Ndugu msikilizaji wa Radio Vatican, tunaendelea kukumegea utajiri uliomo kwenye ujumbe
wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika Kipindi cha Kwaresima 2013 sanjari
na Maadhimisho ya Mwaka wa Imani. Kutujuza zaidi ni Sr. Gisela Upendo Msuya. “Simameni
imara katika imani” (1Kor 16:13). Hivi ndivyo Mtume Paulo anavyowaandikia waamini
wa Korintho. Anawahimiza wasimame imara katika imani ili wasije wakapoteza zawadi
hiyo kubwa iliyo mlango wa zawadi zote za kimungu. Kanisa la Korintho lilikuwa limeanzishwa
na Mtume Paulo mnamo mwaka 51. Baada ya kupanda mbegu ya imani katika mji wa Korintho,
Paulo alikaa hapo mwaka mmoja na miezi sita (Mdo 18:11) akilijenga kanisa hili kwa
mafundisho yake. Korintho ya wakati huo ilikuwa tayari ni mji mkubwa, wenye watu wengi
na mchanganyiko, watu waliokuwa na uwezo na hadhi tofauti.
Miaka mitano
baada ya kuanzishwa kwa kanisa la Korintho, unajitokeza mpasuko mkubwa unaotishia
kutokomeza imani changa ya waamini wa Korintho. Tatizo la kwanza lilikuwa ni mgawanyiko
baina ya waamini walioanza kujiainisha kuwa ni wafuasi wa mtume huyu au yule (Rej.
1Kor 1:12-15). Ulianza pia kujitokeza ulegevu katika kufuata kanuni za ibada (1Kor
11:17-18); na utepetevu wa kimaadili (1Kor 1:12-15; 5:1-5; 6:12-20). Msingi wa imani
ulipotikiswa, wakristo wa Korintho walifikia hatua ya baadhi yao kuanza kupinga ufufuko
(1Kor 15:12). Katika hali hii ya upotofu ulioanza taratibu kuota mizizi. Mtume Paulo
anasimama kidete kuwakumbusha kuwa “kama Kristo hakufufuka, basi, kuhubiri kwetu ni
bure na imani yenu ni bure” (1Kor 15:14). Mtume Paulo analihimiza Kanisa lirudi katika
njia ya misingi ya imani aliyokuwa amewafundisha. Anawaambia Wakristo wa Korintho
wakeshe na kusimama imara katika imani (Rej. 1Kor 16:13). Matatizo na migogoro
iliyokuwa inalikabili Kanisa la Korinto ilitishia kuua imani changa ya waamini wa
Korintho. “Kwa vipimo vya kibinadamu hali ya Korintho haikuwa na rutuba nzuri kwa
upandaji wa imani na maadili ya kikristo, lakini kisichowezekana kwa akili ya binadamu,
kiliwezekana kwa nguvu ya Mungu.” Paulo anayatafutia ufumbuzi matatizo ya jumuiya
hii akijengea yote juu ya msingi wa imani.
Imani maana yake ni nini? Imani
ni zawadi tunayopata kutoka kwa Mungu. Zawadi hii inakuwa ndilo jina la uhusiano kati
ya Mungu na mwanadamu katika mpango wa ukombozi. Kwake yeye aliyepokea zawadi na jina
hili, imani inabeba maana yake halisi; yaani, imani, “ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo,
ni bayana ya mambo yasiyoonekana” (Ebr 11:1). Hii ni hali ya mwanadamu kuinua moyo
na akili yake kumwelekea Mungu na ahadi zake, kwa maana sisi tunaomwamini Mungu “twaenenda
kwa imani, si kwa kuona” (2Kor 5:7).
Haya
mambo “yatarajiwayo” na “yasiyoonekana” si nadharia isiyokuwa na msingi. Haya mambo
“yatarajiwayo” na “yasiyoonekana” ni tamanio la kuishi katika muungano na Mungu, Mungu
ambaye tumekwishamuona katika nafsi yake ya pili; yaani, katika Yesu Kristo. Kama
Yesu mwenyewe anavyosema, “Aliyeniona mimi amemwona Baba” (Yn 14:9), kwa sababu imani
“ni jibu la mtu kwa Mungu ambaye anajifunua mwenyewe na kujitoa mwenyewe kwa mwanadamu.”
Uhusiano huu mpya kati ya Mungu na mwanadamu ambao kwa njia ya Ubatizo, mwanadamu
anafanyika kuwa mwana wa Mungu, unatuwezesha kutembea katika imani ya yale tunayoyatarajia
katika ulimwengu ujao.
Neno
la Mungu na Sakramenti zake zinatufunulia njia za imani na zinakuwa ni hakikisho la
kile tunachokiamini. Na kama anavyosema Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili, “Kwa kusadiki
na kujikabidhi kwa Mungu, tunaitikia neno la Mungu.” Mt. Ambrose anapowafundisha Wakristo
wapya waliobatizwa mabadiliko yanayoendana na Sakramenti ya ubatizo waliyoipokea anasema:
“Hapo awali mliona kwa macho ya mwili, sasa mnaona kwa macho ya moyo.” Hivi ndivyo
wale wote waliompokea Yesu kama Bwana na Mwokozi wao wanavyotakiwa kuishi na kutembea
kuelekea Ufalme wa Mungu. Kuona huku kwa macho ya moyo ndiyo kuona kwa imani. Hii
ndio kusema anayeamini ameamua kujikabidhi kwa Mungu na anaahidi kuishi kiaminifu
kadiri ya matakwa ya Neno la Mungu na ahadi zake. Tendo hili la imani kuu ya kusadiki
pasipo kuona (Rej. Yn 20:29) lina tuzo lake, kama anavyotusaidia kung’amua Mt. Agostino
anaposema: “Imani ni kuamini kile usichokiona, na tuzo ya imani hii ni kuona kile
ulichoamini.”
Imani
ndio inayotupatia hakikisho la msingi ambalo juu yake tunayasimika maisha yetu yote.
Imani inakuwa ni mlango usioweza kufungwa na yeyote. Kama tunavyosoma katika waraka
wa sita kati ya nyaraka saba zilizoelekezwa kwa makanisa, kanisa la Filadelfia wanaambiwa:
“Tazama, nimekupa mlango uliofunguliwa mbele yako, ambao hapana awezaye kuufunga”
(Ufu 3:8). Mlango huu daima uko wazi na kwa neema ya Mungu kila mtu anaweza kuupitia,
iwapo tutakuwa tayari “kurekebisha maisha yetu kuendana na ukweli wa ulimwengu mpya.”
Kanisa katika Mwaka
huu wa imani linatuelekeza pia kukua katika imani kwa njia ya tafakari na kujifunza
kwa kina Kanuni ya Imani; yaani, imani tunayoikiri. Kwa njia ya Sakramenti; yaani,
imani tunayoiadhimisha. Kwa njia ya Amri Kumi za Mungu; yaani, imani tunayoiishi.
Na kwa njia ya tafakari ya Sala ya Bwana; yaani, imani tunayoisali. Hivi ndivyo mafundisho
ya Katekisimu ya Kanisa Katoliki yalivyopangwa na kubainisha kwa ufasaha mkubwa muhtasari
wa namna mkristo anavyotakiwa kuishi.