2013-04-10 09:11:23

Hata katika madhulumu ya kidini na vitisho vya mabomu ya kujitoa mhanga, Wakristo bado wanatoka kifua mbele kukutana Kristo Mfalme wa Amani! Maajabu ya Mungu!


Kardinali John Onaiyekan, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Abuja, Nigeria, Jumapili ya Huruma ya Mungu, alisimikwa rasmi kama Kardinali Padre wa Parokia ya Saturni, Shahidi iliyoko mjini Roma, kielelezo cha mshikamano katika huduma na Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Katika mahubiri yake, Kardinali Onaiyekan alisema yeye yuko kati yao kama ndugu na mwenza katika hija ya maisha ya kiroho anaposimikwa rasmi kama Kardinali Padre wa Parokia ya Saturni. Yote haya ni mapenzi ya Mungu yaliyojionesha kwa namna ya pekee kwa Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, aliyemteuwa hata bila mastahili kuwa miongoni mwa wasaidizi wake wa karibu kama Kardinali.

Anasema, Maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu kiwe ni kielelezo makini cha Familia ya Mungu inayotekeleza dhamana na utume wake wa kutangaza Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia. Amewaalika waamini kuliishi tukio hili la imani kama sehemu ya mchakato wa kujenga na kuimarisha neema iliyoko ndani mwao, umoja na mshikamano wa Kikristo katika nyakati za raha na furaha, matumaini na magumu ya maisha; madhulumu na kukata tamaa, bila kusahau changamoto na fursa mbali mbali ambazo Mama Kanisa anakabiliana nazo katika mapambazuko ya Millenia ya Tatu ya Ukristo.

Ni dhamana na wajibu wao kuendelea kushikamana na katika imani, matumaini na mapendo na Baba Mtakatifu Francisko, Khalifa wa Mtakatifu Petro. Yesu Mfufuka alipowatokea mitume waliokuwa wamejifungia kwenye chumba cha juu kwa kuogopa mkong'oto wa Wayahudi, aliwapatia zawadi ya: Amani na Roho Mtakatifu pamoja na kuwajalia uwezo wa kusamehe na kuwaondolea watu dhambi zao ili waweze kuonja upendo na huruma ya Mungu isiyokuwa na kifani.

Huu ni mwaliko kwa waamini kukimbilia kwenye Sakramenti ya Kitubio ili waweze kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani zao, kwa kuitengeneza dunia ili iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi.

Kardinali Onaiyekan anasema, Maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa iwe ni fursa maalum kwa waamini kuimaarisha imani yao kwa Kristo na Kanisa lake, ili hatimaye, waweze kuwa na ujasiri wa kuitolea ushuhuda katika uhalisia wa maisha yao ya kila siku kwa maneno na matendo yao adili. Amegusia pia vitendo vya uvunifu wa misingi ya haki, amani, upendo na utulivu miongoni mwa wananchi wa Nigeria, wanaokabiliwa na vitisho vya kigaidi na madhulumu ya kidini.

Kardinali Onaiyekan anasema kwa uchungu mkubwa kwamba, hata katika vitisho na madhulumu ya kidini, watu bado wanapiga moyo konde na kutoka kifua mbele kwenda Makanisani ili kukutana na Yesu katika Sakramenti za Kanisa na katika Neno lake ambalo ni chemchemi ya uzima wa milele, kwani wanatambua kwamba, Yesu Kristo ni Mfalme wa Amani.

Upendo, shauku, hamu na ari ya kukutana na Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka katika wafu inashinda vitisho vya mabomu ya kujitoa mhanga na madhulumu ya kidini. Ndiyo maana wakristo bado wanaendelea kumiminika kwa wingi licha ya vitisho vya mabomu na mashambulizi ya kujitoa mhanga. Yote haya ni matendo makuu ya Mungu kama yalivyojionesha katika maisha na utume wa Wakristo wa Kanisa la mwanzo, wengi wao wakaamini na kujiunga na Kanisa.

Kardinali John Onaiyekan anasema hata watu wa nyakati hizi kutokana na kuwa na imani haba kama ilivyokuwa kwa Mtume Tomaso, wanatafuta uhakika wa imani yao kwa njia ya miujiza, badala ya kutumaini huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na kifani. Huu ni mwaliko kwa waamini kutambua kwamba, imani ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu na kwamba, wanapaswa kumtumaini Mungu.

Licha ya maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia, lakini mwanadamu bado anaendelea kuogelea katika dimbwi la athari za myumbo wa uchumi kimataifa; mmong'onyoko wa maadili na utu wema; vita, kinzani na migogoro ya kijamii. Waamini watambue kwamba matumaini yao yamejikita kwa Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka katika wafu na kwamba, Yeye ndiye Mkombozi wa Ulimwengu. Waamini wanapaswa kushuhudia imani yao kwa njia ya vitendo.

Jumuiya ya Waamini ishirikiane kwa pamoja kuwaonjesha na kuwamegea wengine ile furaha ya kumwamini Kristo, daima wakijitahidi kutunza ile neema ya utakaso waliyoipokea wakati wa Ubatizo. Pale wanapojikuta wanaogelea na kutopea kwenye dhambi, watambue kwamba, wanayo nafasi ya kukimbilia upendo na huruma ya Mungu kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho, kwa kutambua kwamba, kamwe mwenyezi Mungu hachoki kuwahurumia watu wake, kama anavyokazia Baba Mtakatifu Francisko.

Waamini waombe huruma na upendo wa Mungu kwa ajili yao, jirani na ulimwengu kwa ujumla, ili dunia iweze kuwa kweli ni mahali pazuri zaidi pa kuishi.







All the contents on this site are copyrighted ©.