2013-04-09 07:51:59

Toleeni ushuhuda wa imani yenu kwa Kristo na Kanisa lake kwa njia ya matendo ya huruma na upendo!


Imani inapaswa kumwilishwa na kutolewa ushuhuda katika hija ya maisha ya mwamini kila siku, kama njia ya kuwashirikisha wengine ile imani inayopata chimbuko lake kutoka kwa Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka katika wafu. Kila mwamini kwa na mna ya pekee kabisa anaalikwa kuwashirikisha wengine ile furaha ya Kristo mfufuka, ili kwa pamoja waweze kupata tuzo la maisha ya uzima wa milele.

Ni changamoto ambayo imetolewa na Monsinyo Brian Wells, kiongozi mwandamizi kutoka Sekretarieti ya Uongozi wa Vatican kwa wanashirika wa vyama vya Mtakatifu Petro na Paulo, katika Ibada ya Misa Takatifu, iliyoadhimishwa, Jumapili iliyopita, kwa kutolea sadaka hii kwa Bikira Maria Mama wa Mungu. Wanachama wa vyama hivi wamerudia tena ahadi yao ya uaminifu na mshikamano na Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Monsinyo Wells, katika mahubiri yake amewapongeza wanachama hao kutokana ma chango mkubwa wanaoutoa kwa njia ya majitoleo yao kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa miongoni mwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii. Anasema kwa njia ya sadaka na majitoleo yao, watu kutoka sehemu mbali mbali za dunia wanaweza kuonja upendo na huruma ya Mungu kwa kukutana na Yesu Mfufuka katika maisha na utume wa Kanisa.

Hii ndiyo changamoto kwa waamini kuhakikisha kwamba, wanashuhudia katika maisha ile imani tendaji, kama njia ya kutangaza Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia. Fumbo la Pasaka linakamilisha mpango wa Mungu uliojionesha kwa mara ya kwanza katika kazi ya Uumbaji. Kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wa Kristo, mwanadamu aliyekuwa anaogelea katika dimbwi la dhambi na mauti anakombolewa na kupewa hadhi ya kuitwa tena mwana mpendwa wa Mungu. Yesu Kristo ni kielelezo cha huruma na upendo wa Mungu kwa mwanadamu.

Monsinyo Bryan Wells akizungumzia kuhusu uhaba wa imani ulioonesha na Mtume Tomaso kiasi cha kushangazwa na Yesu alipokutana naye uso kwa uso, ni kielelezo cha waamini wengi wanaotangatanga kwa kukosa msingi imara wa imani kwa Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka. Yesu anawaalika wafuasi wake kumwangalia kwa jicho la imani, ili kutambua na kuonja uwepo wake katika maisha na utume wa Kanisa; wanapolisoma na kulitafakari Neno la Mungu na hatimaye kulimwilisha katika maisha.

Waamini wanaonja uwepo wa Kristo wanaposhiri kikamilifu katika Sakramenti za Kanisa, lakini kwa namna ya pekee, wanapotoa muda wao kwa ajili ya kumwabudu Yesu katika Sakramenti ya Ekaristi Takatifu na wanapomshiriki, ili hatimaye, kuwaonjesha wengine ule upendo wa Kristo kwa waja wake.







All the contents on this site are copyrighted ©.