2013-04-10 09:36:25

Watawa nchini Taiwan wakutana na Kardinali Joào Braz de Aviz


Kardinali Joào Braz de Aviz, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume, tangu tarehe 8 Aprili hadi tarehe 18 Aprili 2013 atakuwa nchini Taiwan kwa ziara ya kichungaji, ili kutembelea na kuimarisha Jumuiya za Kitawa nchini humo, ili ziweze kutolea ushuhuda amini kwa Kristo na Kanisa lake.

Huu ni mwaliko uliotolewa na Wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume nchini Taiwan wakati huu wanapoadhimisha Mkutano mkuu sanjari na kumbu kumbu ya miaka mitano tangu alipofariki dunia Mama Chiara Lubich, mwanzilishi wa Chama cha Kitume cha Wafokolare, kumbu kumbu ambayo itafanyika hapo Ijumaa tarehe 12 Aprili 2013, kwenye Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Fu Jen, nchini Taiwan.

Alipowasili nchini Taiwan, amepokelewa na viongozi wa Kanisa na tayari ameanza kutembelea Jumuiya kadhaa za Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume ili kuangalia huduma ya upendo, haki na mshikamano inayotolewa na Mashirika haya katika sekta ya afya, elimu na huduma za kijamii. Anatumia fursa hii pia kushirikishana mawazo, mang'amuzi na vipaumbele vya Mama Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo mintarafu maisha ya kitawa.

Jumapili ijayo, tarehe 14 Aprili 2013, Familia ya Mungu nchini Taiwan, itasali kwa ajili ya nia ya kumwombea Baba Mtakatifu Francisko; ibada ambayo inatarajiwa kuwa ni kilele cha hija ya kichungaji ya Kardinali Braz de Aviz nchini Taiwan na itaadhimishwa kwenye Kanisa la Familia Takatifu. Akiwa nchini humo atapata pia fursa ya kutembelea Seminari ya Kanda, Kitivo cha Taalimungu cha Mtakatifu Robert Bellarmino.

Kardinali Braz, Jumamosi jioni, tarehe 13 Aprili 2013 anatarajiwa kukutana na kuzungumza na vijana wa kizazi kipya kama sehemu ya Maandalizi ya Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani, itakayoanza kutimua vumbi kuanzia tarehe 23 hadi tarehe 28 Julai 2013 kwa uwepo wa Baba Mtakatifu Francisko.

Wachunguzi wa mambo wanasema, kwa hakika, Rio de Janeiro, hapatatosha kama wanavyosema Waswahili. Kutokana na umbali mkubwa na gharama vijana wengi kutoka Taiwan, hawataweza kushiriki katika tukio hili la kiimani, lakini watawasindikiza wenzao kwa sala na kuendelea kufuatilia matukio haya yote kwa njia za mawasiliano ya jamii.







All the contents on this site are copyrighted ©.