2013-04-10 15:48:05

Mateso, kifo na ufufuko wa Yesu Kristo ni kiini cha Imani ya Kanisa


Siku ya tatu alifufuka kutoka katika wafu, ni sehemu ya Kanuni ya Imani ambayo Baba Mtakatifu Francsiko ametafakari pamoja na waamini, mahujaji na wageni waliofika mjini Vatican siku ya jumatano, tarehe 10 Aprili 2013 ili kusikiliza Katekesi yake kama sehemu ya mwendelezo wa Katekesi za Maadhimisho ya Mwaka wa Imani. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kujitaabisha kufahamu kwa kina maana ya ufufuko katika maisha na kwa ajili ya wokovu.

Mateso, kifo na ufufuko wa Yesu anasema Baba Mtakatifu ni kiini cha Imani ya Kanisa, kwani ni matendo yanayoonesha ushindi wa Kristo dhidi ya dhambi na mauti na kwa njia hii, Kristo anawafungulia waamini njia ya maisha mapya. Kwa kuzaliwa upya katika Sakramenti ya Ubatizo; waamini wanapokea mapaji ya Roho Mtakatifu na hivyo kufanyika waana wateule wa Mungu. Kwa njia hii, Mwenyezi Mungu anakuwa ni Baba yao!

Anawahudumia kama watoto wake wateule, anawafahamu fika na kuwasamehe dhambi zao wanapotopea katika dhambi, anawakumbatia na kuendelea kuwapenda hata pale wanapomponyoka. Baba Mtakatifu Francisko anakazia kwamba, Ukristo si tu kufuata amri na maagizo, bali ni changamoto ya kuwa wapya na kuishi katika upya wa maisha kwa kuwa ndani ya Kristo; kwa kufikiri na kutenda na hatimaye, kugeuzwa na upendo wa Yesu!

Maisha haya mapya hayana budi kurutubishwa kila siku kwa kusikiliza na kulitafakari Neno la Mungu, Sala, kwa kushiriki kikamilifu Sakramenti za Kanisa hasa Sakramenti ya Upatanisho na Sakramenti ya Ekaaristi Takatifu inayomwilishwa katika Matendo ya Huruma. Mwenyezi Mungu anapaswa kuwa ni kiini cha maisha ya waja wake.

Kwa njia ya ushuhuda wa uhuru katika maisha, furaha na matumaini yanayobubujika kutokana na ushindi wa Kristo Mfufuka dhidi ya dhambi na mauti; waamini wanaweza kutoa huduma makini duniani; kwa kuwasaidia jirani zao kuona mwanga wa ukombozi unaotoka kwa Mwenyezi Mungu.

Baba Mtakatifu akizungumza na waamini na mahujaji katika lugha mbali mbali, amewapongeza wanafunzi wa kijeshi kutoka Chuo cha Kijeshi cha NATO kwa huduma katika kukuza misingi ya amani na ushirikiano wa kimataifa. Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka katika wafu anawawezesha waamini kuwa ni watoto wateule wa Mungu, changamoto ya kuwashirikisha wengine furaha hii inayobubujika kutoka kwa Kristo mwenyewe pamoja na kuendelea kuwa wapya katika maisha ya Kikristo.

Kamwe waamini wasikatishwe tamaa na ubaya unaowazunguka bali watambue kwamba, yote ambayo wameambiwa na Kristo yanalenga kuwapatia amani ya ndani. Ulimwenguni watakuwa na dhiki, lakini wanapaswa kujipa moyo, kwani Kristo mwenyewe ameushinda ulimwengu. Amewatakia wote amani kutoka kwa Kristo Mfufuka.

Mwishoni, Baba Mtakatifu amewashukuru na kuwapongeza Maaskofu na Waamini wao wanaofanya hija ya maisha ya kiroho hapa mjini Vatican kama sehemu ya Maadhimisho ya Mwaka wa Imani. Anawatakia wafanyakazi wanaoteseka kutokana na kukosa mishahara yao kupatiwa ufumbuzi wa haraka. Hija ya waamini katika Makaburi ya Mitume iwe ni sehemu ya mchakato wa kuimarisha imani, matumaini na mapendo.

Baba Mtakatifu anawataka Vijana wajifunze kujenga utamaduni wa kusikiliza; wagonjwa wapate faraja kutoka kwa Kristo na wanandoa wapya watambue na kuona uwepo endelevu wa Mungu kati yao!







All the contents on this site are copyrighted ©.