2013-04-10 08:06:25

Kardinali Jorge Bergoglio na Maadhimisho ya Mwaka wa Imani


Kutokana na ukosefu wa usalama, amani na utulivu, watu wengi wamejikuta wanafunga milango ya nyumba na maisha yao kwa wageni na watu wasiowafahamu, ili kujihakikishia usalama wa maisha. RealAudioMP3

Mlango uliofungwa ni kielelezo makini cha maisha ya Jamii nyingi katika ulimwengu mamboleo, ni hali halisi inayoyojionesha kwa sasa na kwa siku za usoni katika kukabiliana na changamoto za maisha.

Mlango uliofungwa madhubuti ni kielelezo pia cha mtu kujifunga katika undani wa maisha yake, zile ndoto, matumaini, mahangaiko na nyakati za furaha zinafungwa na hivyo kushindwa kuwashirikisha majirani na watu wengine. Mlango uliofungwa ni kielelezo cha moyo uliofungwa pia kwa watu wengine, kiasi kwamba watu wengi zaidi wanashindwa kupita na hatimaye, kushiriki undani wa maisha ya mtu. Kimsingi, mlango uliofunguliwa daima umekuwa ni kielelezo cha mwanga, urafiki, furaha, uhuru na uaminifu.

Katika maadhimisho ya Mwaka wa Imani, waamini wanapaswa kuzitafuta tena tunu hizi msingi katika hija ya maisha yao ya imani, kwani mlango uliofungwa unaleta madhara kwa wahusika kwa kuwatenga na wengine. Mlango wa Imani, ndiyo picha iliyotumiwa na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita katika Waraka wake wa kichungaji kuhusu Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, “Porta Fidei”. Anawaalika waamini kupitia katika mlango huu ili waweze kupata mambo msingi katika maisha yao ya kiimani kwa kuanza maisha mapya.

Hivi ndivyo Kardinali Jorge Bergoglio ambaye kwa sasa ni Baba Mtakatifu Francisko alivyowaandikia waamini wake katika Maadhimisho ya Mwaka wa Imani. Mlango wa Imani ni taswira inayowarudisha waamini katika Kanisa la Mwanzo, lilipofungua malango yake hata kwa watu wa Mataifa wakabahatika kusikia Habari Njema ya Wokovu ikitangazwa masikioni mwao. Ndiyo ile picha ya Yesu anayebisha hodi katika mlango wa moyo wa kila mwamini, akimfungulia, ataweza kuingia na kukaa ndani mwake.

Imani ni neema na zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Mwamini anapopitia katika Mlango wa Imani anaanza hija ya maisha ya uzima wa milele. Kwa bahati mbaya anasema Kardinali Bergoglio kuna malango yenye mvuto na mashiko yanayowaahidia waamini mafanikio na raha tele, lakini baadaye yanakuwa ni chanzo cha kuchanganyikiwa, mahangaiko, kukata tamaa na hatimaye kupoteza mwelekeo kwa siku za usoni.

Mlango wa Imani daima uko wazi, humo Kanisa linaendelea kutangaza Habari Njema ya Wokovu na kuwakirimia waamini neema inayowaletea mabadiliko ya ndani katika maisha yao na Mlango huu ni Yesu Kristo ambaye ni njia, ukweli na uzima na kwamba, Yeye ndiye yule Mchungaji mwema aliyeyamimina maisha yake kwa ajili ya ukombozi wa ulimwengu.

Mwenyeheri Yohane Paulo wa pili alipokuwa anaanza utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, aliwaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kumfungulia Kristo malango ya maisha yao. Kw anjia ya ukarimu, wafuasi wa Emmaus waliweza kumfungulia Yesu malango ya maisha yao, akaingia na kula pamoja nao na hatimaye, wakabahatika kufafanuliwa Maandiko Matakatifu.

Mwaka wa Imani ni fursa ya kumshukuru Mungu kwa zawadi ya Sakramenti ya Ubatizo ambayo inawawezesha waamini kuwa ni wana wateule wa Mungu na ndugu zake Kristo. Maadhimisho ya Mwaka wa Imani yasaidie kujenga na kuimarisha umoja miongoni mwa Wakristo; iwe ni fursa ya kutubu na kuongoka na changamoto ya kuwa watakatifu, ili kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda makini wa imani katika matendo, ili kuweza kupata furaha ya kweli katika maisha.

Waamini wajitaabishe kuifahamu imani kwa kina na mapana; wajitahidi kuiungama kwa vinywa na matendo yao adili; kuishuhudia katika maisha na vipaumbele vyao katika maisha ya hadhara, daima wakijitahidi kuwa ni Wamissionari katika kutangaza Habari Njema ya Wokovu.

Mwaka wa Imani anasema Kardinali Bergoglio uwasaidie waamini kuweza kukabiliana na changamoto mbali mbali katika maisha na utume wa Kanisa, daima wakitambua kwamba, Mwenyezi Mungu yuko pamoja nao! Iwe ni nafasi murua ya kuboresha mawasiliano kati ya watu ndani ya Jamii; kwa kuheshimiana na kuthaminiana; kwa kupendana na kusaidiana, daima kwa kutafuta mafao ya wengi. Roho Mtakatifu awasaidie waamini kuchuchumilia haki na utakatifu wa maisha; kuendelea kurithisha imani na matumaini kwa vijana wa kizazi kipya.

Waamini wajitahidi kufanya kazi katika mazingira bora, kwa kulinda na kuheshimu utu wa binadamu, ili kila mtu aweze kupata utimilifu wa maisha. Mwaka wa Imani iwe ni fursa ya kusimama kidete kulinda na kutetea uhuru wa kidini kwa kwa kuishi na kutenda kwa haki; kwa kupenda na kutenda wema.

Mwaka wa Imani uwe ni mwanya wa kusameheana na kujenga urafiki katika tabasamu kwa kuwajali wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii; watu ambao hawana thamani mbele ya macho ya wengi! Kwani hawa ndio wale ambao Yesu mwenyewe anawaita kuwa ni ndugu zake. Ni wakati muafaka wa kuadhimisha zawadi ya maisha, ili kuungana na hatimaye, kuwa wamoja katika Kristo katika Maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, ili kujenga na kuuimarisha Ufalme wa Mungu.

Ni changanmoto na mwaliko wa kuumwilisha Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican na Mafundisho yaliyotolewa na Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Amerika ya Kusini na Caribbean; Kanisa lijitahidi kufungua malango yake kwa watu wanaoishi katika mazingira magumu lakini zaidi kwa watu wa nyakati hizi wenye kiu na hamu ya kutaka kumwona Mungu katika hija ya maisha yao, kwa kusikiliza Habari Njema ya Wokovu.

Hii ni changamoto kwa Kanisa kujikita katika utume wa Kanisa kwa njia ya ushuhuda wa maisha yanayojikita katika sala, kazi na utume, daima likiwa na mwelekeo wa Kimissionari. Maadhimisho ya Mwaka wa Imani ni nafasi ya kupyaisha maisha ya waamini katika Kristo Mfufuka.

Kardinali Jorge Mario Bergoglio katika barua yake ya Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kumwendea Bikira maria, Mama wa Mungu ili aweze kuwasindikiza katika mapambazuko mapya ya imani sanjari na kumwomba Roho Mtakatifu aweze kulishukia na kukaa na Kanisa, tayari kwenda kutangaza matendo makuu ya Mungu katika maisha ya wanawadamu.

Imehaririwa na Padre Richard Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.