Miaka 50 ya Waraka wa Amani Duniani iwe ni changamoto ya kujitoa bila ya kujibakiza
kukuza na kudumisha upatanisho na amani
Baba Mtakatifu Francisko, Siku ya Alhamisi, tarehe 11 Aprili 2013 amekutana na kuzungumza
na wajumbe wa Mfuko wa Papa unaogharimia shughuli mbali mbali za kichungaji kadiri
ya matakwa na utashi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu
amewshukuru wajumbe kwa sala na matashi mema waliyomwonesha tangu alipochaguliwa kuliongoza
Kanisa.
Anatambua mchango mkubwa wa Mfuko huu katika kusaidia kusukuma mbele
utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Anawashukuru kwa namna ya pekee kwa kuchangia
maendeleo na ustawi wa Makanisa katika nchi za Kimissionari; kwa kusaidia majiundo
makini na endelevu kwa Makleri na Watawa bila kusahau msaada ambao wamekuwa wakitoa
kwa ajili ya ujenzi wa makazi na huduma kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni
mwa Jamii.
Mfuko wa Papa umechangia maboresho ya huduma ya elimu sanjari na
kutoa fursa za ajira kwa watu wengi sehemu mbali mbali za dunia. Mahitaji ya Familia
ya Mungu yanazidi kuongezeka maradufu na kwamba, wao wamekuwa mstari wa mbele katika
kuchangia jitihada za Mama Kanisa katika mapambano dhidi ya umaskini wa hali na maisha
ya kiroho unaomwandama mwanadamu katika ulimwengu mamboleo pamoja na kuchangia ukuaji
wa mshikamano wa upendo na amani.
Baba Mtakatifu Francisko anaomba kwamba,
Kumbu kumbu ya Maadhimisho ya Jubilee ya Miaka 50 ya Waraka wa Kichungaji, Pacem In
Terris, Amani Duniani, iwe ni changamoto ya kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya
kukuza na kudumisha upatanisho na amani katika ngazi mbali mbali za maisha ya mwanadamu.
Anawatakia
kheri, baraka na huruma ya Mungu, wakati huu Mama Kanisa anapoendelea kuadhimisha
Kipindi cha Pasaka, ili kiweze kuwa ni chemchemi ya furaha inayobubujika ndani mwao
kwa kutambua zawadi nyingi ambazo wamekirimiwa na Mwenyezi Mungu katika hija ya maisha
yao; daima wakitamani kuendelea kuwahudumia jirani zao wanaoogelea katika shida na
mahangaiko mbali mbali.
Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha hotuba yake kwa
kuwakumbusha wanachama wa Mfuko wa Papa kwamba, wao wanachangia kwa namna ya pekee
mshikamano wa kiroho na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Anawaomba kuendelea kusali kwa
ajili ya utumishi wake ndani ya Kanisa, lakini zaidi, waendelee kuombea toba na wongofu
wa ndani, ili uzuri na ukweli wa Kiinjili uweze kupenya akili na mioyo ya watu. Amewaweka
wanachama wa Mfuko wa Papa chini ya ulinzi na maombezi ya Bikira Maria Mama wa Kanisa
pamoja na kuwapatia baraka zake za kitume.