaji wa huduma bora za mawasiliano katika eneo kubwa zaidi na kwa gharama nafuu.
Sambamba na hatua hiyo, Serikali imeanza ujenzi wa Mfumo wa Kuratibu Huduma za Mawasiliano
Nchini (Traffic Monitoring System). Mfumo huo utasaidia kuhakikisha mapato yanayotokana
na huduma katika Sekta ya Mawasiliano yanajulikana ili Makampuni ya Mawasiliano Nchini
yalipe kodi stahiki kwa Serikali.
Mheshimiwa Spika,
Tanzania pamoja na Nchi zote Duniani kupitia Umoja wa Mawasiliano Duniani (ITU) zimekubaliana
kusitisha matumizi ya teknolojia ya utangazaji kutoka Mfumo wa Analojia na kuanza
Matumizi ya Teknolojia ya Dijitali ifikapo Juni 2015. Hapa Nchini, usitishaji wa
matumizi ya mfumo wa mitambo ya analojia umeanza kutekelezwa tarehe 31 Desemba 2012
kwa awamu kwa kuanzia na Jiji la Dar es Salaam na kufuatiwa na Mikoa ya Dodoma,
Tanga na Mwanza. Matangazo ya analojia yataendelea kusitishwa katika Mikoa mingine
Nchini kulingana na ratiba iliyowekwa. Natambua kwamba kuna changamoto zilizojitokeza
katika utekelezaji wa zoezi hilo la mabadiliko. Hata hivyo, mabadiliko hayo yanalenga
kuimarisha mawasiliano na kuiwezesha Nchi yetu kuendana na hali halisi ya mabadiliko
ya teknolojia Duniani. Katika mazingira ya sasa, sisi kama Taifa siyo vyema kubaki
kama kisiwa wakati tumeunganishwa na mifumo ya teknolojia ya kidunia.
Hivyo,
ni busara tuendelee na mabadiliko hayo sasa kuliko kusubiri na hatimaye tukajikuta
tuko nyuma na nje ya mstari. Natoa wito kwa Watanzania wote kuyaona mabadiliko hayo
kwa mtazamo chanya na kuyakubali kama hatua kubwa sana ya maendeleo ya teknolojia
Nchini.
Sayansi na Teknolojia Mheshimiwa Spika, Serikali
inafanya jitihada kubwa za kuendeleza Sayansi na Teknolojia kama njia ya kuongeza
kasi ya ukuaji wa uchumi. Jitihada hizo ni pamoja na kutenga fedha za kutosha kila
mwaka kwa ajili ya utafiti na maendeleo ya kisayansi. Serikali pia, imekamilisha ujenzi
wa Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela iliyopo Mkoani Arusha ambayo
ilizinduliwa rasmi tarehe 2 Novemba 2012. Kukamilika kwa ujenzi wa Taasisi hiyo kumeongeza
udahili wa wanafunzi wa Shahada ya Uzamili na Uzamivu kutoka wanafunzi 83 mwaka 2011/2012
hadi wanafunzi 135 mwaka 2012/2013.
Mheshimiwa Spika,
katika mwaka 2013/2014, Serikali itaendelea kueneza Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano
na kupanua matumizi yake katika maeneo mbalimbali Nchini na Nchi jirani. Vilevile,
Serikali itaendelea na zoezi la kuhama kutoka katika mfumo wa analojia kwenda dijitali
na kupanua na kuboresha Mtandao wa Huduma za Mawasiliano ya simu na intaneti Nchini.
Barabara
na Madaraja Mheshimiwa Spika, Serikali imewekeza kwa kiwango kikubwa
katika kujenga, kukarabati na kuboresha mtandao wa Barabara Kuu, za Mikoa, Wilaya
pamoja na za Vijijini ili zipitike wakati wote wa mwaka. Lengo ni kuwa na mtandao
bora wa barabara utakaowezesha Wananchi, hasa Wakulima kusafirisha mazao yao hadi
kwenye Masoko ya ndani na nje ya Nchi. Katika mwaka 2012/2013, Serikali imejenga
jumla ya Kilometa 294.4 za kiwango cha lami katika Barabara Kuu na za Mikoa
na kukarabati kwa kiwango cha lami jumla ya Kilometa 111.8 katika barabara
hizo. Aidha, kazi za ujenzi na ukarabati wa Barabara Kuu na za Mikoa zenye urefu wa
Kilometa 179 kwa kiwango cha lami unaendelea katika maeneo mbalimbali Nchini.
Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Nne imedhamiria kujenga na kukamilisha
ujenzi wa Madaraja makubwa na ya kisasa mawili ambayo ni Daraja la Mto Malagarasi
na Daraja la Kigamboni. Ujenzi wa Daraja la Mto Malagarasi unaojumuisha ujenzi
wa Daraja kubwa lenye urefu wa Meta 200 na Madaraja mengine madogo katika Bonde la
Mto Malagarasi unaendelea vizuri. Hadi mwezi Machi 2013, Mkandarasi amekamilisha
ujenzi kwa Asilimia 85. Sambamba na hatua hiyo, taratibu zimekamilika za kupata mkopo
wa nyongeza kutoka Mfuko wa Ushirikiano wa Maendeleo ya Kiuchumi wa Korea kwa ajili
ya ujenzi wa barabara kiungo za Daraja hilo zenye urefu wa Kilometa 37 kwa kiwango
cha lami.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Daraja
la Kigamboni lenye urefu wa Meta 680 linalojengwa kuunganisha eneo la Kurasini na
Kigamboni katika Bahari ya Hindi, tayari Mkandarasi amekamilisha kazi za maandalizi
kwa Asilimia 90. Kazi ya ujenzi wa Daraja la Kudumu na Barabara zake inatarajiwa kuanza
wakati wowote kuanzia sasa. Daraja hili linajengwa kwa Ubia kati ya Serikali
na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF). Lengo ni kukamilisha ujenzi wa Daraja hilo mwanzoni
mwa mwaka 2015.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014
Serikali itajenga Barabara Kuu kwa kiwango cha lami zenye urefu wa Kilometa 495 na
kukarabati Barabara zenye urefu wa Kilometa 190 na Madaraja 11. Serikali pia, itajenga
barabara za Mikoa za lami zenye urefu wa Kilometa 54.3 na kukarabati Kilometa 855
kwa kiwango cha changarawe na Madaraja 36. Aidha, matengenezo ya kawaida na matengenezo
ya muda maalum ya Barabara Kuu na za Mikoa yataendelea kufanyika katika kipindi kijacho.
Usafiri
wa Barabara katika Jiji la Dar es Salaam Mheshimiwa Spika, msongamano
wa magari katika barabara za Jiji la Dar es Salaam ni moja ya changamoto ambayo Serikali
inaendelea kuifanyia kazi. Jitihada zinazofanyika kupunguza msongamano wa magari barabarani
ni pamoja na kujenga miundombinu zaidi ya barabara mpya za kuingia na kutoka katikati
ya Jiji; kuanzisha usafiri wa Treni ya Abiria; kuharakisha utekelezaji wa Mradi wa
Mabasi Yaendayo Haraka (DART); na kuimarisha usimamizi wa Sheria za Usalama Barabarani.
Mheshimiwa Spika, kuhusu ujenzi wa barabara mpya za
kupunguza msongamano katika Jiji la Dar es Salaam, hadi Machi, 2013 ujenzi wa Barabara
ya kiwango cha lami yenye urefu wa Kilometa 6.4 kutoka Kituo Kikuu cha Mabasi Ubungo
- Kigogo hadi mzunguko wa barabara ya Kawawa imekamilika na barabara yenye urefu wa
Kilometa 2.7 kutoka barabara ya Kawawa – Bonde la Msimbazi hadi Makutano ya Jangwani
na Twiga imekamilika kwa Asilimia 70. Aidha, ujenzi wa Barabara yenye urefu wa Kilometa
10.3 kutoka Jet Corner - Vituka hadi Davis Corner imekamilika kwa Asilimia 90. Vilevile,
utekelezaji wa Awamu ya Kwanza ya Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka unaendelea ambapo
kazi zilizofanyika ni pamoja na ujenzi wa barabara za DART na za magari mchanganyiko
na baiskeli katika Barabara ya Morogoro, na ujenzi wa Miundombinu ya Mifumo ya Maji,
Vituo vya Mabasi na Madaraja. Katika mwaka 2013/2014, Serikali itaendelea na ujenzi
wa barabara nyingine za kupunguza msongamano katika Jiji la Dar es Salaam pamoja na
ujenzi wa miundombinu ya DART.
HALI YA UCHUKUZI
Huduma za Usafiri
wa Reli Jijini Dar es Salaam Mheshimiwa Spika, mwezi Oktoba 2012,
Serikali ilianzisha huduma ya usafiri wa treni ya abiria Jijini Dar es Salaam kupitia
Kampuni ya Reli (TRL) na TAZARA kwa lengo la kukabiliana na tatizo la msongamano wa
magari na abiria. Wastani wa idadi ya Abiria wanaosafiri kwa Treni ya TAZARA ni 4,500
kwa siku na TRL ni Abiria 5,000. Takwimu zinaonesha kuwa, Abiria 9,500 wanaosafiri
kila siku kwa njia ya treni wangehitaji kutumia mabasi zaidi ya 380 yenye uwezo wa
kubeba Abiria 25 kila moja. Kwa ujumla mwitikio wa wananchi wa kutumia huduma ya
treni ya abiria ni mkubwa ikilinganishwa na uwezo wa kutoa huduma hiyo. Kwa kuzingatia
mahitaji hayo makubwa, Serikali imeunda Kamati maalum ya wadau wa usafiri Jijini Dar
es Salaam kwa lengo la kuchambua, kuanisha na kushauri mipango na mikakati ya baadaye
ya kuboresha huduma hiyo ili iwe endelevu na salama. Ni mategemeo yangu kwamba Kamati
hiyo itaandaa Mpango mzuri zaidi wa kupanua huduma hiyo muhimu kwa Jiji la Dar es
Salaam ambalo kwa mujibu wa Takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 lina
idadi ya watu Milioni 4.36, sawa na Asilimia 10 ya Wakazi wote wa Tanzania Bara. Ongezeko
hilo ni kubwa na hivyo linahitaji Mpango Kabambe wa usafiri na usafirishaji.
Usafiri wa Reli ya Kati na TAZARA Mheshimiwa Spika, katika
mwaka 2012/2013, Serikali imeendelea kuboresha miundombinu ya reli ya kati kwa kujenga
na kukarabati maeneo mbalimbali ili kuiwezesha kupitika wakati wote. Pamoja na ukarabati
huo, usanifu wa kina wa Mradi wa Uendelezaji na Ujenzi wa Reli kutoka Dar es Salaam
- Isaka - Keza - Kigali na Keza - Musongati kwa kiwango cha Kimataifa umekamilika
mwezi Februari 2013. Serikali pia, imekamilisha mchakato wa kumpata Mshauri mwelekezi
atakayefanya upembuzi yakinifu wa kuinua kiwango cha reli kuwa katika kiwango cha
kimataifa kutoka Tabora hadi Kigoma, Kaliua hadi Mpanda na Isaka hadi Mwanza. Lengo
ni kuwezesha reli hiyo ifanane na inayotarajiwa kujengwa kutoka Dar es Salaam-Isaka-Kigali/Musongati.
Upembuzi Yakinifu wa reli ya kutoka Dar es Salaam hadi Rwanda na Burundi na kutoka
Arusha hadi Musoma unatarajiwa kuanza mwaka 2013/2014.
Mheshimiwa
Spika, itakumbukwa kwamba mwezi Machi 2012, Serikali ya Tanzania na Serikali ya Jamhuri
ya Watu wa China zilitia saini Itifaki ya 15 ya kuboresha Reli ya TAZARA.
Tayari
Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China imetoa jumla ya Shilingi Bilioni 38.2 kwa ajili
ya kutekeleza miradi iliyo chini ya Itifaki hiyo ambayo inajumuisha kufanya upembuzi
yakinifu wa kuboresha reli hiyo, kukarabati njia ya reli, kununua vichwa vipya vya
treni na kukarabati mabehewa ya abiria. Hatua hizi zikikamilika zitaboresha kwa kiwango
kikubwa usafiri wa Reli ya TAZARA.
Bandari Mheshimiwa Spika,
Serikali inachukua hatua mbalimbali za kuongeza uwezo na ufanisi wa bandari zake kwa
kutekeleza Mpango Kabambe wa Mamlaka ya Bandari. Baadhi ya Miradi inayotekelezwa chini
ya Mpango huo ni Upembuzi Yakinifu kwa ajili ya kuimarisha na kuongeza kina cha maji
katika Gati Namba 1 hadi 7 katika Bandari ya Dar es Salaam na kuanza awamu ya pili
ya mradi wa ujenzi wa matanki ya kuhifadhia mafuta. Mradi mwingine ni kufanya Upembuzi
Yakinifu wa ujenzi wa kituo kikubwa cha kuhifadhia mizigo ya kwenda Nchi jirani katika
eneo la Kisarawe.
Mheshimiwa Spika, kutokana na nafasi
ya Nchi yetu kijiografia na ongezeko kubwa la biashara na uingizaji wa mizigo ya hapa
Nchini na Nchi jirani ambazo hazina bandari, uwezo wa Bandari ya Dar es Salaam kuhimili
ongezeko hilo unapungua. Pamoja na jitihada zinazoendelea za kupanua miundombinu ya
bandari hiyo, Serikali imeona umuhimu wa kuwa na Bandari mpya ya Bagamoyo ili isaidiane
na Bandari zilizopo kukabiliana na ongezeko hilo. Tarehe 24 Machi 2013, Serikali ya
Tanzania na China zimetia saini makubaliano ya kujenga Bandari mpya ya Bagamoyo ambayo
itakuwa kubwa kuliko zote katika Ukanda wa Nchi za Afrika Mashariki na Kati. Makubaliano
hayo yanajumuisha pia ujenzi wa eneo huru la biashara na miundombinu mingine muhimu
ikiwemo reli itakayounganisha Bandari ya Bagamoyo na Reli ya Kati na ya TAZARA pamoja
na barabara ya lami kutoka Bagamoyo hadi Mlandizi. Huu ni mradi mkubwa na wa kimkakati
ambao utabadili kabisa mfumo wa uendeshaji wa Bandari na usafirishaji Nchini.
Usafiri
wa Anga Mheshimiwa Spika, Serikali imetekeleza kwa mafanikio Awamu
ya Kwanza ya Uboreshaji na Upanuzi wa Viwanja vya Ndege vya Tabora, Kigoma na Bukoba.
Ujenzi wa barabara ya kuruka na kutua ndege kwa kiwango cha lami katika kiwanja cha
Ndege cha Tabora umekamilika na kazi za ujenzi zinazoendelea katika kiwanja cha Kigoma
zinatarajiwa kumalizika mwezi Juni 2013. Kwa upande wa Kiwanja cha Ndege cha Bukoba,
ukarabati wa njia ya kuruka na kutua ndege kwa kiwango cha lami unaendelea. Aidha,
Kiwanja kipya cha Kimataifa cha Songwe, Mbeya kilianza kutoa huduma tarehe 13 Desemba,
2012. Kiwanja hicho ambacho kijiografia kipo karibu na Nchi za Zambia, Malawi, Jamhuri
ya Kidemokrasia ya Kongo na Nchi nyingine za Kusini mwa Afrika ni kichocheo muhimu
cha shughuli za uchumi na kijamii zikiwemo utalii na kilimo hasa cha matunda, mbogamboga
na maua kwa Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini. Ni muhimu sana wananchi wa maeneo hayo
na mengine wahamasishwe na kujipanga kutumia fursa za kiuchumi zitakazoambatana na
kukamilika kwa kiwanja hicho.
Mheshimiwa Spika, katika
mwaka 2013/2014, Serikali itaendelea na utekelezaji wa Mradi wa Upanuzi na Uboreshaji
wa Viwanja vya Ndege. Kazi zitakazofanyika ni pamoja na Upembuzi Yakinifu na usanifu
wa kina wa ukarabati kwa kiwango cha lami wa njia za kuruka na kutua ndege kwa viwanja
vya Iringa, Kilwa Masoko, Ziwa Manyara, Musoma, Mtwara, Njombe, Songea, Singida na
Tanga.
MAENDELEO YA SEKTA YA ELIMU
Elimu ya Msingi Mheshimiwa
Spika, Serikali ilianza kutekeleza Programu kubwa za kuendeleza elimu Nchini mwaka
2001 kwa lengo la kuongeza idadi ya Wanafunzi wa rika lengwa wanaojiunga na shule
na kuboresha elimu. Utekelezaji wa Awamu ya Kwanza na ya Pili ya Mpango wa Maendeleo
ya Elimu ya Msingi (MMEM I & II) umeleta mafanikio makubwa katika kuboresha miundombinu
ya elimu, kuandikisha Wanafunzi wa rika lengwa na kupunguza pengo la uandikishaji
kati ya Wanafunzi wa Kike na wa Kiume. Mafanikio hayo yaliambatana na changamoto
za upungufu wa Walimu, Vifaa vya kujifunzia na kufundishia pamoja na madawati.
Kwa kutambua changamoto hizo, Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010 inaelekeza
Serikali kulinda mafanikio yaliyopatikana pamoja na kuweka msisitizo mkubwa katika
ubora wa elimu.
Mheshimiwa Spika, ili kuendeleza
kasi tuliyoanza nayo, Serikali inatekeleza Awamu ya Tatu ya Mpango wa Maendeleo ya
Elimu ya Msingi (MMEM III) unaolenga kuboresha elimu kwa kuongeza idadi ya Walimu,
vitabu vya ziada na kiada na vifaa vya kujifunzia na kufundishia. Jitihada za Serikali
za kuajiri walimu zinaendelea ambapo Walimu wapya 13,568 wameajiriwa katika Shule
za Msingi mwaka 2012/2013. Serikali itaendelea kuweka msisitizo katika kuboresha Elimu
ya Msingi Nchini kwa kuzingatia manufaa makubwa yanayopatikana katika ngazi hiyo muhimu
ya elimu.
Elimu ya Sekondari Mheshimiwa Spika, mafanikio
ya utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi Nchini ambayo ni pamoja na
kuongezeka kwa idadi ya wahitimu wanaofaulu ngazi hiyo, yameongeza mahitaji ya
nafasi zaidi katika Shule za Sekondari. Kutokana na hali hiyo, Serikali ilianza kutekeleza
Mpango wa Maendeleo wa Elimu ya Sekondari (MMES) mwaka 2006. Mpango huo umesaidia
sana kukabiliana na changamoto ya nafasi zaidi katika Shule za Sekondari kwa kujenga
Shule nyingi za Sekondari na hivyo kuwa na wanafunzi wengi zaidi. Ni dhahiri kuwa
ongezeko hilo la Wanafunzi lilihitaji Walimu wengi zaidi, Maabara, Vitabu
na Vifaa vingine muhimu. Aidha, Serikali iligatua usimamizi wa Shule za Sekondari
kutoka Serikali Kuu kwenda katika Mamlaka za Serikali za Mitaa ili kuboresha usimamizi
wa shule hizo pamoja na kuanzisha programu kabambe ya kufundisha walimu zaidi ili
wafundishe katika shule zinazoongezeka. Katika mwaka 2012/2013, Serikali imeajiri
jumla ya Walimu 12,969 ambao watafundisha katika Shule mbalimbali za Sekondari Nchini.
Hatua hizo zote ni uwekezaji mkubwa ambao matokeo yake yatawezesha kuboresha elimu
Nchini hatua kwa hatua.
Mheshimiwa Spika, sote tumehuzunishwa
sana na matokeo yasiyoridhisha ya mtihani wa Kidato cha Nne kwa mwaka 2012. Matokeo
hayo siyo tu kwamba yamewahuzunisha wazazi ambao wamewekeza rasilimali kwa Watoto
wao bali pia Serikali ambayo imetumia rasilimali nyingi kwenye Sekta ya Elimu. Huu
siyo wakati wa kulaumiana ama kutafuta mchawi wa matokeo hayo yasiyoridhisha. Ni lazima
tutafute suluhisho, kusonga mbele na kubuni mikakati na hatua za haraka za kusaidia
Watoto hao ambao wamepata matokeo mabaya. Tumeanza kwa kuunda Tume yenye Watu makini
ambayo itachunguza chanzo cha matokeo hayo mabaya na kutoa mapendekezo ya namna ya
kutatua tatizo hilo katika muda mfupi, kati na mrefu na pia kupendekeza suluhisho
la haraka kwa wale waliopata daraja la IV na sifuri. Napenda niwahakikishie Waheshimiwa
Wabunge na Watanzania wote kwamba, matokeo ya Tume hiyo yatawekwa bayana na hatua
zitakazopendekezwa zenye lengo la kuimarisha elimu Nchini zitachukuliwa. Hata hivyo,
ni vyema tukumbuke kwamba, sote tuna wajibu wa kutoa mwongozo na mapendekezo yatakayosaidia
kutoka hapa tulipo. Wazazi, Wanafunzi na Jamii nzima wana nafasi yao pia katika kuboresha
elimu ya Nchi hii. Hili siyo suala la Serikali pekee.
Elimu Maalum Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kuweka msukumo wa kipekee katika
kutoa Elimu Maalum kwa watu wenye Ulemavu wakiwemo wenye Ulemavu wa Ngozi,
Uoni Hafifu na Usikivu. Katika mwaka 2012/2013, Serikali imeandaa Mwongozo wa kufundishia
Wanafunzi wenye Ulemavu wa Ngozi na Uoni Hafifu. Aidha, Serikali imenunua na kusambaza
vifaa maalum na visaidizi vya kufundishia na kujifunzia kuanzia ngazi ya Elimu ya
Awali hadi Chuo Kikuu. Kazi nyingine zilizofanyika ni kukarabati na kujenga majengo
rafiki kwa walemavu katika Chuo cha Ualimu Patandi. Katika mwaka 2013/2014, Serikali
itaendelea kuboresha utoaji wa Elimu Maalum hususan baada ya kupata takwimu sahihi
za walemavu kutokana na Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012.
Elimu ya
Juu Mheshimiwa Spika, Serikali inatekeleza Mpango wa Maendeleo wa
Elimu ya Juu kwa kupanua na kuongeza Taasisi za Elimu ya Juu za Serikali na Binafsi.
Katika kipindi takribani cha miaka 8 idadi ya wanafunzi wanaosoma Vyuo vya Elimu ya
Juu Nchini imeongezeka kutoka 40,993 mwaka 2005/2006 hadi 166,484 mwaka 2012/2013,
sawa na ongezeko la Asilimia 306. Serikali pia, inatoa mikopo kwa wanafunzi wa Vyuo
vya Elimu ya Juu vya Umma na vile vya Mashirika ya Dini na vya Sekta Binafsi. Katika
mwaka 2012/2013, Serikali imetoa mikopo ya Shilingi Bilioni 345 kwa wanafunzi 98,772
ikilinganishwa na mikopo ya Shilingi Bilioni 291 kwa wanafunzi 93,784 mwaka 2011/2012.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Serikali
itaendelea kuongeza kiasi cha fedha kwa ajili ya Mikopo ya Elimu ya Juu na kuimarisha
usimamizi wa urejeshaji wa mikopo ili wanafunzi wengi zaidi waweze kunufaika. Nitumie
fursa hii kuwakumbusha wale wote walionufaika na mikopo ya elimu ya juu kulipa mikopo
hiyo yenye masharti nafuu sana ili wanafunzi zaidi waweze kunufaika nayo. Aidha,
waajiri watimize wajibu wao kwa kuwataka waajiriwa walionufaika kulipa mikopo hiyo.
Vilevile, Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu iongeze kasi ya kukusanya madeni na kuchukua
hatua stahiki kwa wale wasiolipa kwa mujibu wa Sheria.
MAENDELEO YA SEKTA
YA AFYA
Vituo vya Utoaji wa Huduma za Afya Nchini
Mheshimiwa
Spika, Serikali imeweka jitihada kubwa za kuhakikisha kwamba Vituo vya Utoaji wa Huduma
za Afya katika ngazi zote Nchini vinapatiwa dawa muhimu na vifaa vya Teknolojia ya
kisasa vya kuchunguza na kutibu magonjwa. Katika mwaka 2012/2013, Serikali imenunua
Dawa, Vifaa, Vifaa Tiba na vitendanishi na kuvisambaza kwenye Zahanati, Vituo vya
Afya na Hospitali zote za Serikali Nchini. Serikali pia, imeongeza uwezo wa ndani
wa kutibu maradhi mbalimbali. Mathalan, Hospitali ya Taifa ya Muhimbili imewezeshwa
kutoa huduma za Afya za ubingwa wa juu ikiwa ni pamoja na upasuaji wa moyo ambapo
hadi sasa zaidi ya Wagonjwa 450 wamepatiwa huduma hiyo. Vilevile, huduma ya usafishaji
damu kwa Wagonjwa wa figo na Upasuaji kupitia tundu dogo pamoja na uchunguzi wa magonjwa
kwa kutumia mashine za kisasa unafanyika hapa Nchini. Hatua hiyo imewezesha Serikali
na Wananchi kuokoa fedha nyingi zinazotumika kupeleka wagonjwa kutibiwa nje ya Nchi.
Napenda kutumia fursa hii kuwapongeza Madaktari, Wauguzi na Wataalam wengine wa Afya
kwa kuliwezesha Taifa letu kupiga hatua kubwa katika kutibu magonjwa hayo na mengine
yanayohitaji utaalam na ubingwa wa hali ya juu.
Mheshimiwa
Spika, Serikali imeimarisha huduma ya tiba ya saratani Nchini kwa kukamilisha ujenzi
wa Jengo la kulaza wagonjwa katika Hospitali ya Saratani ya Ocean Road na hivyo kuongeza
uwezo wake kutoka vitanda 120 hadi 270. Aidha, Serikali imesogeza huduma ya tiba ya
saratani karibu na Wananchi kwa kukamilisha ujenzi wa Jengo Maalum la kutoa huduma
hiyo katika Hospitali ya Bugando. Hatua hiyo itapanua wigo wa kutoa huduma ya tiba
ya saratani na kupunguza msongamano wa Wagonjwa wa saratani kutoka Mikoa mbalimbali
waliokuwa wanalazimika kufuata huduma hiyo katika Hospitali ya Saratani ya Ocean Road
Jijini Dar es Salaam.
Udhibiti wa Maambukizi ya Malaria na UKIMWI Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012, Serikali ilifanya Utafiti kuhusu Viashiria
vya UKIMWI na Malaria. Taarifa ya matokeo ya utafiti huo inaonesha kuwa kiwango cha
Malaria Nchini kwa watoto walio na umri chini ya miaka mitano kimepungua kutoka Asilimia
18 mwaka 2007 hadi Asilimia Tisa mwaka 2012. Hali hii imechangiwa zaidi na ongezeko
kubwa la matumizi ya Vyandarua vilivyowekwa Viuatilifu vya muda mrefu ambapo zaidi
ya Vyandarua milioni 34 vimesambazwa katika Kaya zenye Watoto walio na umri chini
ya miaka mitano na Wanawake Wajawazito. Kutokana na usambazaji huo, matumizi ya Vyandarua
yameongezeka kutoka Asilimia 26 mwaka 2007 hadi Asilimia 72 mwaka 2012 kwa Watoto
wenye umri chini ya miaka Mitano. Kwa Wanawake Wajawazito, matumizi ya Vyandarua yameongezeka
kutoka Asilimia 27 mwaka 2007 hadi Asilimia 75 mwaka 2012. Ni dhahiri kupungua kwa
kiwango cha Malaria Nchini ni jitihada za kipekee za Serikali ya Awamu ya Nne kwa
kushirikiana na Wananchi na Washirika wa Maendeleo kupitia Kampeni mbalimbali za Kudhibiti
Malaria.
Mheshimiwa Spika, napenda kutumia fursa hii
kuwashukuru na kuwapongeza Wananchi na Wadau wote walioshirikiana na Serikali katika
kupata mafanikio haya ambayo yanatokana na utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Kudhibiti
Malaria Nchini na Mpango wa Hati Punguzo kwa Wanawake Wajawazito ulioanza kutekelezwa
mwaka 2008 hadi 2012. Natoa wito kwa Wananchi wote kuendeleza juhudi za Kujikinga
na Malaria, hususan kwa kutumia Vyandarua vyenye Viuatilifu vya muda mrefu na kutokomeza
Mazalia ya Mbu.
Mheshimiwa Spika, juhudi za Serikali
za kupambana na ugonjwa wa UKIMWI Nchini pia zimeanza kuzaa matunda. Kwa mujibu wa
Utafiti wa mwaka 2011 - 2012 wa Viashiria vya Malaria na UKIMWI, maambukizi ya Virusi
vya UKIMWI yamepungua kutoka Asilimia 5.7 mwaka 2007/2008 hadi Asilimia 5.1 mwaka
2011/2012 kwa wanawake na wanaume wa umri wa miaka 15 - 49. Ili kuendelea kupunguza
kasi ya maambukizi ya UKIMWI Nchini, Serikali inaendelea kutoa elimu ya UKIMWI;
kutoa ushauri nasaha na kuhamasisha upimaji wa hiari. Katika mwaka 2013/2014, Serikali
itaanza kutekeleza Mkakati Mpya wa Taifa wa Kudhibiti UKIMWI wa mwaka 2013 hadi 2017
unaolenga kuwa na Sifuri tatu, yaani Kutokuwa na Maambukizi Mapya; Kukomesha Vifo
Vitokanavyo na UKIMWI na Kuondoa Kabisa Unyanyapaa na Ubaguzi. Lengo hilo litatimia
iwapo sote tutabadili tabia zinazosababisha maambukizi mapya.
Lishe Mheshimiwa Spika, Serikali inachukua hatua thabiti za kupambana na utapiamlo
hususan udumavu unaoathiri watoto wenye umri chini ya miaka mitano. Katika hotuba
yangu ya mwaka 2012/2013 nilieleza kwamba Serikali imezindua Mkakati wa Kitaifa wa
Lishe wa mwaka 2010/2011 hadi 2014/2015. Mkakati huo umeanza kutekelezwa kwa kuandaliwa
Mpango wa Utekelezaji ulioainisha gharama na majukumu ya kila mdau katika kupunguza
Utapiamlo Nchini. Pamoja na mambo mengine, Mpango huo umesisitiza umuhimu wa kutoa
elimu kwa umma kuhusu lishe bora hasa kwa mama wajawazito na watoto wachanga, kuongeza
viini lishe kwenye vyakula pamoja na kuingiza masuala ya lishe kwenye Sera na Mipango
mbalimbali ya Serikali. Tayari hatua zimechukuliwa ambapo masuala ya lishe yameingizwa
kwenye Mpango wa Taifa wa Uwekezaji katika Kilimo na Chakula (Tanzania Agriculture
and Food Security Investment Plan - TAFSIP). Vilevile, Serikali inaendelea na zoezi
la kuhuisha Sera ya Usalama wa Chakula na Lishe ya mwaka 1992 ili iendane na Mkakati
wa Taifa wa Lishe wa mwaka 2010/2011 hadi 2014/2015.
Mheshimiwa
Spika, tunayo kazi kubwa mbele yetu ya kupambana na tatizo la lishe duni katika maeneo
yote Nchini. Takwimu zinabainisha kwamba, hakuna tofauti kubwa ya kiwango cha udumavu
katika Mikoa inayozalisha chakula kwa wingi na ile yenye uhaba wa chakula. Napenda
kusisitiza tena kwamba hali ya udumavu humtokea mtoto katika siku elfu moja za kwanza
za uhai wake, yaani tangu kutungwa mimba hadi umri wa miaka miwili. Hivyo, tunahitaji
kuimarisha utoaji elimu ya lishe kwa Wajawazito na Mama wanaonyonyesha ili wapate
mlo kamili na kunyonyesha watoto wao kikamilifu hususan miezi sita ya mwanzo tangu
kuzaliwa. Natoa wito kwa Waheshimiwa Wabunge zaidi kujiunga na Kikundi cha Wabunge
kinachohamasisha umuhimu wa Lishe Bora ili kuongeza kasi na chachu ya kutoa elimu
ya lishe katika maeneo yetu ya uwakilishi.
HALI YA UPATIKANAJI MAJI NCHINI
Huduma
ya Maji Vijijini Mheshimiwa Spika, upatikanaji wa maji ya uhakika
na ya kutosha kwa wananchi Vijijini bado ni changamoto inayohitaji nguvu zaidi na
mbinu mpya kwa kuzingatia ongezeko kubwa la watu pamoja na mabadiliko ya Tabianchi.
Katika kukabiliana na changamoto hizo, Serikali imetenga na kupima maeneo ya vyanzo
vya maji na kuyawekea mipaka ili kuzuia uchafuzi na uharibifu wa vyanzo hivyo. Aidha,
Vituo mbalimbali vya kuchotea maji vimeainishwa katika Halmashauri 122 na kuwekwa
kwenye ramani ili vifahamike. Ujenzi wa miradi mipya, upanuzi na ukarabati wa miundombinu
ya maji Vijijini pia umefanyika katika maeneo mbalimbali ili kusogeza huduma ya maji
karibu na wananchi. Kutokana na juhudi hizo, idadi ya Wananchi wanaoishi Vijijini
ambao wanapata huduma ya majisafi, salama na ya kutosha karibu na makazi imeongezeka
kutoka watu Milioni 16.3 mwaka 2006 hadi Milioni 20.6 mwaka 2012.
Huduma
ya Maji Mijini Mheshimiwa Spika, huduma ya Maji Mijini inasimamiwa
na kutekelezwa na Mamlaka 19 za Majisafi na Usafi wa Mazingira katika Miji Mikuu ya
Mikoa, Mamlaka 109 katika ngazi za Wilaya, Miji Midogo na Miradi ya Maji
ya Kitaifa. Serikali kupitia Mamlaka hizo imeongeza kiwango cha upatikanaji wa maji
kwa wakazi wa Miji hiyo kutoka Asilimia 84 mwaka 2010/2011 hadi Asilimia 86 mwaka
2011/2012. Katika Jiji la Dar es Salaam, Serikali inaboresha upatikanaji wa huduma
ya maji kwa kupanua uwezo wa mtambo wa maji wa Ruvu Chini ambapo ujenzi umefikia Asilimia
85. Kazi ya kulaza bomba kuu la pili lenye kipenyo cha Meta 1.8 na urefu
wa km 55.5, kutoka Ruvu Chini hadi kwenye matanki ya kuhifadhia maji yaliyopo eneo
la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam inatarajiwa kukamilika mwezi Februari 2014. Aidha,
kazi ya usanifu wa Mradi wa Kuchimba Visima Virefu 12 katika maeneo ya Kimbiji na
Visima 8 katika eneo la Mpera imekamilika na Wananchi waliohamishwa wamelipwa
fidia. Katika mwaka 2013/2014, Serikali itaendelea kukarabati na kujenga miradi ya
maji Mijini na Vijijini pamoja na kujenga mabwawa kwa ajili ya matumizi ya majumbani
na mifugo hususan katika maeneo kame.
TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA
MITAA
Uanzishaji wa Maeneo Mapya ya Utawala Mheshimiwa Spika,
Serikali imekamilisha taratibu za kuanzisha Halmashauri Mpya 31 ili kusogeza huduma
karibu na Wananchi. Halmashauri hizo ni Jiji la Arusha, Manispaa ya Ilemela, Manispaa
ya Lindi na Halmashauri za Miji ya Kahama, Masasi, Makambako, Geita na Bariadi. Vilevile,
imeanzisha Halmashauri za Wilaya ya Kalambo, Busega, Nsimbo, Bumbuli, Mlele, Ushetu,
Msalala, Momba, Mbogwe, Kyerwa, Busokelo na Buhigwe. Halmashauri nyingine zilizoanzishwa
ni Nyangh’wale, Wanging’ombe, Chemba, Mkalama, Gairo, Nyasa, Kakonko, Itilima, Uvinza,
Ikungi na Kaliua. Serikali itaendelea kuzipatia Halmashauri mpya vitendea kazi, Watumishi
pamoja na kujenga miundombinu muhimu hatua kwa hatua.
MASUALA MTAMBUKA
Vita
Dhidi ya Rushwa Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuchukua
hatua mbalimbali katika kukabiliana na tatizo la rushwa kwa kuelimisha Umma kuhusu
athari za Rushwa, kuziba mianya ya rushwa na kuwasihi Wananchi kujiepusha na
vitendo vya rushwa. Aidha, Vyombo vya Dola vimechunguza tuhuma za makosa ya Rushwa
na kuwafikisha watuhumiwa mbele ya Vyombo vya Kisheria. Hadi kufikia Desemba 2012,
tuhuma 2,911 zilichunguzwa ambapo uchunguzi wa tuhuma 390 umekamilika na Kesi 121
zimefunguliwa Mahakamani. Katika mwaka 2013/2014, TAKUKURU itaendelea na uchunguzi
wa tuhuma zilizopo na mpya zitakazojitokeza, kuendesha Kesi nyingine zilizopo Mahakamani
na zitakazoendelea kufunguliwa kutokana na kukamilika kwa chunguzi mbalimbali. Serikali
pia itaendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu athari za rushwa.
Maafa Mheshimiwa Spika, changamoto kubwa iliyoikumba Nchi yetu kwa mwaka 2012/2013
ni ukame uliosababisha upungufu mkubwa wa Chakula katika baadhi ya maeneo
Nchini. Kutokana na hali hiyo, Serikali ilifanyaTathmini za kina za Hali ya Chakula
na Lishe Nchini na kubaini kwamba Watu 1,615,440 katika Halmashauri 47 Nchini wanahitaji
msaada wa chakula. Katika kukabiliana na hali hiyo, kuanzia mwezi Julai 2012 hadi
Machi 2013, Serikali imetoa Tani 69,452 za chakula cha msaada chenye thamani ya Shilingi
Bilioni 26.39 kwa walengwa katika maeneo yenye upungufu. Serikali pia imetoa Shilingi
Bilioni 4.6 kwa ajili ya usafirishaji wa chakula hicho.
Mheshimiwa Spika, katika kurejesha hali ya kawaida kwa waathirika wa Mabomu
eneo la Gongolamboto, Serikali imekamilisha ujenzi wa Nyumba 36 eneo la Msongola Wilayani
Ilala na Nyumba moja eneo la Mbweni Wilayani Kinondoni. Zoezi hilo kwa ujumla
limegharimu kiasi cha Shilingi Bilioni 1.75. Nyumba hizo ambazo zimewekewa huduma
za msingi za maji na umeme zilikabidhiwa kwa walengwa na Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho
Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tarehe 11 Desemba 2012.
Mheshimiwa Spika, itakumbukwa kwamba mafuriko yaliyotokea Dar
es Salaam mwezi Desemba 2011 yalisababisha Kaya 1,007 za waathirika waliokuwa wanaishi
katika maeneo hatarishi zaidi kuhamishiwa katika eneo la Mabwepande Wilayani Kinondoni.
Serikali kwa kushirikiana na wadau imeendelea kuwapatia huduma mbalimbali za kijamii
na kuwajengea miundombinu muhimu ikiwemo barabara, maji, umeme, shule, zahanati
na Kituo cha Polisi. Aidha, hivi karibuni Serikali imetoa Mifuko 100 ya Saruji
kwa kila Kaya ili kuziwezesha kujenga nyumba bora na za kudumu. Napenda kutoa wito
kwa Wananchi ambao bado wanaishi mabondeni kuhama ili kuepuka athari zinazoweza kuwapata.
Aidha, Mamlaka za Serikali za Mitaa Nchini ziendelee kutenga maeneo yenye usalama
kwa ajili ya kuwahamisha wananchi wanaokaa katika maeneo hatarishi.
Dawa
za Kulevya Mheshimiwa Spika, biashara na matumizi ya Dawa haramu
za Kulevya bado ni tatizo Nchini. Hali hii inadhihirishwa na idadi kubwa ya watumiaji
walio mitaani na wale wanaojitokeza kupata tiba. Hata hivyo, kutokana na jitihada
kubwa zinazofanywa na Serikali kwa kutumia Kikosi Kazi Maalum cha Kitaifa cha Udhibiti
wa Dawa za Kulevya, jumla ya Kilo 255 za Heroin na Kilo 151 za Cocaine zilikamatwa
mwaka 2012 na Watuhumiwa 45 walikamatwa. Vilevile, jumla ya Ekari 184 za Mashamba
ya Bangi na Kilo 3,200 za Bangi kavu ziliteketezwa na Kilo 4,840 za mirungi zilikamatwa.
Katika kipindi hicho, Waathirika wa Dawa za Kulevya wapatao 20,426 walijitokeza katika
Vituo mbalimbali vya tiba. Hospitali ya Taifa ya Magonjwa ya Akili ya Mirembe imekuwa
ikipokea wastani wa Waathirika 400 kila mwaka.
Mheshimiwa
Spika, katika mwaka 2013/2014, Serikali itakamilisha Sera ya Taifa ya Udhibiti wa
Dawa za Kulevya Nchini na kuandaa Mkakati wake wa Utekelezaji. Serikali pia itaendelea
kutoa elimu kwa umma juu ya madhara ya Dawa za Kulevya na kupanua huduma za matibabu
kwa waathirika wa Dawa za Kulevya. Wito wangu kwa jamii nzima ni kuendelea kupambana
kwa nguvu zote na tatizo la biashara na matumizi ya dawa za kulevya ili kunusuru vijana
wetu. Wasafirishaji na watumiaji wa dawa hizo tunaishi nao mitaani na ni wajibu wa
kila mmoja wetu kuwabaini na kutoa taarifa katika Vyombo vya Dola.
Ustawishaji
Makao Makuu Dodoma Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012/2013, Serikali
imeendelea kuimarisha miundombinu ya Manispaa ya Dodoma kwa kujenga barabara zenye
jumla ya Kilometa 20.6 kwa kiwango cha lami katika maeneo ya Kisasa, Chang'ombe, Kikuyu
na Area A. Aidha, imekarabati mtandao wa maji wenye urefu wa Kilometa 17.5 na kusambaza
umeme wa msongo mkubwa wenye urefu wa Kilometa 13.5 katika eneo la uwekezaji la Njedengwa.
Vilevile, Viwanja 1,098 vimepimwa katika maeneo ya Ndachi, Ilazo C-centre, Nala Mizani,
Mwangaza, Ipagala, Kizota Relini pamoja na lyumbu New Town Centre.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Serikali imepanga kukamilisha
ujenzi wa Barabara kwa kiwango cha lami katika maeneo ya Kisasa, Chang'ombe, Kikuyu
na Area A. Vilevile, itaendelea na ujenzi wa Barabara kwa kiwango cha lami, usambazaji
wa umeme wa msongo mkubwa pamoja na usambazaji wa mabomba ya maji safi katika eneo
la Uwekezaji la Njedengwa. Pia, itapima Viwanja vipya 4,476 katika maeneo ya Nzuguni,
Mkonze, Ndachi na maeneo ya Viwanda. Pamoja na kazi hizo, kazi iliyoanza ya kuimarisha
utendaji wa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma itaendelea.
HITIMISHO Mheshimiwa Spika, nimeelezea kwa muhtasari baadhi ya shughuli ambazo Serikali
imetekeleza kwa kipindi kilichopita. Aidha, nimetoa Mwelekeo wa Kazi zitakazofanyika
mwaka 2013/2014. Kwa kuhitimisha, napenda kusisitiza mambo machache yafuatayo:
Matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 yameonesha kuna ongezeko
la watu Milioni 10.1 kutoka watu Milioni 34.4 mwaka 2002 hadi Milioni 44.5 mwaka 2012,
sawa na ongezeko la Asilimia 30. Ni dhahiri ongezeko hilo kubwa linahitaji juhudi
za pamoja kati ya Serikali, Sekta Binafsi, Wadau wa Maendeleo na Wananchi kwa ujumla
kuongeza uwekezaji katika huduma mbalimbali za kiuchumi na kijamii. Rai yangu kwenu
ni kuzitumia takwimu hizo kikamilifu katika kupanga mipango ya maendeleo kwa ajili
ya watu wetu.
Tumebakiza miaka takribani 12
kabla ya kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025, miaka miwili kufikia
malengo ya Maendeleo ya Milenia na miaka miwili ya kukamilisha utekelezaji wa Mpango
wa Kwanza wa Miaka Mitano. Mfumo mpya ulioanzishwa na Serikali wa kufuatilia na kusimamia
kikamilifu utekelezaji wa miradi ya kipaumbele na kufanya tathmini ya mara kwa mara
ya kupima matokeo utasaidia kuharakisha kufikiwa kwa malengo hayo mapema. Serikali
itahakikisha kwamba Mfumo huo unaimarisha uwajibikaji na kuleta matokeo makubwa na
ya haraka katika kipindi kifupi.
Jitihada
za Serikali ya Awamu ya Nne katika kuvutia uwekezaji katika kilimo hususan katika
Ukanda wa Kilimo wa Kusini mwa Tanzania (SAGCOT) zimeleta mwamko na matumaini makubwa.
Azma ya Serikali ni kuona kwamba Wawekezaji wakubwa wanashirikiana kwa karibu na wakulima
wadogo ili waweze kuondoka kwenye kilimo cha kujikimu na kuingia katika kilimo cha
kisasa chenye tija na cha kibiashara. Nawahakikishia Watanzania wote kwamba upatikanaji
wa ardhi iliyopimwa kwa ajili ya Mkulima mdogo ndicho kipaumbele cha Serikali.
Mchakato wa kuandaa Katiba Mpya umeingia katika hatua ya kuunda
Mabaraza ya Katiba katika ngazi mbalimbali yatakayopitia Rasimu ya Katiba Mpya na
kutoa maoni. Tume baada ya kuzingatia maoni ya Mabaraza itaandaa Rasimu ya Katiba
Mpya itakayowasilishwa katika Bunge Maalum la Katiba. Natoa wito kwa wananchi watoe
ushirikiano kwa Tume iweze kukamilisha zoezi hilo muhimu kwa ufanisi na kwa wakati.
Amani iliyopo Nchini imetujengea heshima kubwa katika Bara la Afrika
na Duniani kote. Sote tuna wajibu wa kuienzi na kuisimamia isitoweke. Serikali ya
awamu ya Nne itahakikisha kwamba Amani na umoja wa Kitaifa vinadumishwa ili kuwawezesha
Wananchi kuendelea kufanya shughuli zao za maendeleo bila hofu. Serikali haitavumilia
kuona mtu au kikundi cha watu wenye dhamira mbaya wakivuruga Amani, Umoja na Mshikamano
uliopo Nchini kwa kisingizio chochote. Sote tuna wajibu wa kuheshimu utawala wa Sheria,
Kanuni na Taratibu zilizopo.
Mheshimiwa Spika, kabla
ya kumaliza Hotuba yangu, nimwombe Mheshimiwa Hawa Abdulrahman Ghasia (Mb.), Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa atoe maelezo
ya Mapitio ya Kazi zilizofanyika katika mwaka 2012/2013 na Mwelekeo wa Kazi za Tawala
za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa mwaka 2013/2014.
SHUKRANI Mheshimiwa
Spika, nitumie fursa hii sasa kuwashukuru Mawaziri na Naibu Mawaziri kwa ushirikiano
walionipa katika kipindi hiki. Aidha, nawashukuru Watumishi wote wa Serikali na Taasisi
zake chini ya Uongozi wa Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Yohana Sefue kwa kusimamia
Shughuli za Serikali vizuri. Nawashukuru Watanzania wote na Washirika wetu wa Maendeleo
kwa michango yao ambayo imewezesha Serikali kutoa huduma mbalimbali kwa Wananchi.
Mheshimiwa Spika, vilevile, napenda kuwashukuru
Mheshimiwa Dkt. Mary Michael Nagu, Mbunge wa Hanang, Waziri wa Nchi (Uwezeshaji
na Uwekezaji); Mheshimiwa William Vangimembe Lukuvi, Mbunge wa Ismani, Waziri wa Nchi
(Sera, Uratibu na Bunge); Mheshimiwa Hawa Abdulrahman Ghasia, Mbunge wa Mtwara Vijijini,
Waziri wa Nchi, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa; Mheshimiwa Aggrey Joshua Mwanry,
Mbunge wa Siha, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali
za Mitaa; na Mheshimiwa Majaliwa Kassim Majaliwa, Mbunge wa Ruangwa, Naibu Waziri,
Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Elimu) kwa ushirikiano
walionipa katika utekelezaji wa majukumu ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Nawashukuru pia
Wakuu wa Mikoa na Wilaya kwa jitihada walizoonesha katika kipindi hiki. Nawashukuru
vilevile Wafanyakazi wote wa Ofisi ya Waziri Mkuu, chini ya Uongozi wa Katibu Mkuu,
Bwana Peniel Moses Lyimo na Kaimu Katibu Mkuu, Bwana Jumanne Abdallah Sagini kwa kazi
nzuri wanayoifanya. Niwashukuru Naibu Makatibu Wakuu, Bwana Charles Amos Pallangyo,
na Bwana Alphayo Japan Kidata kwa ushauri wao wa Kitaalam ambao wamenipa mimi na Waheshimiwa
Mawaziri wa Nchi katika kipindi hiki. Nawashukuru kwa kukamilisha maandalizi yote
ya Makadirio ya Matumizi ya Fedha ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka 2013/2014.
Mheshimiwa Spika, napenda kumshukuru kwa dhati Mheshimiwa Dkt. Jakaya
Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uongozi wake mahiri na
maelekezo anayonipatia katika kutekeleza majukumu yangu. Pia ninamshukuru Mheshimiwa
Dkt. Mohamed Gharib Bilal, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mheshimiwa
Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa
ushirikiano wao mkubwa. Vilevile, ninawashukuru Waheshimiwa Wabunge, Viongozi wote
wa Kitaifa na wa ngazi nyingine zote kwa ushirikiano wanaonipa katika kutekeleza majukumu
yangu. Niwashukuru sana Wapiga Kura wangu wa Jimbo la Katavi kwa ushirikiano wanaonipa
katika kuleta maendeleo ya Jimbo letu. Nawashukuru sana!
Mheshimiwa
Spika, kwa namna ya pekee, naomba uniruhusu kutumia fursa hii kumshukuru sana Mama
Tunu Pinda na Familia yangu yote kwa kunitia moyo, kunivumilia kwa kila hali na kunipa
nguvu katika utekelezaji wa majukumu yangu ya Kitaifa. Nawashukuru sana!!
MAKADIRIO
YA MATUMIZI YA FEDHA YA OFISI YA WAZIRI MKUU, OFISI YA WAZIRI MKUU - TAWALA
ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA NA OFISI YA BUNGE YA MWAKA 2013/2014
MUHTASARI Mheshimiwa Spika, kwa muhtasari, naomba sasa Bunge lako Tukufu likubali
kuidhinisha Makadirio ya Matumizi ya Fedha kwa mwaka 2013/2014 ya jumla ya Shilingi
Bilioni Mia Moja Ishirini na Tatu, Milioni Mia Nne na Moja, na Hamsini na Tisa Elfu
(123,401,059,000); kwa ajili ya Mfuko wa Bunge, na jumla ya Shilingi Trilioni Nne,
Bilioni Mia Mbili Ishirini na Sita, Milioni Mia Moja Ishirini na Tatu, Mia Tisa Hamsini
na Nne Elfu na Mia Nane na Mbili (4,226,123,954,802) kwa ajili ya Ofisi ya Waziri
Mkuu na Ofisi ya Waziri Mkuu - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ikiwa ni Matumizi
ya Kawaida na Fedha za Maendeleo za Ndani na Nje kwa ujumla wake.
Mheshimiwa Spika, pamoja na Hotuba hii, yapo Majedwali ambayo yanafafanua
kwa kina Makadirio ya Matumizi ya Fedha ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi zake, Ofisi
ya Waziri Mkuu - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Bunge.