2013-04-10 11:41:24

Miaka 366 tangu Chuo Kikuu cha Urbaniana kilipoanzishwa, changamoto ya kuendeleza utume wake, kwa kuwa waaminifu kwa Kristo na Kanisa lake


Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu katika Maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu kwa Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kipapa cha Urbaniana, Jumatano tarehe 10 Aprili 2013, Sherehe ya Chuo Kikuu cha Kipapa cha Urbaniana, ambayo kimsingi ilipaswa kufanyika Kanisa lilipokuwa linaadhimisha Kumbu kumbu ya Bikira Maria kupashwa habari kwamba, atakuwa ni Mama wa Mungu, amekumbushia yale yaliyojiri miezi kadhaa iliyopita.

Anasema, hivi karibuni Kanisa limekumbwa na matukio kadhaa katika maisha na utume wake: Jambo la kwanza ulikuwa ni mshtuko ambao uliwakumba waamini wengi waliposikia nia na utashi wa Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, kung'atuka kutoka madarakani. Kukafuatiwa na mchakato wa kumtafuta Kiongozi mpya ambaye angeendeleza kazi ya kitume ya Mtakatifu Petro.

Makardinali wakaanza mchakato huo kwa mikutano elekezi na hatimaye, wakaingia kwenye Conclave na kumchagua Papa Francisko. Haya ni matukio ambayo yamekuwa na mguso mkubwa katika maisha na utume wa Kanisa katika ujumla wake.

Kardinali Filoni anasema, alipokutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko alimkaribisha kutembelea Chuo Kikuu cha Kipapa cha Urbaniana na taasisi zake, ambacho kwa mwaka huu kinaadhimisha Miaka 366 tangu kilipoanzishwa. Kimekuwa mstari wa mbele katika kutoa majiundo kwa Majandokasisi, Mapadre na watawa kutoka katika nchi 120, wakiwa na utajiri wa tamaduni wanakotoka. Anawapongeza Wanajumuiya ya Urbaniana inayoundwa na Majaalim, Wanafunzi na Wafanyakazi, bila kuwasahau wafadhili wanaojitoa kwa hali na mali kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Chuo cha Kipapa cha Urbaniana.

Kardinali Fernando Filoni anawaalika wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kipapa cha Urbaniana kujifunza kutoka kwa Bikira Maria, mwalimu wa taalimungu makini, Tabernakulo ya kwanza ya Neno wa Mungu aliyefanyika mwili; Mama mwenye imani na mapendo thabiti kwa ndugu na jirani, kama sehemu ya utekelezaji wa Historia ya Ukombozi wa mwanadamu. Ni mwaliko na changamoto kwa Jumuiya hii kujitosa kimaso maso kuwaendelea wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jami kutokana na ujinga, umaskini na maradhi.

Huu ni wito wa kichungaji unaotolewa na Baba Mtakatifu Francisko kwa sasa. Chuo Kikuu cha Kipapa cha Urbaniana kinapaswa kuendelea na utume wake kwa kuwasaidia wanafunzi kukua na kuimarisha imani pamoja na kuwaandaa Wamissionari wapya watakaotoka kifua mbele kutangaza Injili ya Kristo wakiendelea kuwa waaminifu kwa Kristo na Kanisa lake.







All the contents on this site are copyrighted ©.